Chaneta yasaka ushindi miaka mitatu


Mohamed Akida's picture

Na Mohamed Akida - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version

MGAAGAA na upwa hali wali mkavu. Methali hiyo ya Kiswahili inafaa kutumia kuonesha namna timu ya taifa ya netiboli, Taifa Queens.

Ushindi wa medali ya shaba waliorudi nao kutoka Maputo, Msumbiji walikoshiriki Michezo ya Mataifa ya Afrika umepatikana baada ya miaka mitatu ya mazoezi na ushiriki mashindano ya kimataifa.

Desemba 2009 kikosi cha Taifa Queens kilikwenda Singapore kwa mashindano maalum yaliyoshirikisha nchi sita ambako ilishika nafasi ya nne nyuma ya Ireland Kaskazini, Scotland na Canada. Wenyeji Singapore walishika nafasi ya tano na Malaysia nafasi ya sita.

Mbali ya kushiriki mashindano hayo, Taifa Queens pia mwaka jana ilishiriki mashindano nchini Afrika Kusini ambako ilipata uzoefu mkubwa na ilijiimarisha zaidi kwa mazoezi ilipofanya ziara katika jiji la Manchester, Uingereza na baadaye ilienda Scotland itakakofanyika michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 2014.

Hadi mwaka jana wakati inafanya ziara za michezo ya kirafiki Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya 22 duniani na ya nne barani Afrika. Lakini hadi kufikia Julai mwaka huu ilikuwa imepanda hadi nafasi ya 20 kwa mujibu wa chati ya Shirikisho la Vyama vya Netiboli Duninia (IFNA).

Uzoefu iliopata katika ziara hizo umetumika kushiriki kiushindani katika Michezo ya Mataifa ya Afrika mwaka huu iliyofanyika Maputo, Msumbiji na kushika nafasi ya pili nyuma ya Uganda.

Katika michezo hiyo, Taifa Queens iliinyamazisha Botswana kwa magoli 43-35 Jumatano iliyopita hivyo kuipa heshima kubwa Tanzania.

Katika hafla ya mapokezi ya timu hiyo mwishoni mwa wiki, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi alisema, “Tunajivunia ushindi huu mkubwa kwenu na kwa nchi kwani tungeweza kabisa kurudi mikono mitupu.”

Pamoja na kujivunia ushindi huo Nchimbi anakiri, “Maandalizi yetu hayakuwa mazuri, lakini wakati mnaondoka niliwaambia kila mtu abebe silaha anayoiweza, na leo hii imedhihirika sisi ni wagonjwa tunahitaji kutibiwa.”

Katika mashindano hayo yaliyofanyika kwa mtindo wa ligi, mbali ya kuirarua Botswana pia Taifa Queens iliichapa Kenya 36-35, Ghana 94-24, Msumbiji 92-8, Zimbabwe 38-27 na Afrika Kusini 32-29. Taifa Queens ilipata vipigo viwili kutoka Zambia 46-42 na washindi wa medali ya dhahabu Uganda 52-41.

Rose Mkisi, katibu mkuu wa Chaneta akiwa amejawa furaha alisema, “Kufanya vizuri kwa timu yetu hakika ni ni matunda ya miaka mitatu. Tunafurahi tumeanza kuyapata  kwani tumeiandaa timu hii kwa muda mrefu lakini hatimaye imetuliwaza.

“Mwaka juzi tulialikwa Mancherstar, Uingereza kwa ajili ya kufanya mazoezi na tulicheza na vyuo mbaslimbali. Mwaka huo pia tulikwenda Afrika Kusini kushiriki mashindano ya Netiboli Afrika ambayo yalitupa uzoefu na pia tulikwenda Singapore kushiriki mashindano ya mataifa sita na tulimaliza katika nafasi ya nne,” anasema Mkisi.

Mkisi anasema pamoja na kurudi na medali ya shaba, mashindano hayo yalikuwa magumu ila aliwapongeza wachezaji na kocha mkuu wao Marry Protas kwa ujasiri na kuweka utaifa mbele.

Mashujaa waliorejea na medali ni Mwanaidi Hassan ‘Perreira’, Nelly Anyingisye, Pili Peter (GS), Agnes Simkonda (GA), Doritha Mbunda, Siwa Juma, Jackline Shemeza (GD), na Magreth Constantine (GK).

Wengine ni Mwanahamis Said (WA), Evodia Kazinja (C), Pascalia Kibayasa ambae ni nahodha (WD) na Faraja Malaki (WA). Mwenyekiti wa Chaneta ni Anna Bayi.

 “Tunaiomba serikali yetu na makampuni yajitokeze ili kuusaidia mchezo huu hasa kuiweka timu kambini kwa maandalizi walau mara tatu kwa mwaka ili izidi kufanya vizuri,” alisema Mkisi.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania Taifa Queens kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa yanayojumuisha timu mbalimbali za Afrika.

Taifa Queens imewahi kutamba katika mashindano ya kimataifa ilipotwaa ubingwa katika sherehe za kutimiza miaka 10 Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADCC) mwaka 1990, Gaborone, Botswana.

Tofauti na miaka hii ambapo Chaneta inahaha kutafuta fedha za kuihudumia timu, wakati ule serikali ndiyo hasa ilikuwa inahudumia kila kitu.

Wachezaji waliotwaa ubingwa mwaka ule walikuwa Zamda Masoud, Brigita Msamati, Marry Michael, Magdalena Paul, Mbuke Tubanga, Happy Zunda, Winfrida Emmanuel, Specihoza Budodi, Aisha Muhina na Joyce Lewis.

“Mwaka ule timu yetu ya taifa ilikuwa na kila sababu ya kufanya vizuri kwa sababu wizara ndio ilikuwa inahudumia kila kitu kuanzia kambi, posho za wachezaji na kila kitu na wachezaji walikuwa na ari ya kufanya vizuri kutokana na matunzo wanayopewa na Serikali,” anakumbuka aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chaneta, Anna Kibira.

Katika michezo hiyo ya Maputo, Tanzania iliwakilishwa pia na timu ya mpira wa miguu ya wanawake ‘Twiga Stars’, wanariadha na mabondia ambao wamerudi mikono mitupu.

0713 192096, mudy_akida@yahoo.com
0
No votes yet