Charles Mwera Nyanguru: Tumaini jipya la wana Tarime


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 23 September 2008

Printer-friendly version
CHARLES Mwera Nyanguru

CHARLES Mwera Nyanguru ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara. Anatafuta kofia nyingine ya chama chake. Ni ubunge.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) – ambacho ni chama cha Nyanguru, tayari kimempa idhini.

Kamati Kuu ya CHADEMA imemteua rasmi kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa kiti cha Tarime kilicho wazi baada ya mbunge wake, Chacha Zakayo Wangwe, kufariki dunia Julai mwaka huu.

“Hakuna tatizo. Nikichaguliwa nitakuwa tu nimeongeza majukumu lakini sitawajibika kujiuzulu maana inaruhusiwa,” anasema katika mahojiano na MwanaHALISI yaliyofanyika Jumapili, muda mfupi baada ya kuteuliwa.

Unaweza kudhani Mwera (49) ameanza jana harakati. Wakati mfumo wa vyama vingi unaingia, tayari alikuwa mtetezi wa haki za watu wilayani Tarime.

Mara tu alipoacha kazi Shirika la Reli Tanzania (TRC) mwaka 1987 alikofikia Ofisa Ugavi, Kituo cha Shaurimoyo, Ilala, Dar es Salaam, Mwera alirudi Tarime kuanzisha kampuni ya Mwera Investment Firm.

Alikuwa Ofisa Manunuzi na mmoja wa wakurugenzi. Baadaye walianzisha shirika la SACHITA – Save Children of Tanzania – wakilenga kupigania haki za watoto wa Tarime.

Kupitia SACHITA, wanasaidia kujenga matumaini ya maisha ya watoto kielimu, afya na stadi za maisha na wanalea wale wanaoishi katika mazingira magumu, wakiwemo walioathirika kwa ukimwi.

Taasisi hiyo imejenga kituo cha afya kinachotoa huduma kwa watoto wasio na uwezo pamoja na wananchi wa kawaida wilayani Tarime wanaolipia tiba kwa gharama nafuu.

SACHITA ambayo rais wake ni kaka yake, Peter Mwera, inatoa huduma za kliniki kupitia gari maalum. Magonjwa yanayohusika ni pamoja na malaria.

Kupitia mradi wa RFE unaoratibiwa na Tume ya Ukimwi Tanzania (TACAIDS), SACHITA inagawa dawa kwa wenye virusi vya ukimwi zinazosaidia kuwarefushia maisha au kuwawezesha kuishi kwa matumaini zaidi.

Mwera alianzia chama cha NCCR-Mageuzi kama mwanachama wa kawaida na alishiriki katika harakati nyingi za kujenga jamii. Mwaka 2004 alihamia CHADEMA baada ya NCCR-Mageuzi kulegea na kupoteza umaarufu.

“Ni chama kilichonivutia kwani kinaonyesha malengo yaliyo wazi na kina katiba inayoelekeza malengo yake hayo kwa ukombozi wa Watanzania,” anasema kuhusu CHADEMA.

Mwera aliingia katika kinyang’anyiro cha udiwani mwaka 2005. Alichaguliwa kwa zaidi ya kura 4,000 kati ya 5,000 zilizopigwa; mshindani wake wa karibu akiwa Peter Babere wa Chama cha Mapinduzi.

“Nilifurahi kuona wananchi wamenipa imani. Wamenipa jukumu la kuwawakilisha katika chombo cha maamuzi,” anasema Mwera, mzaliwa wa Kobori Kata ya Mriba, wilayani Tarime mwaka 1959.

Alionyeshwa imani zaidi 26 Julai mwaka jana alipochaguliwa kuongoza Halmashauri baada ya Rorya kutambuliwa kama halmashauri mpya. Alimshinda Sylivester Dirini wa CCM.

Anasema wananchi wanahitaji maendeleo bila kujali itikadi; kuongeza mapato na kuyasimamia vizuri ili kupata hati safi na hivyo kupatiwa ruzuku iliyokuwa imefutwa na serikali kutokana na kukithiri kwa ubadhirifu.

“Tulikuwa na vikao vingi vya mikakati. Mimi niongoze vizuri madiwani na mkurugenzi aongoze vizuri watendaji ili tupige hatua. Mikakati yetu imejibu, kwani ndani ya mwaka mmoja tunapata tena ruzuku,” anasema.

Anasema kila kata ilipatiwa mradi na baada ya wananchi kuona matunda ya uongozi mpya wa Halmashauri, waliunga mkono viongozi wao. Hivi sasa halmashauri inalipia karo wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaojiunga na shule za kata na wale wanaokwenda shule za bweni za serikali.

“Tulipata fedha za mrahaba zipatazo Sh. 140 milioni kutoka Barrick; zote tulizipeleka kwenye ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu. Kila kata ilipatiwa Sh. 7 milioni,” anaeleza.

Katika kutumia ruzuku kulipia karo watoto, Mwera anasema walilenga mambo mawili makuu: kwanza kuwapa watoto haki yao ya elimu, na pili, kuwapunguzia wazazi mzigo wa kugharamia elimu ya watoto wao.

Mpango wa kulipia karo unaendelea; mpango wa kujenga daraja linalounganisha – barabara ya Nimrito-Masanga, Kata ya Bumera, Tarafa ya Ingwe – na makao makuu ya wilaya upo tayari na zabuni imetangazwa. ASnasema umeme upo bali unahitaji kufikishwa vijijini.

Anasema amefanikiwa kupata fedha serikalini za kuweka umeme wa jua katika sekondari za Kata za Magoto, Nyang’ungu, Buruma na Mbogi.

Mgombea mteule anasema serikali ilifanya makosa kuhamisha wananchi bila ya kuwapa maeneo ya kuchimba dhahabu. Anasema wataendelea kupigania haki hiyo kwa kujenga mahusiano mazuri ya wananchi na wawekezaji.

Mbunge mtarajiwa anasema wananchi wanalima kahawa na mahindi lakini bei ni ndogo. Kwa kutumia kiwanda cha kukoboa kahawa cha Mriba amesema wanataka wakulima wapate sauti ya kuamua bei kama wanavyopata wenzao wa Kilimanjaro.

“Tunataka serikali iruhusu kilimo cha tumbaku ambacho mwaka jana kiliingiza Sh. 12 milioni katika Halmashauri, Sh. 50 milioni Serengeti na Sh. 3 milioni halmashauri ya Rorya.

Mwera anasema mpango wa kulipia karo watoto utaanzia chekechea hadi vyuo vya ufundi. “Tukilipia watoto tunashawishi wazazi kushiriki kujenga uchumi wa familia, watasaidia mapato ya Halmashauri,” anasema.

Anasema migogoro ya ardhi hasa kwenye mipaka ya vijiji, ni chanzo cha mapigano ya koo kwa koo na kuongeza kuwa atapigania usalama wa wananchi wote.

“Vita ni mambo yaliyopitwa na wakati wananchi ambao ni nguvukazi muhimu kwa maendeleo wanahitaji usalama ili kujenga uchumi,” anaeleza.

Mwera anasema ipo changamoto ya kusaidia shughuli za akinamama wanaojishughulisha na kilimo na biashara. “Tunataka kufuta unyanyasaji Tarime. Hatutaki watoto wetu wa kike wapate mimba wakiwa shuleni; sharti wawe na haki yao ya kusoma,” anasema.

Tatizo la mipaka ya mbuga na vijiji linakwamisha shughuli za wafugaji katika Kata ya Goroma na linahitaji ufumbuzi. Vijiji vya Kegonga, Imangucha na Masanga vinahusika katika hili.

“Unajua serikali inashangaza; inahamini mifugo kuliko binadamu. Mbona Umasaini kule wanafuga pamoja eneo la hifadhi Ngorongoro?” anauliza mgombea wa Chadema.

“CHADEMA tumepewa imani na wana Tarime. Ninakusudia kuanzia alipoacha marehemu mpendwa wetu Chacha Wangwe. Tutayaenzi yote aliyoyafanya mpiganaji mzuri yule,” anasema Mwera huku akitamba kuwa “tumaini jipya la wana Tarime.”

 

Wasifu:
1967/74 Nyasincha Primary;
1977/79 Sekondari ya Ifakara, Morogoro;
1980/82 Stashahada ya Uboharia, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dar es Salaam;
Kozi mbalimbali za uboharia, uandishi katika Madhara ya Mila Potofu;
Mkufunzi – Stadi za Maisha na Haki za Binadamu;
Kozi ya Clearing and Forwarding, Canada;
Mweka Hazina wa Mwera Mission Foundation;
Mkurugenzi Sekondari ya Misheni ya Mwera.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: