Chaka la Majanga

Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version

Ziwani Viktoria, ndipo nitapoanzia
Si vifo vya malaria, katika hii tanzia
Kwa kina kifikiria, tukiri wamesinzia
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Mamia walifariki, kwa uzembe narudia
Chombo hawakuhakiki, kushusha walozidia
Wakaja kutudhihaki, janga halitorudia
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Hili limeshatokea, tumepoteza mamia
Jingine likitokea, kikosi kimetimia
Tume zimetokomea, ripoti mwaatamia
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Majini hii ya tatu, nikiwa na ufahamu
Wanakufa ndugu zetu, wenye yao majukumu
Vyombo vyazidisha watu, wapate pesa haramu
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Kikosi cha uokozi, Bukoba tulililia
Wachache pasi ujuzi, vifaa wanalilia
Posho mwatoa machozi, wengine mkisinzia
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Magari wanotumia, milioni miambili
Posho zisipotimia, mwasaini mara mbili
Tabibu kataka mia, eti potelea mbali
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Treni ikajatuliza, hatuwezi kusahau
Wakaja kutuliwaza, kwa misemo na nahau
Tume ikawa ya kwanza, ripoti zao sahau
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Mabomu kule Mbagala, yakatutenda vilivyo
Kama ada wakalala, na kauli hovyo hovyo
Mjengoni wakalala, yakaja Gongolamboto
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Kwenye majanga ya moto, nako kuna muchemusho
Kikosi cha zimamoto, kikija huwa cha mwisho
Maigizo ya kitoto, ni shoo na machapisho
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Barabara usiseme, ajali haina kinga
Takwimu msiziseme, zinatuchoma upanga
Nimizani tuiname, konda aja kutupanga
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Toka Dar hadi Mwanza, vipi ndugu usimame
Mchomoko pita kwanza, ili mizani tupime
Umma badilika kwanza, ajali hizi zikome
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Tumejenga mabondeni, ajali haina kinga
Mabwepande ni porini, siendi sijajipanga
Tumebanana Jangwani, zikija mvua wahanga
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Wahandisi wa majengo, wanaweza kunipinga
Ardhi isiyo kiwango, itibu kabla kujenga
Lisije kushuka jengo, ajali haina kinga
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Kauli tusipopinga, tutaongeza majanga
Eti Mungu amepanga, tutawajali wahanga
Wana mapesa ya kanga, kampeni waje honga
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

Ajali haina kinga, humo wamejifichia
Wezi leo mwawakinga, wa EPA umeachia
Tunaweza kujikinga, mkiacha chikichia
Ajali haina kinga, chaka lao la majanga.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)