Chegeni: Tumepoteza uzalendo


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 03 February 2010

Printer-friendly version
Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni

"HATA kiongozi akiwa mzuri vipi, akitoka katika kundi fulani hawezi kukubalika."

Hii ni kauli isiyo ya kawaida kutoka kwa Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni (CCM), akijadili sifa mbaya inayowakabili baadhi ya viongozi katika chama chake katika mazingira ya kashfa hizi za ufisadi.

Katika mahojiano na gazeti hili majuzi, Chegeni anasema tatizo kubwa la chama tawala kwa sasa ni kulindana, na kwamba Watanzania wengi sasa wamepoteza uzalendo.

Vinginevyo, anasema, taifa lisingekabiliwa na kashfa nzito kama za mikataba tata ya Richmond, IPTL, TRL na mingine mingi inayohusu madini.

Chegeni ni miongoni mwa wabunge ambao bado wanaamini katika Azimio la Arusha lililoasisiwa na baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1967. Anasema kuzikwa kwa Azimio hilo mwaka 1992, kumesababisha matatizo mengi ya kitaifa yanayoisumbua nchi sasa.

Anasema, Azimio la Arusha ndilo liliwezesha taifa kuwa na umoja, na kwamba ingawa kuna viongozi ambao hawakuliamini, kwa sababu ya nguvu ya utendaji ya Mwalimu Nyerere, liliweza kudumu hadi alipoondoka, wasiolitaka wakabaki madarakani.

“Wale ambao hawakuliamini azimio na misingi yake, walikuwa wenzake katika utawala na utumishi wa nchi, ndio maana wakalitelekeza,” anasema.

Anaamini Tanzania ya leo inahitaji Azimio la Arusha kujijenga upya.

“Kwa kuwa Azimio la Arusha limezikwa na kuleta Azimio la Zanzibar, na sasa tunaona matatizo yaliyojitokeza ina maana tunalihitaji,” anasema.

Anasema kupitia Azimio la Arusha, raslimali za taifa zilipata ulinzi, tofauti na ilivyo sasa ambapo zinatumiwa kwa maslahi binafsi ya wahusika.

Anasema misingi ya azimio ilisaidia kuzuia matumizi mabaya ya raslimali za taifa na pale ilipotokea, waliokosa walikemewa na kuadhibiwa.

“Wale waliopatikana na tuhuma (wakati wa Mwalimu) waliadhibiwa. Leo, hali ni tofauti.”

Anasema Mwalimu Nyerere alimsema hata Rais wa wakati ule Ali Hassan Mwinyi kwa kumwambia utawala wake unanuka rushwa.

“Tatizo kubwa hapa, mimi ninaloliona ni kule wanasiasa kutofuata nyayo zake (Mwalimu Nyerere). Wengi wetu ni wanafiki na hata pale tunapojitokeza kukosoa serikali tunakuwa na sababu binafsi,” anasema.

Uongozi wa dhamira safi umekwisha miongoni mwa viongozi wengi; badala yake “ubinafsi umeshamiri.”

Anatambua taifa kuwa na wasomi wazuri wa taaluma mbalimbali, lakini anasema, baadhi yao ndio wanaofanikisha serikali kusaini mikataba mibovu na wawekezaji.

“Mikataba hii chanzo chake ni sisi wenyewe kwa kuwa walafi. Huwa tunazungumza tusichokitenda…”

Lakini Chegeni anashangaa kwanini Tanzania isiige mifano ya nchi nyingine zilizochukua hatua kali dhidi ya watumishi walafi.

“Kulindana kumezidi zaidi, ifike mahali mtu akikosea aadhibiwe, tusisubiri mahakama. Mtu anapokosea aondolewe. Kizazi hiki tunakirithisha ubaya,” anasema.

Chegeni anatoa mfano wa tatizo la malipo hewa ya walimu, na kuhoji, “nani ameulizwa?”

Anaitaja Rwanda kama nchi iliyopiga hatua kubwa kukomesha rushwa, na ambayo Tanzania inaweza kuitumia kujifunza mbinu walizotumia.

Chegeni anasema Mwalimu Nyerere alikuwa mwadilifu, alithaminiwa zaidi kutokana na roho yake ilivyo safi..

Anasema: “Tatizo lake alikuwa na huruma. Inawezekana kulikuwa na uhaba wa watu.

Alikuwa anaendesha chombo ambacho abiria wake walikuwa nje.”

Anaumia kukiona chama chake, CCM kilivyogawanyika makundi yanayohatarisha uhai wake.

Anaona hatari kwamba CCM kitazidi kuonekana dudu kubwa iwapo uongozi hautajenga nidhamu ndani ya chama.

Akizungumzia maendeleo ya jimboni kwake, Chegeni anasema kielimu alikuta sekondari tatu lakini sasa zipo 24.

Kuhusu sekta ya afya, anasema baadhi ya vituo na zahanati vimekarabatiwa, vikiwamo vituo vilivyopo kata za Bugege, Igalukilo vilivyopata msaada wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wakati kituo cha Lukungu kimepata msaada wa Ubalozi wa Uingereza.

Kituo cha Nassa kimepatiwa gari la wagonjwa linalotoa huduma mitaani na misaada zaidi inatarajiwa kutoka ubalozi huo..

Tayari visima zaidi ya 60 vimechimbwa kwa msaada wa serikali ya Japan na Marekani.

Kuhusu miradi ya umeme, anasema itafanikishwa kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).

Kwenye miundombinu ya barabara, Chegeni anasema barabara ya Lamadi–Bariadi, Maswa, Shinyanga yenye urefu wa kilomita 192 inajegwa kwa kiwango cha lami.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: