Chambo cha Nishati na Madini chanasa wengine


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

FEBRUARI 7, 2008 Baraza la Mawaziri lilipovunjika. Hayo yalikuwa matokeo ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Kwa kuondoka waziri mkuu maana yake kila waziri aliondoka, na kwa maana hiyo, serikali ilianguka bungeni.

Takribani miaka minne baadaye janga jingine linalotaka kufanana na la Februari mwaka 2008 limetokea. Serikali imefurushwa bungeni tena si na wabunge wa kambi ya upinzani tu, bali pia na wabunge wa chama tawala, CCM, kama ilivyokuwa mwaka 2008. Tatizo ni lilelile, umeme!

Juzi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alijikuta katika wakati mgumu. Alifikishwa hapo na wabunge walipokutana kama kamati ya wabunge CCM. Maneno makali yalizungumzwa, walinyoosheana vidole. Kisa? Umeme! Ilianza kama mzaha Ijumaa ya Julai 15, baada ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kueleza kutokuridhishwa na mwenendo mzima wa serikali, hususan Wizara ya Nishati na Madini kushughulikia dharura ya umeme wa mgawo ambao umetangazwa kuwa ni janga.

Ni dhahiri, hamkani si shwari tena ndani ya Wizara ya Nishati na Madini kama ilivyokuwa mwaka 2008. Kwa hali ilivyo, Katibu Mkuu, David Jairo, ni kama hana kazi, anayesubiriwa kutamka ni Rais Jakaya Kikwete aliyemteua; hana jinsi atamtimua tu. Hii ni kutokana na kubainika kuhusika katika kuchangisha taasisi zilizo chini yake kila moja kiasi cha Sh. 50 milioni ili kufanikisha kupitisha bajeti ya wizara hiyo.

Zahama yote hii ni ya nini? Na ni kwa nini ni umeme tu? Ni bahati mbaya kwamba umeme umekuwa mwiba mkali kwa serikali ya awamu ya nne kiasi kwamba haiwezi kujiondoa kwenye kabali hiyo kali. Hali hii ndiyo msingi wa uchambuzi wangu kwa leo.

Ukitafakari kwa kina sana matatizo ya umeme wa nchi hii hata kama una historia katika kile kinachoitwa kujikita zaidi katika chanzo kimoja kwa asilimia zaidi ya 55, yaani maji, bado rushwa na ufisadi katika sekta hiyo imekuwa kansa ambayo asilani haitawaacha wakubwa wa serikali yetu salama kwa kipindi kirefu kijacho.

Si jambo la bahati mbaya, kwa mfano, mikataba mingi ya umeme kuwa na migogoro na utata mwingi; kuanzia ule wa IPTL; Richmond na Dowans; Pan African Energy na mgogoro wa kulipa kodi; Agrekko, Kiwira ya Mkapa kutaja kwa uchache tu, ni matokeo ya mkao wa ulaji kwenye sekta ya nishati.

Mwezi uliopita kulikuwa na tuhuma zilizotanda kwamba kabla ya wabunge wa kamati ya Nishati na Madini ya Bunge kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, kulikuwa na fedha zimetembea. Wajumbe walihongwa katika mazingira ya siri siri hivi!

Kamati ilijaribu kuzima tuhuma hizo kwa kuendesha vikao vya ndani. Kwa kuamini kwamba dhambi hiyo imefutika, wizara husika iliendelea na mbinu zake chafu, kusaka fedha za kuhonga watu aghalabu wabunge ili kulainisha mambo.

Mungu amekaa juu ya Watanzania, amesikia kilio chao, ameona jinsi wanavyochezewa na viongozi waliopewa dhamana kwa ajili ya kuleta umeme, maji, kujenga barabara, shule, kutoa huduma za afya, elimu na kila huduma; sasa ameamua kuwaumbua.

Michango ya Sh. milioni 50 kutoka taasisi mbalimbali zinazosimamiwa na Wizara ya Nishati na Madini, imetukumbusha tena somo la mwaka 2008. Uwajibikaji kwa mujibu wa sheria, kanuni; lakini juu ya yote uadilifu!

Kwanini watu wanapenda njia za panya kufika safari yao? Jibu ni jepesi, hawataki kutoka jasho, hawataki kufikiri, hawataki kujisumbua kwa kuwa wananchi wa nchi hii wameonekana kuwa ni mabwege kama walivyo wabunge wao wengi, basi; ni ubwege kwa kwenda mbele.

Pinda alisema barua ya Jairo kwenda kwa taasisi zinazosimamiwa na wizara kuzitaka kuchanga fedha kufanikisha upitishwaji wa bajeti hauna utetezi wa aina yoyote.

Maana ya kauli ya Pinda ni kwamba rushwa ndiyo kitu pekee nyuma ya kukusanywa kwa michango hiyo. Hizo ni mbinu chafu; ni hatua mbaya na chafu kwa kila aina ya lugha, kwamba wizara inakusanya fedha ili bajeti yake ipitishwe. Fedha hizo zinatoka katika fungu gani katika taasisi hizo na kwa ajili ya nini? Jibu ni jepesi mno. Kuhonga!

Ni vigumu kupata majibu ya mbinu hizi. Taarifa za ndani zinasema kwamba, chini ya utaratibu huo zimepatikana Sh. 1.05 bilioni kwa ajili ya kufanikisha kupitisha bajeti ya wizara hiyo, ili bajeti ipite hata kama haitoshelezi mahitaji na changamoto za nishati ya umeme inayokabili taifa hili.

Kwamba kiongozi wa ngazi ya katibu mkuu anajisahau kiasi cha kuagiza watu wachange fedha, hakika ni kielelezo cha wazi jinsi uoza ulivyojisimika katika kina kirefu serikalini. Ni kielekezo cha uchovu wa fikra, kushindwa kubuni mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za wajibu, ni kielelezo cha dhahiri kwamba ni kwa nini kero ya mgawo wa umeme haiwezi kwisha, ni kielelezo kingine cha kwa nini mikataba mibovu haiwezi kukomeshwa.

Yaani kama katibu mkuu anawaza, njia ya kupitisha bajeti ya kuwaletea wananchi maendeleo ni kuwahonga wabunge, hivi ni kwa njia gani anaweza kuwa anasukumwa na nia ya kweli ya kuleta maendeleo? Je, waziri na naibu wake kama walijua au hawakujua, wanasema nini katika hili?

Mwezi uliopita walihonga wakakwepa kukamatwa, leo hii wameumbuka hadharani, wanajitia kuwa na uso mkavu ilihali ndani wanavuja damu mwenye mioyo yao, wanamwaga nyongo ya kutosha ndani kwa ndani, hawana pa kuwaka nyuso zao.

Nashindwa kujizuia kuwaza kwa roho mbaya zaidi, yaani Jairo kiongozi ambaye alikuwa Ikulu kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Nishati na Madini, anataka kusema kuwa barua yake kwenda kwa taasisi zilizo chini yake inamwonyesha kuwa ni kiongozi wa aina gani?

Je, yeye ni yule mkali wa kutumia filosofia ya ‘penye udhia penyeza udhia?’ Kama hivyo ndivyo, basi safari hii Mungu amekuwa wa Watanzania, Mungu amechoka kuwaona Watanzania wakiburuzwa, wakidanganywa na kuibiwa mchana kweupe, amewafichua watenda maovu hawa.

Mungu ameamua kuadhibu watendaji wa ovyo kupitia Wizara ya Nishati na Madini, ameamua kuweka utaratibu wa arobani za kila mtu kwenye wizara hii.

Hapa ndipo alipojikwaa Lowassa, akajikwaa Dk. Ibrahim Msabaha, akijikwaa Nazir Karamagi, na mlolongo mkubwa wa waliotajwa kwenye sakata la Richmond; lakini sasa kuna kila dalili kwamba wengine wataingia kwenye orodha hii.

Inawezekana kwenye sekta ya nishati na madini kuna fedha zilizo nje nje, lakini sasa Mungu ameamua kufanya sekta hiyo kuwa ni mtego wa kila alaye njama dhidi ya wana wa nchi hii. Hapa ndipo ilipo arobaini ya wenye ulaghai wote.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: