Chenge, Chikawe sasa wamjaribu Rais Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 13 July 2011

Printer-friendly version
Andrew Chenge

MRADI wa “kumtakasa” aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali (1995-2006), Andrew Chenge, kwa mara nyingine, umeshindwa. Pamoja na jitihada kubwa za washirika wa Chenge katika mradi huo, bado utakaso haujaweza kutimia.

Aliyeonekana mbele katika kutekeleza mradi wa sasa, ni Mathias Chikawe, waziri wa nchi ofisi ya rais (utawala bora). Ni baada ya wenzake wa awali, Yusuf Makamba, Sophia Simba, John Chiligati na Tambwe Hiza kushindwa kufanya kazi waliyojipa.

Chenge ambaye ni mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), hajaponyoka. Anaendelea kung’ang’aniwa na tuhuma za wizi wa fedha za rada kwa “bei ya kuruka” kutoka Uingereza, matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa maadili ya uongozi wa umma.

Si mara moja wala mbili, serikali imekuwa ikimtetea Chenge kwa kusema, “hahusiki na wizi wa fedha za rada.” Walitaka wenye ushahidi wawasilishe ushahidi wao serikalini; mara baada ya ushahidi huo kuwasilishwa, serikali itaufanyika kazi na itamfikisha mtuhumiwa mahakamani.

Katika kutekeleza mradi wa kumtakasa Chenge, wiki iliyopita, Chikawe aliliambia Bunge mjini Dodoma, “Serikali haina ushahidi wa kuwezesha Chenge kufikishwa mahakamani.” Hakuishia hapo. Akamtetea kwa kutaja raia watatu wa kigeni kuwa ndiyo wahusika wakuu katika wizi wa fedha za rada.

Naye akarudia maneno ya watangulizi wake, “…mwenye ushahidi aulete serikalini ili hatua ziweze kuchukuliwa siku hiyohiyo.” Ni kauli inayolenga kulinda mtuhumiwa na kudhoofisha jitihada za kusaka wengine.

Hata hivyo, ushahidi juu ya Chenge uko wazi. Kinachokosekana ni ujasiri wa kutenda. Kwamba fedha za rushwa katika ununuzi wa rada zilipitia akaunti ya kampuni ya Chenge iliyoko katika benki ya Barclays, tawi la Jersey, nchini Uingereza, halina utata. Hili limewekwa vizuri ndani ya ripoti ya uchunguzi wa Shirika la Uchunguzi wa Makosa ya Jinai la Uingereza (SFO).

Mbali na kupokea dola za Marekani milioni 1.5 (karibu Sh. 2.5 bilioni) kutoka madalali wa ununuzi wa rada iliyonunuliwa na serikali mwaka 1999 kupitia kampuni yake ya Franton Investiment Ltd., Chenge hawezi kukwepa tuhuma za kutapanya fedha hizo kwa washirika wake wengine.

Ni Chenge aliyemmegea Dk. Idris Rashid, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kiasi cha dola za Marekani 600,000 (Sh. 1.2 bilioni) kwa lengo la “kumlainisha.” Yote haya yameelezwa katika ripoti ya SFO na linafahamika vema serikalini na kwa Chikawe “aliyekodishwa kumtakasa” kwa sasa.

Ripoti ya SFO inasema ugawaji fedha za mlungula kuhusiana na rada ulifanyika kati ya 19 Juni 1997 na 17 Aprili 1998. Chenge aliishauri serikali kuridhia kutumika kwa sheria ya Uingereza katika mkataba wa ununuzi wa rada, badala ya sheria za Tanzania.

Si hivyo tu. Chenge alikubali akaunti za BoT zishikiliwe jijini London, ili iwapo serikali ya Tanzania ingechelewa kulipa deni hilo na mahakama ikaamua kuwa ni lazima ilipe, basi iwe rahisi kwa kampuni ya kutengeneza zana za ulinzi ya British Aerospace (BaE) kuchukua fedha zake.

Hili halikufanyika kwa nia njema na wala Chenge hawezi kusimama hadharani akalitetea; kwani pale ambako kungetokea tatizo lolote la kisheria, Chenge alizinyima mahakama za Tanzania mamlaka ya kusikiliza shauri linalohusu rada. Alikabidhi wajibu huo mahakama ya Uingereza.

Nani awezaye kubisha kuwa Chenge asingeweza kufanya mambo hayo makubwa bila kushawishiwa? Aidha, mambo hayo hayakuwa na maslahi kwa taifa na ni ya hatari” kwa maendeleo yake kiuchumi.

Wala Chikawe aliyejipa kibarua hiki kigumu, hawezi kusema Chenge hakuwa mtu muhimu katika kufanikisha “dili la ununuzi wa rada.”

Chikawe anajua kwamba Chenge ndiye alikuwa mtu mwenye dhamana ya kuamua iwapo mkataba wa ununuzi wa rada kati ya serikali na BaE ufungwe au usifungwe.

Lakini hata kama watawala wanataka kukubaliana na watetezi wa Chenge, kwamba tuhuma za rushwa ni vigumu kuthithibitisha, lakini Chenge hawezi kukwepa tuhuma ya kufanya udaganyifu.

Kwanza, anuani ya Chenge ilikuwa S.L.P 11958, Dar es Salaam. Nyumba ya Chenge ilikuwa Na. 546, Barabara ya Ghuba, Oyster Bay.

Lakini taarifa za SFO zinadai Chenge hakutumia anuani yake halisi ya Dar es Salaam kwa kuwa alijua kwa kufanya hivyo, angeweza kushtukiwa kirahisi na mamlaka za serikali wakati wa kutekeleza dili lake.

Hata maelezo ya Chenge kuhusu fedha alizonazo yanatofautiana. Wakati awali alimweleza mshauri wake wa masuala ya fedha, JO Hambro anayeishi Uingereza kuwa “utajiri huo unatokana na shughuli zake za kitaaluma na akiba aliyojiwekea yeye na mkewe Tinnah Chenge,” katika maelezo yake mengine, Chenge alieleza SFO “utajiri unatokana na urithi katika familia yake.”

Pili, Chenge hakuwahi kueleza utajiri wake wote kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kama sheria inavyoelekeza.

Kifungu Na. 27 cha Sheria ya Mapambano dhidi ya Rushwa ya mwaka 2007 kinasema, “Kiongozi wa umma atakuwa ametenda kosa la jinai iwapo atakutwa na mali ambayo hakuitolea maelezo.”

Sheria inamtaka mtumishi wa umma, kama Chenge, kutoa maelezo ya namna alivyopata mali yake. Kutenda kinyume na maelekezo hayo, atakuwa ametenda kosa la jinai na anastahili kushitakiwa kwa mujibu wa sheria.

Sheria inasema, “Kiongozi wa umma atakuwa ametenda kosa iwapo ni au alikuwa kiongozi wa umma na anaishi katika maisha ambayo hayalingani na mapato anayopata au aliyokuwa akipata (wakati ni mtumishi).”

Chikawe anajua yote haya. Anajua kuwa Chenge ana fedha, tena nje ya nchi. Anajua kuwa Chenge hakueleza tume ya maadili ya viongozi wa umma kuhusiana na fedha zake hizo kama sheria inavyotaka.

Sheria hiyo haiishii hapo. Inasema, “Ni kosa la jinai kwa mtumishi wa umma kumiliki mali isiyolingana na mapato yake, ya sasa au zamani akiwa mtumishi…”

Sheria inaweka hata adhabu kwa mtuhumiwa wa makosa hayo. Ni kulipa faini ya kiasi cha fedha kisichozidi Sh. 10 milioni au kifungo cha miaka isiyozidi saba; au adhabu zote mbili kwa pamoja.

Chikawe anajua Chenge akiwa mtumishi wa umma anamiliki mali. hajawahi kutoa maelezo kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Public Leadership Ethics Secretariat) juu ya fedha zake hizo alizohifadhi katika akaunti yake kisiwani Jersey, nchini Uingereza.

Wala hajaweza kueleza kwa ufasaha wapi alitoa kiasi cha dola za Marekani 600, 000 hadi akaziweka kwenye akaunti ya Dk. Rashid. Hajajibu tuhuma kupokea malipo kwa siri.

Naye Chikawe ambaye anajua Chenge alilipwa kwa siri, hajaeleza kwa nini BAE System walilipa Chenge kwa siri? Walifanya hivyo ili iweje? Walilenga nini? Je, si kweli kwamba fedha hizo zilitumika kulainisha viongozi wa serikali?

Hivi hiki kinachoitwa, “leteni ushahidi,” kinatoka wapi, kama hakulengi kumlinda mtuhumiwa?

Kimsingi, kauli ya Chikawe bungeni imezidi kumuweka njia panda bosi wake, Rais Jakaya Kikwete. Je, kama Chenge hahusiki na wizi wa rada, Kikwete anawezaje kuhalalisha mkakati wake wa kufukuza ndani ya chama chake Andrew Chenge, Edward Lowassa na Rostam Aziz?

Vinginevyo, awe ametenda hayo kwa maelekezo ya Kikwete mwenyewe ili aweze kupata upenyo wa kujikwamua ili aweze kupata kisingizio cha kushindwa kuwafukuza marafiki zake ndani ya chama. Iwapo Chikawe anasema, Chenge ni msafi, Kikwete atawezaje kumfukuza kwenye chama?

Haikutarajiwa katika kipindi hiki ambamo chama kimekuwa mbali na wananchi, kiasi cha viongozi kusahau majukumu; serikali ikiwa hoi bungeni na Kikwete mwenyewe akiendelea kulaumiwa kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliyopita, Chikawe aibuke kumtetea Chenge.

Si hivyo tu: Haikutarajiwa pia katika kipindi hiki ambacho wananchi wanaamini kuwa madhila wanayopata ya ugumu wa maisha – kupanda kwa gharama za chakula, usafiri, njaa, kukosekana kwa umeme wa uhakika – yote hayo ni matunda ya ufisadi na uongozi mbovu, Chikawe aibuke na kusema, “Chenge ni msafi.”

Wala haikutarajiwa katika kipindi hiki ambacho CCM kimepoteza dira hadi kulazimika kufanya bethdei ya marehemu – Tanganyika African National Union (TANU), Chikawe aeleze wenzake ndani ya chama kuwa “mnayetaka kumfukuza hahusiki na wizi wa fedha za rada.”

Aidha, Chikawe hakupaswa kueleza hayo katika wakati huu. Wachunguzi wa masuala ya siasa katika utawala wa Kikwete wanasema anachofanya Chikawe ni kumtega rais wake, hasa hivi sasa ambapo Rais Kikwete anabebeshwa zigo la tuhuma za kushindwa kufanya maamuzi magumu, huku akiwashangaa wenzake kusahau wajibu wao na kupenda anasa.

Kikwete mwenyewe amekiri katika sherehe za kuzaliwa TANU, kwamba wenzake katika chama na serikali wamekosa moyo wa kutumikia wananchi, licha ya rasilimali nyingi zilizo nchini.

Kauli yake hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa wenzake wamechoka na sasa wanaomba kupumzika. Bali kuna tafsiri nyingine.

Viongozi nchini wamezoea kunyamazia hoja nzito; hata kashfa za kusaga mfupa. Wanatumia mtindo wa “watasema watachoka,” na wakichoka watanyamaza.

Chenge anasema acha waseme watachoka. Hasemi tena. Rais Kikwete amekuwa kimya juu ya tuhuma dhidi ya Chenge. Anaona watasema na mwisho watalala. Chikawe naye anasema; tena bila kuonyesha kuwa wananchi wana akili timamu na wana kumbukumbu. Naye anasema hata wakisema watachoka na mwisho watalala.

Kwa uchambuzi mwanana, yote haya ni kuonyesha dharau kwa wananchi; hasa ni tusi kwamba ama hawana akili au hawana kumbukumbu au baya zaidi, hawana mamlaka. Nani ana mamlaka sasa?

ngowe2006@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: