Chenge na tuhuma mpya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 17 June 2008

Printer-friendly version
Ni ushirikina ukumbi wa Bunge
ANDREW Chenge

ANDREW Chenge, ambaye anakabiliwa na tuhuma za "ufisadi" sasa ametoswa katika tuhuma mpya za ushirikina.

Mbunge huyo wa Bariadi Magharibi (CCM), anatuhumiwa kuingia ukumbi wa Bunge, usiku wa Jumanne ya wiki iliyopita (10 Juni 2008) na kuonekana "akitupa vitu fulani ukumbini."

Spika wa Bunge Samwel Sitta aliliambia bunge juzi, Jumatatu, kwamba kamera za ndani ya bunge zilinasa watu wawili walioonekana "wakitangatanga ukumbini."

Alisema mmoja anasadikiwa kuwa mbunge na mwingine ni mfanyakazi wa ofisi ya bunge.

Sitta alisema usiku huo, wabunge wengine walikuwa katika vikao vya vyama vyao. Wabunge wa CCM walikuwa ukumbi mwingine tofauti na bunge.

Spika hakutaja majina ya walioingia ukumbi wa bunge, lakini taarifa za kuaminika zinataja Andrew Chenge na mfanyakazi wa ofisi ya bunge aliyejulikana kwa jina la Japhet Sagasii.

Taarifa za kuaminika zinasema Chenge na Sagasii waliingia ukumbini usiku huo. Maelezo ya ndani yanasema Sagasii alikuwa akienda kumwonyesha Chenge kiti atakachokuwa akikalia baada ya mbunge huyo kupoteza nafasi ya uwaziri.

Kawaida mawaziri wana nafasi yao ya kukaa, ambayo ni mbele, wakati wabunge wengine hukaa nyuma ya wawakilishi wa serikali. Chenge amekuwa akikaa mbele kwa miaka yote bungeni akiwa Mwanasheria Mkuu aliyesimamia utetezi wa serikali.

Taaraifa za ndani zinasema tarehe 25 Aprili mwaka huu, Chenge alimwandikia ujumbe Katibu wa Bunge, Damian Foka akiomba ampangie nafasi ya kukaa.

Katika ujumbe huo Chenge ananukuliwa kusema kuwa anataka "permanent seat" (kiti cha kudumu) na kwamba "kiwe upande wa kulia wa Spika ambako pia kuna "room for manouvre" (kusikobana).

Imefahamika kuwa mara baada ya Katibu wa bunge kupata ujumbe huo, aliuelekeza kwa Sagasii na kuamuru Chenge atafutiwe kiti mahali anakotaka.

Siku moja kabla ya mkutano wa sasa wa Bunge, zinaeleza taarifa, Sagasii anaripotiwa kukuta Chenge akiwa anaongea na mbunge wa kuteuliwa, Kingunge Ngombale-Mwiru nje ya ukumbi, na kumwomba Chenge aende kuonyeshwa kiti alichotaka.

Mbunge mmoja aliyeongea na Sagasii ameliambia MwanaHALISI kuwa Sagasii alimweleza kuwa hakuna chochote alichofanya yeye au alichoona Chenge akifanya ndani ya bunge mbali na kumwonyesha mahali pa kukaa.

Hata hivyo, Sitta aliliambia Bunge kuwa bado uchunguzi unafanywa kuhusiana na suala hilo na kwamba mpaka sasa ni "uvumi tu" na kusema kuwa, "tusubiri."

Alisema uchunguzi siyo lazima uwe unahusu mambo ya ushirikina. Alisema vinavyodaiwa kuwa vilikuwa vinatupwa bungeni siyo lazima viwe vya ushirikina bali "sumu za kisasa."

Sitta aliripoti bungeni kuwa tukio hilo tayari linashughulikiwa na vyombo vya usalama. Alisema mara baada ya kupata taarifa hizo, aliviarifu vyombo hivyo.

Alisema vyombo hivyo tayari vimeripoti kwake na kwamba alikuwa akiwathibitishia kuwa "ukumbi uko salama."

Awali katika tamko lake bungeni, Sitta alisema, "mimi binafsi wala ofisi yangu, hatuna imani za ushirikina" na kurudia kuwahakikishia wabunge kuwa ukumbi ni salama.

MwanaHALISI liliongea na Sagasii ambaye alikiri kupewa na katibu wa bunge, jukumu la kumtafutia Chenge mahali pa kukaa kufuatana na matakwa yake. Alisema hakufanya jingine zaidi wala kuona tukio tofauti.

Sagasii alisema, kwa sauti ya kusononeka, kuwa hajawahi kujiingiza katika mambo ya ushirikina na haoni kama mtu yeyote anaweza kumwingiza katika shughuli hizo.

"Wanaonifahamu wanajua hilo. Niko bungeni hapa kwa miaka mingi sasa. Nifanye ushirikina kwa kitu gani; kwa faida ya nani na ili iweje," alihoji alipokuwa akiongea na gazeti hili kwa simu kutoka Dodoma.

Simu ya Andrew Chenge, Na. 0754 782577 iliyoko kwenye orodha ya wabunge wa sasa wa Jamhuri ya Muungano, ilikuwa ikijibu kwa muda mrefu, "haipatikani, jaribu tena baadaye."

Spika alijitetea kwa wabunge kwa kutotoa taarifa yake mapema kwa kusema kuwa Alhamisi ilikuwa siku ya shughuli kubwa ya bajeti; Ijumaa haikuwa siku ya kikao cha bunge na Jumamosi na Jumapili zilikuwa siku za mapumziko.

Spika aliliambia bunge kuwa siku ya bajeti, aliandikiwa ujumbe na Victor Mwambalasa, mbunge wa Lupa kuwa alikuwa nje ya bunge akimhudumia Dk. Harrison Mwakyembe (CCM-Kyela) ambaye hali yake ilibadilika ghafla na akasaidiwa kupelekwa hospitali.

Dk. Mwakyembe ambaye hivi sasa yuko jijini Dar es Salaam, hakuweza kupatikana jana kueleza hali yake kwa kuwa simu yake ilikuwa haipatikani. Hata hivyo, Mwambalasa alilieleza gazeti hili kuwa alikuwa akiendelea vizuri.

Kubadilika ghafla kwa afya ya Dk. Mwakyembe na kukimbizwa kwake hospitalini, kulihusishwa haraka na taarifa za waliodaiwa kuonekana ukumbi wa bunge na kuchochea hisia za ushirikina.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: