Chikawe akumbana na ushoga


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 18 August 2009

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe

JULAI 13 na 14 mwaka 2009, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenda Geneva, Uswisi, kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kijamii na Kisiasa (ICCPR) wa mwaka 1966 katika Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNHRC).

Tanzania iliridhia mkataba huo mwaka 1976. Hii ilikuwa ni ripoti ya nne kwa serikali mbele ya kamati hiyo. Taarifa ya Chikawe iligusia maeneo mengi ya utekelezaji yakiwemo kuingiza haki za mkataba huo katika sheria za nchi.

Chikawe hakujua kuwa huko Uswisi kutakuwa na ujumbe mwingine juu ya suala hilohilo, lakini usio wa serikali. Huu ulikuwa ujumbe wanaotetea ushoga.

Hivyo wakati Waziri Chikawe alieleza jinsi haki za msingi za binadamu zilivyoingizwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, watetezi wa ushoga walitoa taarifa kuwa kuna ubaguzi dhidi ya watu wa jinsia moja wanaotaka kujamiiana.

Serikali ilieleza kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa jinsi haki za binadamu zinavyokuzwa, zinavyolindwa, zinavyozingatiwa na kutekelezwa kupitia Tume ya Haki za Binamu na Utawala Bora na utaratibu mwingine wa usimamiaji na utoaji taarifa wa Wizara ya Sheria na Katiba.

Aidha, serikali ilieleza kwamba imetekeleza kwa kiwango kikubwa mapendekezo ya Tume ya Nyalali kuhusu sheria arobaini kandamizi.

Maelezo mengine ya kina katika taarifa ya serikali yalihusu haki za makundi maalum kama wanawake, watoto na wenye ulemavu, yakiwemo masuala ya marekebisho ya sheria ya ndoa na mirathi.

Taarifa ilieleza pia juu ya haki za uraia kwa wanaume wanaooa wanawake wa Tanzania, ubakaji ndani ya ndoa (kwa waliooana), ukeketaji, adhabu ya kifo, haki za wafungwa, na hali ya kisiasa Zanzibar.

Hata hivyo, kikundi cha watu watatu (Watanzania) wanaodai kuwakilisha Watanzania wanaotetea mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja, nacho kilisambaza nakala za taarifa yake.

Kikundi hicho kinajulikana kama "Lesbian, Gay, Bisexual Persons Transgender" (LGBT). Taarifa yake ilionyesha serikali ya Tanzania isivyojali haki za ushoga.

Wanaharakati hao waliita taarifa yao, kwa Kiingereza, "The Violations of the Rights of Persons in The United Republic of Tanzania – A Shadow Report" (Ukiukaji wa Haki za watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Taarifa mbadala).

Watu hao watatu wamejitambulisha kuwa ni Julius L. Kyaruzi (Mratibu wa LGBTI Tanzania), Monica Mbaru (Mratibu wa Afrika wa Progamu ya Tume ya Kimataifa ya Haki za Mashoga – IGLHRC) na Stefano Fabeni (Mkurugenzi wa kuanzisha na kueneza haki za LGBTI Duniani).

Watu hao wanaungana na mzungu mmoja, Derek Tripp, anayesoma na kufanya utafiti wa shahada ya uzamivu (PhD) katika sheria.

Katika taarifa yao ya kurasa nane kuhusu Tanzania, wanasema Ibara ya 2 (1) na 26 ya mkataba wa ICCPR inazitaka nchi husika kuheshimu usawa wa raia wake.

Wanasema ibara ya 26 inapinga ubaguzi wa aina yoyote hasa katika "Mahusiano ya kimapenzi na kujamiiana." Ibara hiyo inaruhusu na kulinda mahusiano hayo ya mapenzi ya jinsia moja ikiwemo kujamiiana.

Wanabainisha kuwa hata Katiba ya Tanzania inatoa haki ya usawa kwa watu na kwamba ubaguzi wa aina yoyote unakatazwa na Katiba hiyo katika Ibara ya 12 na 13.

Wanaharakati hao ambao hawajasema wazi iwapo wao ni mashoga, wanasema kuna sheria Tanzania inapingana na ICCPR na Katiba.

Kwa mfano, wanasema kifungu cha 154 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kinakataza watu wazima wa jinsia moja kujamiiana.

Kifungu hicho kipo katika kundi la makosa ya jinai ya kujamiiana "kusiko kawaida," (mfano: kujamiiana kwa jinsi moja, ndugu waliozaliwa tumbo moja na wanadamu kwa wanyama).

Kifungu hicho kinakataza pia ulawiti au vitendo vya kujamiiana (mwanamme na mwanamke) kinyume cha maumbile. Mtu akipatikana na hatia kwa kosa hilo anaweza kufungwa miaka 14.

Wanaharakati hao wa haki za ushoga wanasema sheria hiyo inazuia matamanio ya kimapenzi ya watu wa jinsia moja na huingilia faragha yao, haki inayolindwa na Ibara ya 16 ya Katiba.

Wanalaani pia marekebisho ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 1998 ambayo yalienda sanjari na kutungwa kwa Sheria Maalum ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA).

Vitendo hivyo vinavyokatazwa na SOSPA ni kama vile kukonyeza, kupiga miluzi, kupapasa na kukumbatia. Wanasema hii inawazuia pia wanaume ambao wanatazamana kimahaba au wanapigana mabusu au kushikana mikono kimahaba au wanalala pamoja kimapenzi.

Wanasema vifungu vyote vya sheria ambavyo vinasemekana kulinda maadili ya raia kwa misingi ya imani zao za kidini, mila na desturi, zinawabagua wale wachache ambao hawafuati maadili hayo, wakiwemo mashoga.

Wanahoji mbona kuna mpango wa kuwatambua makahaba, masikini wauza ngono na wanaume wanaojamiiana ili kuwapa elimu ya ukimwi?

Katika kujenga hoja yao, wananukuu ukurasa wa 57 wa Mpango wa Pili wa Mkakati wa Masuala ya Ukimwi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) wa mwaka 2008 – 2012.

Wanasema kwa serikali kutambua umuhimu wa kupunguza au kuondoa hatari ya maambukizi ya virusi vya ukimwi, tayari inatambua kuwepo kwa haki za mahusiano yao ya mapenzi au kujamiiana.

Wana madai mengi. Bali hawajui kuwa tafsiri na utekelezaji wa mikataba ya haki za binadamu kwa kila nchi, inaendana na mazingira ya nchi husika.

Kwa mfano ni makosa makubwa kutumia mfano wa kesi moja iliyoamuliwa nchini Australia (Toonen v. Australia, UN Communication No. 488/1992) katika mazingira ya Tanzania ambayo utamaduni wake ni tofauti na nchi hiyo.

Hukumu ya kesi hiyo inasema, mapenzi ya jinsia moja yakikatazwa kwa sheria ya jinai, "ni ubaguzi" hata kama sheria inataka kulinda maadili ya jamii fulani.

Tukumbuke hata ndani ya Kanisa la Madhehebu ya Kikristo ya Kiangalikana, wanapingana kuhusu kuruhusu ushoga na wamelitenga jimbo moja nchini Marekani lenye wachungaji na askofu shoga.

Msimamo wa Kanisa la Waanglikana Afrika (ikiwemo Tanzania) ni mkali sana. Madhehebu mengine ya ki-Kristo na Kiislam wanalaani vitendo hivyo na kutotaka hata kuvisikia.

Kwa uwazi au kimyakimya, mashoga wapo Tanzania. Inaonekana wanalipwa na taasisi zisizo za kiserikali za mashoga wa Ulaya.

Huu ndio mwanzo wa mjadala. Wanaharakati wanasema Katiba inawakubali, hata kama haitaji neno "ushoga." Sheria inayopaswa kuwa chini ya Katiba inawakataa.

Je, Tanzania ielekee wapi katika mazingira hayo?

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)