Chenge: Jasiri asiyeacha asili


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Andrew Chenge

JASIRI haachi asili! Ni Andrew Chenge. Wiki iliyopita, bila kutafuna maneno Chenge alithibitisha kuwa bado ni shujaa wa mikataba.

Akiwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Fedha na Uchumi, waliokuwa wakisikiliza taarifa ya utendaji wa Benki ya Posta, “Mzee wa vijisenti,” aliibuka na kuiambia serikali kwamba yupo tayari kuishauri katika mchakato mzima wa kuigeuza benki hiyo kutoka shirika la umma kuwa kampuni.

Hoja zilizotolewa kwamba ili benki hiyo iweze kuhimili ushindani wa sekta ya benki ni vema ikageuzwa kutoka kuwa chini ya sheria ya mashirika la umma kwenda sheria ya kampuni.

Wengi wanamtambua Chenge kama mwanasheria zaidi kuliko alivyo mwanasiasa. Huyu alikuwa mwanasheria mkuu wa serikali tangu mwaka 1995 hadi mwaka 2005.

Kwa maneno mengine, Chenge alikuwa mshauri mkuu wa serikali kwa mambo yote yanayohusu sheria kwa kipindi kifupi cha utawala wa awamu ya pili cha Mzee Ali Hassan Mwinyi, lakini akishikilia wadhifa huo kwa kipindi chote cha utawala wa awamu ya tatu chini ya Benjamin Mkapa.

Ukipitia kwa haraka haraka, utakuta Chenge alikuwa na mikono katika mikataba mikubwa ambayo taifa hili liingia na makampuni au watu binafsi kati ya mwaka 1995 hadi 2005.

Chenge anajitolea kufanya kazi ya kuisaidia serikali wakati mikono yake ikiwa imejaa mawaaa mengi juu ya mikataba mingi mibovu ambayo taifa hili limeshuhudia wakati akiwa katika kiti cha Mwanasheria Mkuu wa serikali.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ibara ya 59 (3) Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiye mshauri mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya kisheria; atawajibika kutoa ushauri juu ya mambo yote ya kisheria na utekelezaji wa mambo yote ya kisheria.

Katika madaraka hayo, Chenge hawezi kujivua kuwajibika vilivyo na mikataba yote ambayo taifa hili liliingia na watu binafsi, makampuni au mataifa mengine na faida au hasara ambazo tumepata kama taifa.

Kauli ya Chenge ya kutaka kuishauri serikali ameitoa huku kukiwa na tuhuma na shutuma lukuki dhidi yake za jinsi alivyoshiriki katika kuingiza nchi katika mikataba tata.

Je, alikuwa wapi wakati sisi kama taifa tunaingizwa mjini katika mikataba ambayo ninaamini kwa mujibu wa madaraka yake ya kikatiba alishiriki kuishauri serikali.

Wakati serikali ikifikiria kuiuza iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) baada ya kuigeuza kuwa NBC 1997, Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hii ni benki iliyokisiwa kuwa na thamani ya karibu Sh. 30 bilioni wakati huo, lakini baada ya safari ya kwenda kuonana na watu wa ABSA wa Afrika Kusini ikiwahusu aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Tanzania wakati huo, Dk. Idris Rashid na Waziri wa Fedha wakati huo, Daniel Yona, umma ukapigwa butwaa kwamba thamani ya NBC 1997 ilishuka kutoka takribani Sh. 30 bilioni hadi 15 bilioni tu.

ABSA ilipewa benki, majengo yake yote yaliyozagaa nchi nzima na yenyewe kwa kiburi ikafunga baadhi ya matawi kwenye wilaya za nchi hii na kubaki na matawi ya kwenye mikoa tu.

ABSA hawakuleta fedha yoyote hapa, walidai kuwa NBC 1997 ilikuwa inaidai Benki ya makabwela NMB, Sh. 15 bilioni katika mahesabu yao. Benki ya NMB ikakamuliwa hadi ikalipa fedha hizo kwa NBC na kisha fedha hiyo ndiyo ililipwa serikali kama mauzo halali ya NBC kwa ABSA.

Haya yalitendeka Chenge akiwa ofisini. Aseme alishauri nini kuepusha taifa na dhuluma hii kiasi sasa cha kutaka kutumbukiza mikono yake katika benki ya Posta?

Mwaka 2002 ulikuwapo mkataba kabambe wa kuuza iliyokuwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL). Wakaja wawekezaji walioitwa MSI/Detcon ambao walijotosa kununua asilimia 35 ya hisa za TTCL kwa thamani ya dola za Marekani 120 milioni (sawa na Sh. 120 bilioni).

Wakapiga mdomo wakapewa TTCL baada ya kulipa nusu ya kiasi hicho, yaani Dola milioni 60 (sawa na Sh. 60 bilioni) kwa madai kwamba watalipa nusu nyingine baada ya kufanya ukaguzi wa hesabu za TTCL wao wakiwa wanaiongoza. Wako jikoni kupika hesabu.

MSI/Detcon wakakabidhiwa TTCL wakafanya vitu vyao, ghafla ukaanza mgogoro usioisha juu ya albaki yetu. Mara visingizio vikaanza, TTCL ni hasara tupu, hakuna faida yoyote, hakuna hiki wala kile.

Mwisho wakashitakiana, lakini kesi ikaondolewa mahakamani na serikali ikaishia kulipwa Dola chini ya 10 milioni. Yaani zaidi ya Dola 50 milioni (wakati huo bilioni 50 na ushei) zikayeyuka. Hapa Chenge alikuwa ofisini akikalia kiti cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Je, alishuri nini serikali wakatu huo?

Orodha ni ndefu. Upo mkataba wa lililokuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATC) lililobinafsishwa kwa Shirika la Ndege la Afrika Kusini, ambao ulizaa ATCL. Kilichovunwa hapo ni ATCL marehemu.

Chenge alikuwa ameenea kwenye kiti cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tunaliwa na kutafunwa yupo tu. Hapa napo, alishauri nini serikali? Afungue mdomo aseme!

Upo mkataba wa ununuzi wa rada wa mwaka 2002 ambao Tanzania ilipigwa bei ya kuua, Sh. 40 bilioni huku kiasi cha Sh. 12 bilioni ziliishia kuliwa na wajanja kama kamisheni. Chenge si tu alishauri kuhusu ununuzi huu, bali pia anatajwa kama mmoja wa watu walionufaika na kamaisheni hiyo.

Ingawa amekanusha kula fedha yoyote, bado jinamizi la rada linamwandama. Ndivyo pia ilivyo katika sakata la ununuzi wa ndege ya rais. Chenge anaonekana kila kona, akiwa mashauri wa serikali.

Akiwa amebadili nafasi kutoka mtendaji serikalini hadi mwanasiasa, akiongoza Wizara ya Miundombinu kama Waziri, Chenge ametumbukiza shirika la Reli la Taifa (TRC) kwenye ubia na kampuni ya RITES kutoka India.

Baada ya kuibadili TRC na kuunda TRL, chini ya serikali ya awamu ya nne, hakuna kinachoeleweka ndani ya TRL hadi sasa. Si huduma, si ukarabati wa mabehewa au injini zake, hali ni ovyo kuliko inavyokuwa awali.

Huduma ni hoi bin taaban, kila mkataba wa kukarabati mabehewa, injini za treni na vifaa vingine vinatoka RITES India kuja kwa mwanawe RITES Tanzania.

Chenge aliuhakikishia umma kwamba safari hii serikali ilikuwa imekuwa makini kweli kweli katika kufikia mkataba huo, kwamba maslahi ya taifa yalikuwa yamezingatiwa vilivyo.

Mkataba ulisainiwa 31 Machi 2008. Muda si mrefu ulianza matatizo. Pamoja na matatizo hayo, serikali imeshikwa na kigugumzi kuuvunja. Lakini Chenge bado yupo hatumsikii akiomba kuitwa kuishauri jinsi ya kisafisha uoza huu alioshiriki kuutengeneza.

Katika mazingira haya kwa kutaja tu baadhi ya mikataba ambayo Chenge alishiriki kwa kiwango cha juu, tunashindwa kujua anapata wapi ujasiri wa kutaka aishauri serikali katika kuibadili Benki ya Posta? Kwa hili la sasa naamini Chenge ni jasiri asiyeacha asili!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: