Chunga unaposikia CCM inalia rafu


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

LEO nimeguswa na mambo mawili – malalamiko ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba kinahujumiwa katika utoaji wa maoni ya Katiba mpya ya Jamhuri, na kauli ya SMZ kuhusu vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Mawazoni mwangu, suala la vitambulisho ndio nilikusudia litawale mada wiki hii. Malalamiko ya CCM yaliibuka katikati na ni vema nikayashughulikia kabla ya kupoa.

Kwa umuhimu wake, nitaanza na malalamiko haya.

Nikitumia uzoefu wa utendaji katika siasa za Zanzibar, nina kila sababu ya kusema ukiona chama hiki kinalalamika hadharani kuhujumiwa, ujue kimezidiwa kete.

Wakati mwingine unaposikia kelele za viongozi wake, hwenda ni dalili za mkakati wake chenyewe kugonga mwamba.

Hebu sikiliza anachosema Katibu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Zainab Khamis Shomari: “Kuna jina la Said Mwema limejitokeza katika barua na baada ya barua hizo, Tume ilitaka kumjua huyo mtu mwenye jina hilo la Said Mwema lakini matokeo yake hakuna aliyejitokeza.

“Kwa hivyo sisi tuna shaka na hao watu wanaokwenda kupeleka maoni kwa njia ya barua tukiamini kuwa zinaandaliwa na baadhi ya wanasiasa.”

Zainab aliyewahi kuwa naibu waziri wakati wa serikali ya Amani Abeid Karume (2000-2010), anasema vitendo vingine “vibaya” ni watu kuzomea watoa maoni pamoja na kutumia wanafunzi kutoa maoni baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa walimu.

Kwa namna nilivyokuwa nikisikia chama hiki kinajiandaa kwa ajili ya utoaji maoni ya katiba, malalamiko haya ni mzaha. Kwani wakuu wa tume wako wapi wasiyaone?

Huyu hakutaja kamwe tukio la kuhusishwa waziri kutoka CCM, na kuandika barua na kuigawa kwa wanachama wengi wa CCM ili yaliyomo ndiyo yawe maoni yao kwa tume.

Ilikuwa bahati tu, baadhi ya waliopewa barua hiyo, waliifichua kwa kumtaja waziri aliyewapa na hatimaye wakaikabidhi Tume.

Mwaka 1995, Ali Ameir Mohamed, akiwa naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, alijitokeza mbele kulalamikia matokeo ya uchaguzi hata kabla hayajatangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya mwenyekiti Zubeir Juma Mzee.

Ameir ambaye pia alikuwa mbunge wa Donge na waziri wa mambo ya ndani, baada ya kutuhumu watendaji wa tume kuwa walishirikiana na upinzani, alihitimisha lawama zake kwa kusema hawakubaliani na matokeo yatakayotangazwa.

Wakati huo, sisi waandishi wachokonozi tulikuwa na taarifa imara kuwa mawakala wa ulinzi na usalama walikuwa wanavuruga kura, ili kuhakikisha mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour Juma, anatangazwa mshindi.

Ndivyo ilivyokuwa. Mzee wa watu, Zubeir, aliingia kwenye ukumbi mdogo wa tume, akiwa ‘amebanwa’ kila pembe na mabunduki katika mbinu ya kumlazimisha kusoma matokeo anayoamini hasa ni haramu.

Waandishi tulisukumwasukumwa na wanausalama waliojaza silaha za dhahiri na walizozificha viunoni, na wengi wao ndio wakapata nafasi ya kuingia ukumbini.

Kweli, mzee yule akatangaza matokeo haramu yaliyompa Dk. Salmin ushindi mwembamba ambao mwenyewe alikiri na kuuita, “ushindi ni ushindi tu hata ukiwa wa goli moja,” alipokutana na waandishi wa habari pale Bosnia, Kikwajuni.

Mara tu matokeo hayo yalipotangazwa, CCM ikiwa imepata asilimia 50.2 dhidi ya asilimia 49 za Maalim Seif Shariff Hamad, Ali Ameir Mohamed alitimka mbio mpaka ofisini kwake Kisiwandui. Tulipomfuata, kumuuliza kama amebadili kauli, alisema, “Mngekuwa nyinyi mngefanyaje.”

Maana yake alitaka tufahamu ushindi katika uchaguzi kwenye nchi za Afrika, si lazima upatikane kwa njia za haki. Hata maguvu yakitumika si tatizo. Bado serikali zote mbili zinahaki ya kujinasibu zinafuata misingi ya utawala bora na utawala wa sheria.

Mara zote CCM walipolalamika kuhujumiwa, matokeo ya mwisho yalionyesha walipata walichokitaka, hata kama ni kwa kujeruhi wananchi na kuvuruga taratibu za uendeshaji mambo kisheria.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, 2010, mambo yalikuwa hivyohivyo – uvurugaji taratibu na mwisho, CCM ikatangazwa mshindi wa kila kitu, urais na viti vingi katika Baraza la Wawakilishi.

Hiyo ndiyo CCM – Unachukua, Unaweka, Waaa (UUWA). Kwa Zanzibar, mbali na kaulimbiu hiyo wananchi wamezoea kusikia “Mapinduziiii Daima.”

Wala viongozi wake hawajali kama wanayoyafanya ni aibu mbele ya umma na ulimwengu. Hawajali chochote maana wao “ndio” mamlaka ya nchi.

Nyakati za uandikishaji wapiga kura na upigaji kura, viongozi wa CCM walipolalamika, basi maji yalikuwa yamewafika shingoni katika kusimamia mikakati ya kuhujumu taratibu. Lakini pia walikuwa wakizuga tu umma uamini eti hawatendewi haki.

Angalieni, kipindi chote hiki ambapo wananchi wamekuwa wakilalamika kubaguliwa katika taratibu za kupata kitambulisho cha Mzanzibari, siyo tu kwamba hakuna kiongozi yeyote wa CCM anayewasikiliza, bali wanawapinga na kuwabeza eti wanatumiwa na wanasiasa.

Viongozi kadhaa wa chama hiki wanasema hakuna tatizo lolote katika upatikanaji wa kitambulisho, labda kwa yule mwananchi ambaye hana sifa za kupewa kitambulisho.

Ule mtandao imara wa kubagua watu wanaohisiwa si wapenzi wa CCM, wanaujua vizuri viongozi hawa; na vile ulivyonyonga haki ya kuchagua 2005 na 2010.

Masheha wote ni watiifu wakuu kwa viongozi wa CCM wa ngazi zote, chini mpaka juu mwisho. Wakielekezwa chochote wanatekeleza hata bila ya kuuliza kama wanachotenda ni haki kisheria na kiutu.

Hata pale Maalim Seif, ambaye tangu Novemba 2010 amekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, alipolalamikia ukorofi wa masheha wa kuzuia wananchi kupata kitambulisho, alionekana kinyago. Viongozi wa CCM hawakujali.

Ni desturi kwa viongozi wa CCM kutojali kitu kwa malalamiko ya watu ambayo kwao, yanachojaribu kufanya, ni kuwasumbua tu. Wanaamini hata watu wakilalamika vipi, hakuna kitakachobadilika.

Ni bahati mbaya sana wakati viongozi wa chama cha siasa wakipuuza na kuchekelea malalamiko ya wananchi kunyimwa haki za kiraia, ikiwemo hii ya kupata kitambulisho, watendaji wa taasisi za serikali, wanaopaswa kuwasaidia kupata haki hiyo, nao hawajali.

Ndio maana wakati malalamiko ya wananchi yanaongezeka kila siku ipitayo kuwa wanakwamishwa kupata idhini ya masheha ya kupata kitambulisho, kunatoka takwimu za kulaghai ulimwengu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, analiambia Baraza la Wawakilishi vitambulisho 112,420 vipo ofisini havijachukuliwa na wenyewe.

Takwimu hizi amepewa na Idara ya Usajili na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambayo, pamoja na jitihada zote za kujieleza kama taasisi inayotii sheria na katiba, haijajivua na lawama za kuchangia sana kunyonga haki za raia katika suala hilo.

Takwimu hizi zinatolewa huku mkuu wa idara hii, Mohamed Juma Ame, akijua fika kuwa mpaka leo hajakubali rai tuliyompa baadhi yetu, ya kutangaza majina ya wenye vitambulisho hivyo ili kuangalia kama wapo kweli.

Hapana shaka, anajua yeye kwanini hili ni gumu mno kwake kutekeleza.

0
No votes yet