Chenge, Mramba, Karamagi na Rostam wasirudi bungeni


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 19 May 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

KWANZA, ni lazima ifahamike kwamba tunapotaka kujenga demokrasia katika taifa, msingi mmoja mkuu ni viongozi kufahamu kuwa uongozi ni utumishi.

Katika msingi huo tulirudia mara kwa mara mawazo kuwa “cheo ni dhamana.” Mawazo haya yote yalitaka kutuonesha kwamba anayetaka kuwa kiongozi wa umma ni lazima atambue kuwa anataka kuwa mtumishi wa umma.

Katika utumishi huu wa umma jambo kubwa zaidi ni imani ya wananchi kwa viongozi wao. Endapo wananchi wanaanza kupoteza imani na viongozi wao, basi viongozi hao wanakuwa hawana mahali tena pa kusimamia.

Wananchi wanapowahoji viongozi wao na viongozi wanaposhindwa kutoa majibu ya hoja za wananchi hao, basi viongozi wanapoteza ile lulu kubwa wanayotakiwa kuwa nayo mbele ya wananchi na wananchi kwa haki wanaweza kabisa kuwakataa viongozi hao.

Hata hivyo, imani hii ya wananchi juu ya viongozi wao hujengwa kwa uadilifu. Uongozi wa umma bila ya uadilifu ni sawasawa na maji bila kata au gurudumu bila upepo. Huwezi kuwa na uongozi wa umma ambapo uadilifu unachukua nafasi ya chini au ya mwisho kabisa.

Uadilifu wa uongozi wa umma huchafuliwa na tuhuma. Kiongozi wa umma hapaswi kuwa chini ya wingu la tuhuma. Uzito wa suala la maadili unaelezwa vema na kanuni za Maadili ya CCM za mwaka 2002.

Kwamba, “jukumu la kiongozi wa CCM katika kukijenga na kukilinda chama ni kubwa. Athari katika chama za kiongozi kutenda maovu, au kutotimiza wajibu, ni kubwa kiasi kwamba maadili yake yakitetereka chama kitavurugika; na nchi itakwenda mrama.”

Kiongozi wa umma ambaye maadili yake yanazua maswali hafai kuendelea na uongozi.

Lakini siyo tu kuzua maswali, bali kiongozi wa umma anapokabiliawa na lundo la tuhuma nzito ambazo zinahusu tabia yake (character), zinahusu ukweli wake (honesty) na zinahusu vitendo vyake, ni tuhuma tosha ambazo hazipaswi kuachwa kuendelea.

Mojawapo ya mambo ya ajabu sana tuliyoyashuhudia miaka hii michache ni kuwa CCM imekuwa goigoi kushughulikia wanachama wake wanaokiuka maadili ya uongozi. Ni tofauti na enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wakati wa Nyerere CCM kilikuwa kweli chama cha wakulima na wafanyakazi. Lakini sasa, CCM inaendeshwa na kikundi cha wachache kupitia kinachoitwa, “mtandao wa Kikwete.”

Kwa hakika, CCM kingekuwa chama kinachofuata maadili kisingeweza tena kuwapitisha viongozi wake wanaokabiliwa na tuhuma lukuki za rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Mtindo huu wa uzito wa tuhuma ndio hutumiwa katika nchi nyingi za kidemokrasia katika kusafisha uongozi wa umma.

Katika nchi kama Marekani, Uingereza, Japani, Ujerumani, Ufaransa, India, uzito wa tuhuma unatosha kumfanya mwanasiasa kuamua kukaa pembeni.

Ziko tuhuma kubwa za aina nne ambazo hufanya viongozi wa umma kuachia ngazi bila hata ya kulazimika kwenda mahakamani na hata kama wakienda mahakamani wanafanya hivyo wakiwa tayari wametoka kwenye uongozi wa umma.

Kimsingi, mwanasiasa hawawezi kuendelea na uongozi wa umma wakati bado hajasafishwa kutoka katika tuhuma nzito zinazomkabili. Na njia pekee ya kujisafisha ni kwenda mahakamani.

Tuhuma za vitendo vya rushwa.

Hizi ni tuhuma zenye kudai kiongozi wa umma amepokea, ametoa au ameendekeza vitendo vya rushwa kwa manufaa yake.

Uzito wa tuhuma hizo unamfanya mtuhumiwa kukaa pembeni kupisha uchunguzi na siyo kung’ang’ania madaraka. Ushahidi kama watu wengine kushtakiwa, kunaswa na vyombo vya dola ni sababu tu ya kuzipa tuhuma hizo uzito unaostahili.

Mtumishi wa umma ambaye anatumia nafasi yake kujipatia starehe za ngono nje ya ndoa yake au kwa watumishi walio chini yake, ni kiongozi ambaye hahitaji mahakama kuthibitisha.

Endapo atatokea mtu na kudai kuwa mbunge fulani amembaka na kukawa na ushahidi mzito (kwa mfano, picha imepigwa wote wakiwa hoteli fulani) basi kiongozi huyo atahitaji kujiuzulu mara moja.

Hata yule anayetuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka, hastahili kuwa bungeni.

Ni kwa sababu, tabia ya kiongozi wa umma kutumia ofisi yake kujinufaisha binafsi au familia yake ama kundi fulani fulani la watu huku akijipatia manufaa aidha ya kifedha au ya kinafsi kutoka na matumizi hayo ya madaraka, haiwezi kukubalika katika jamii iliyostarabika.

Kiongozi anayetumia nafasi yake kupindisha sheria au taratibu kwa sababu yuko kwenye nafasi hiyo hafai kuendelea na uongozi.

Endapo kiongozi wa umma anagundulika kuwa ametumia nafasi yake kujilimbikizia mahali pasipo halali ama kwa kupata kamisheni zisizohusiana na kazi yake au kwa kuruhusu maamuzi fulani ili apata “mshiko” pale inapobainika, kiongozi huyo haraka anatakiwa kukabidhi ofisi ya umma.

Kwa msingi huo basi viongozi wafuatao hawastahili kurudi tena kuomba kura kwa wananchi na wananchi na CCM watakuwa wanafanya makosa makubwa kuwarudishwa.

Hii ni kwa sababu viongozi hawa kwa namna moja au nyingine wamegubikwa na wingu kubwa la tuhuma na kashfa za ukosefu wa maadili. Kashfa na tuhuma hizo zinahusiana moja kwa moja na uadilifu wao katika uongozi wa umma.

Kwanza, ni mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge – aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali (AG) wakati mikabata mibovu ya kifisadi ikiingiwa.

Chenge anatuhumiwa kuficha mamilioni ya fedha ambazo inadaiwa kuwa hazikutangaza kwenye fomu ya maadili ya viongozi kama inavyotakiwa. Ana kesi ya mauaji kwenye mahakama ya Kinondoni na kwamba anatuhumiwa kujipatia mlungula katika ununuzi wa rada ya kijeshi.

Alitakiwa kujiuzulu ubunge pale alipofikishwa tu mahakamani kwa tuhuma za mauwaji ili kuipa uhuru mahakama kutoa haki katika kesi inayomkabili.

Mbili, Basil Mramba: Huyu tayari amefikishwa mahakamani kwa kutuma za matumizi mabaya ya madaraka. Anatuhumiwa kutoa msamaha wa kodi kiholela kwa kampuni ya Alex Stewart.

Anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi yake kujinufaisha yeye mwenyewe. Mlolongo wa kashfa ni mkubwa na wa muda mrefu.

Tatu, Nazir Karamagi: Mwanasiasa huyu anakabiliwa na tuhuma lukuki za kutumia nafasi yake kuliingiza taifa kwenye mkataba wa kinyonyaji wa uchimbaji dhahabu katika mgodi wa Buzwagi, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Si hivyo tu, Karamagi ni mmoja wa watuhumiwa wakuu katika sakata la mkataba tata wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC). Hastahili tena kuwa mbunge hadi atakapojisafisha na tuhuma hizo.

Nne, ni Rostam Aziz: Tuhuma zake ziko wazi. Ni mmoja wa wabunge wenye utata zaidi katika historia yetu ambaye “hagusiki.”

Anahusishwa na kashfa mbalimbali kubwa ikiwamo ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, ukwapuaji kupitia kampuni ya Richmond/Dowans.

Mojawapo ya mambo ambayo hayajawahi kupatiwa majibu ya kuridhisha ni suala la uraia wake. Kutokana na uzito wa tuhuma dhidi yake alitakiwa kujiuzulu muda mrefu uliopita.

Atastahili kugombea na kuchaguliwa iwapo tu, atajisafisha. Vinginevyo kauli kwamba CCM ya sasa imekumbatia mafisadi itathibitika.

Hakika Tutaendelea wiki ile nyingine na kundi jingine la wabunge wa CCM ambao hawastahili kurudi kugombea tena.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: