Cheti cha kuzaliwa ni haki ya kila raia - RITA


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

PAMOJA na kuwepo kampeni ya muda mrefu kutaka watu wahakikishe wanakuwa na vyeti vya kuzaliwa na vifo kutoka Idara ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, bado mwitikio ulikuwa mdogo.

Hata baada ya kufanyiwa marekebisho makubwa kuitoa kutoka Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba na kuwa wakala unaojitegemea, bado wengi hawajui faida yake. Ofisa Mtendaji na Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko anaeleza pamoja na mambo mengine faida za wakala huo.

“Wapo watu ambao hadi leo hawajui faida ya kuwa na cheti cha kuzaliwa. Kutokuwa na cheti cha kuzaliwa si kitu kizuri kabisa,” anasema Saliboko.

Anaongeza, “Kimsingi, cheti cha kuzaliwa ni haki ya kuzaliwa ya kila raia wa nchi hii. Unapokuwa na cheti cha kuzaliwa inakusaidia kufanya vitu vingi.

“Kwa mfano, kwenye kupata ajira, hati za kusafiria (passport) na hata mambo ya uraia yanafanywa kuwa rahisi iwapo mtu ana cheti chake cha kuzaliwa,” anasisitiza.

RITA ilianzishwa mwaka 2006, ikichukua nafasi ya iliyokuwa Idara ya Kabidhi Wasii Mkuu wa serikali iliyokuwa chini ya Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba.

Katika mazungumzo na MwanaHALISI yaliyofanyika ofisini kwake wiki hii, Saiboko anasema vyeti vya kuzaliwa na vifo huisaidia pia serikali katika kupanga mipango yake ya baadaye.

Anasema iwapo kila mtu anayezaliwa atawekwa kwenye rekodi, serikali itakuwa katika nafasi nzuri zaidi kufahamu kiwango na namna ya kufikisha mahitaji ya huduma za jamii katika eneo husika.

“Hebu tufikirie kidogo. Kama serikali haijui idadi ya watu waliozaliwa katika eneo husika, ni kwa vipi itajua dawa kiasi gani zitahitajika, madawati na huduma za maji? Kwa hiyo, mwananchi anafaidika kwa namna zaidi ya moja wakati anapokuwa amejiandikisha kuzaliwa,” anasema.

Saliboko anasema kwa sasa, mtu anayekwenda katika ofisi za RITA ana uwezo wa kupata cheti chake cha kuzaliwa katika muda wa siku mbili tu.

Anasema RITA imeajiri wapiga chapa na wanasheria wa kutosha, kuhakikisha kwamba huduma zote muhimu zinapatikana katika ofisi hizo na kuondolea wananchi usumbufu wa kwenda mahakamani kuapa.

Gharama za kupata cheti cha kuzaliwa zinaanzia kiasi cha Sh 3500 na 20,000 kulingana na umri wa mtu anayepewa cheti na umbali kutoka makao makuu.

“Mtu anayechukua cheti kutoka ofisi zetu za makao makuu Upanga jijini Dar es Salaam jirani na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili atapata kwa gharama nafuu kuliko yule atakayechukua pengine,” anasema.

Sh 3500 ni gharama kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 wakati wale wanaozidi umri huo na ambao hawana nyaraka zozote itagharimu Sh 20,000

Saliboko alisema kwamba mbali ya wakala huo kutoa vyeti vya kusaliwa pia hutoa vyeti vya kufariki dunia, kusimamia talaka na masuala ya mirathi.

“Mtu ambaye ana cheti cha kifo kilichotolewa na RITA anakuwa na faida mbalimbali. Kwanza, atarahisisha masuala ya mirathi na pili kama alikuwa na kesi ya jinai mahakamani, kesi itafutwa kwa vile marehemu hawezi kushitakiwa,” anasema.

Saliboko anasema kuna faida nyingine kubwa ya kuandikisha kifo ambayo wananchi wengi hawaifahamu lakini inasaidia sana.

Kuna hadithi ya eneo moja ambalo watu walikuwa wakifa mfululizo. Kwa sababu hakuna ambaye alikuwa akipima na kutoa sababu za vifo hivyo, watu walianza kushikana uchawi.

Baada ya vifo vingi kuanza kuripotiwa, serikali ikaanza kuchunguza. Muda mfupi baadaye, ikabainika ya kuwa tatizo lilikuwa ni ugonjwa wa uti wa mgongo. Serikali ikatoa dawa watu wakapona.

“Kama wananchi wale wangekuwa wanakwenda ofisi za RITA kuandikisha vifo hivyo, sababu ya vifo ingejulikana mapema na maisha mengi yangeokolewa. Hii ni sababu kubwa sana ya mtu kutaka aandikishwe,” alisema.

Changamoto

Akizungumzia changamoto zinazokumba wakala huo, Saliboko alisema changamoto ya kwanza kubwa ni ufinyu wa bajeti unaosababisha kupunguza ufanisi.

Akitoa mfano, alisema ofisi nyingi za RITA mikoani zinahudumiwa na watendaji wa serikali, chini ya ofisi za makatibu tawala wa mikoa na wilaya; ambao hawahusiki moja kwa moja na wakala.

“Ingekuwa vizuri kama RITA ingekuwa na watumishi wake nchi nzima. Tuna upungufu wa watumishi kusema kweli kwa vile hawa walio chini ya taasisi nyingine za serikali, wana majukumu mengine pia. Hili linaweza kupunguza ufanisi,” alisema.

Jambo lingine alilosema ni ukweli kwamba bado wakala huo unafanya shughuli zake kwa mikono (manual) katika maeneo mengi, ukiondoa wilaya za mkoa wa Dar es Salaam na Kibaha ambazo tayari zimeunganishwa kwenye mtandao.

“Kitu kama tayari kiko kwenye kompyuta, hata kukitafuta inachukua muda mfupi. Kutafuta vitu vilivyo kwenye makatarasi inachukua muda mrefu. Tukianza kutumia kompyuta kila mahali, itachukua muda mfupi zaidi kuliko sasa katika ufanyikaji wa mambo mengi zaidi,” anasema.

Pamoja na changamoto hizo, Saliboko anaamini ndani ya miaka mitano ijayo, itawezekana kwa mtu anayetaka kupata cheti chake cha kuzaliwa, akipate ndani ya siku moja.

Pia, Saliboko anaamini kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo, watoto wote wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka mitano, watakuwa wameandikishwa na wana vyeti vya kuzaliwa.

Saliboko ambaye ndiyo kwanza ana wiki moja ndani ya wadhifa wake huo, ametoa shukrani kwa serikali pamoja na wafadhili wengine kutokana na msaada mkubwa wanaoipatia wakala hiyo.

“Kama nchi yetu ingekuwa tajiri, nadhani tungepata fungu kubwa zaidi. Kila wizara, tassisi au idara ya serikali ina matatizo kama tuliyo nayo sisi lakini tatizo keki yetu ya taifa ni ndogo.

“Kinachotakiwa kufanywa kwetu sisi ni kujitolea kwa asilimia 100 kutimiza tulilopangiwa na serikali. Kile tunachopewa tukitumie na taratibu tutapiga hatua,” anasema.

Kwa mujibu wa Saliboko, wafadhili wengine wakubwa wa RITA ni taasisi zilizo chini ya Umoja wa Mataifa (UN) na nchi wafadhili kama vile Canada.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)