Chenge ‘wa vijisenti’ bado hajasafishwa


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
ANDREW Chenge

ANDREW Chenge, yule mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali (1995-2006), bado hajatakasika kutokana na lundo la tuhuma za ununuzi wa rada kwa “bei ya kuruka” kutoka Uingereza.

Shirika la Uchunguzi wa Makosa ya Jinai la Uingereza (SFO) linaendelea kung’ang’ania kuwa “Chenge aliishauri serikali kuridhia kutumika kwa sheria ya Uingereza katika mkataba wa ununuzi wa rada, badala ya sheria za Tanzania.”

Katika hatua nyingine, SFO wanashikilia kuwa “Chenge alikubali akaunti za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zishikiliwe jijini London, ili iwapo serikali ya Tanzania ingechelewa kulipa deni hilo na mahakama ikaamua kuwa ni lazima ilipe, basi iwe rahisi kwa kampuni ya kutengeneza zana za ulinzi ya British Aerospace (BaE) kuchukua fedha zake.”

Kwa haya mawili, Chenge hajaponyoka, taarifa za ndani na nje ya nchi zimeeleza. Kwani SFO wanasema kungetokea tatizo lolote la kisheria, mahakama za Tanzania zisingeruhusiwa kusikiliza shauri linalohusu rada, kwa kuwa hatua ya Chenge ilitwisha wajibu huo kwa mahakama ya Uingereza.

Ripoti ya SFO ambayo nakala yake anayo pia Rais Kikwete inasema,   “maamuzi haya mawili – kutumia sheria za Uingereza na kuhamishia akaunti ya BoT nje ya nchi – hayakuwa na maslahi kwa taifa wala kwa maendeleo yake kiuchumi… Chenge alihatarisha maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa kufanya maamuzi hayo.”

Makachero wa SFO wanaamini kuwa Chenge asingeweza kufanya mambo hayo makubwa bila kushawishiwa na mlungula kwa vile, “mambo hayo hayakuwa na maslahi kwa taifa na ni ya hatari.”

Mazingira hayo, na mengine kuhusu utata wa utajiri wa Chenge, yalimaanisha serikali ilitakiwa ifanye uchunguzi kuhusu kiini cha utajiri wa mwanasiasa huyo na ikibidi imfikishe mahakamani. Lakini serikali imenyamazia taarifa hiyo.

Kuhusiana na hongo ya BaE, makachero wa SFO wanaeleza katika ripoti yao kwamba Chenge alimmegea Dk. Idris Rashid, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kiasi cha dola za Marekani 600,000 (Sh. 1.2 bilioni) kwa lengo la “kumlainisha.”

Ripoti ya SFO inasema Chenge kupitia kampuni yake ya Franton Investiment Ltd., alipokea dola za Marekani milioni 1.5 (karibu Sh. 2.5 bilioni) kutoka madalali wa ununuzi wa rada hiyo iliyonunuliwa na serikali mwaka 1999.

Mwaka 1999, serikali ilinunua rada ya kijeshi kwa dola 40 milioni (zaidi ya Sh. 60 bilioni), hatua iliyopingwa kwa nguvu zote ndani na nje ya nchi. Fedha za rushwa katika ununuzi wa rada zinadaiwa kupitia akaunti ya kampuni ya Chenge iliyoko katika benki ya Barclays, tawi la Jersey, nchini Uingereza.

Taarifa zinasema ugawaji fedha za mlungula kuhusiana na rada ulifanyika kati ya 19 Juni 1997 na 17 Aprili 1998.

Taarifa hizi zinaibuka wiki mbili baada ya Chenge kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kujitangaza kuwa “mtu safi.”

Huku akikwepa kujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari, Chenge alidai hana hatia yoyote katika ununuzi wa rada hiyo; uchunguzi wa SFO kuhusu suala hilo umemalizika tokea Desemba 2010 na kwamba na tayari taasisi hiyo imemsafisha.

Chenge hakuishia hapo. Alimtuhumu hadi Balozi wa Uingereza nchini, Diana Corner akisema anaparamia vitu asivyovijua. Balozi alitoa tamko kuwa uchunguzi na kesi kuhusiana na rada vilikuwa vinaendelea na kwamba Chenge alikuwa hajasafishwa.

Katika ripoti yake ya kurasa kumi na moja, SFO wanasema, “Hatua ya Chenge kupeleka fedha kwenye akaunti ya Dk. Rashid kunaonyesha si tu alipokea mlungula kwenye suala hilo, bali pia yeye ndiye alikuwa msambazaji wa rushwa ya rada kwa wengine,” inasema taarifa ya SFO ya Machi 21 mwaka 2008.

Miezi mitatu iliyopita, ofisi ya mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Edward Hoseah alinukuliwa na mtandao maarufu wa habari duniani, WikiLeaks akisema, “Vita dhidi ya rushwa imekuwa ngumu nchini kwa kuwa Rais Kikwete analinda mapapa wa rushwa.”

Wachambuzi wa mambo wanasema hatua ya Hoseah kutuhumu Rais Kikwete kubeba watuhumiwa wakuu wa rushwa nchini, imetokana pamoja na mambo mengine yaliyoanikwa na SFO juu ya Chenge.

Inaelezwa katika taarifa ya SFO, ambayo gazeti hili lina nakala yake, kwamba imepelekwa kwa vyombo vyote vya serikali, likiwamo jeshi la polisi na ikulu.

Kwa sasa, Chenge ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mbunge wa Bariadi Magharibi na mjumbe katika kamati ya maadili ndani ya chama chake.

Hadi kufikia mwaka 1997, SFO wanaeleza katika ripoti yao, Chenge ndiye alikuwa mtu mwenye dhamana ya kuamua iwapo mkataba wa ununuzi wa rada kati ya serikali na BaE.

“Dili la ununuzi wa rada” lilianzishwa mwaka 1992 wakati wa utawala wa rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ambapo kampuni ya Siemens Plesseys System (SPS) ilikubaliana na serikali kuiuzia mtambo huo.

Hata hivyo, suala hilo halikufikia mwafaka hadi Rais Mwinyi alipomaliza muda wake wa uongozi, Oktoba 1995. Tatizo kubwa lilikiwa ni jinsi ya serikali itakavyoweza kulipa deni la rada hiyo yenye thamani ya mabilioni ya shilingi.

Mkakati wa kuingiza nchi katika mkenge wa ununuzi wa rada ulifanikiwa wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa. Mwaka 1997, Chenge ambaye wakati huo alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali, SFO wanasema, aliridhia mara moja ununuzi huo na katika mazingira yaliojaa mashaka.

Aidha, SFO ilibaini kuwa katika kipindi hicho, Chenge alikuwa akitumia anuani ya 11 Sidmonth Road, Uingereza kupitishia kile walichoita, “dili zake,” ilhali alikuwa na anuani yake binafsi nchini.

Anuani ya Chenge ilikuwa S.L.P 11958, Dar es Salaam. Nyumba ya Chenge ilikuwa Na. 546, Barabara ya Ghuba, Oyster Bay. SFO wanadai Chenge hakutumia anuani yake halisi ya Dar es Salaam kwa kuwa alijua kwa kufanya hivyo, angeweza kushtukiwa kirahisi na mamlaka za serikali wakati wa kutekeleza dili lake.

Hata maelezo ya Chenge kuhusu fedha alizonazo yanatofautiana. Wakati awali alimweleza mshauri wake wa masuala ya fedha, JO Hambro anayeishi Uingereza kuwa “utajiri huo unatokana na shughuli zake za kitaaluma na akiba aliyojiwekea yeye na mkewe Tinnah Chenge,” katika maelezo yake mengine, SFO wanasema Chenge alieleza “utajiri unatokana na urithi katika familia yake.”

SFO wanafika hadi kugundua kuwa Chenge hakuwahi hata kueleza utajiri wake wote kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kama sheria inavyoelekeza. Serikali ya Rais Kikwete haijamchukulia hatua kwa yote hayo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: