Taifa lipo hatarini


editor's picture

Na editor - Imechapwa 10 March 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MATUMIZI mabaya ya fedha za umma imekuwa ni ugonjwa sugu kwa serikali iliyopo madarakani. Tumewahi kuelezea katika safu hii ubaya wa nidhamu mbovu katika matumizi ya fedha za umma kwamba ni pamoja na kupoteza fursa za nchi kuendelea.

Serikali yenyewe hushindwa kutekeleza kwa ufanisi mipango yake ya maendeleo na hivyo kuchangia uchumi kuzorota na hali ya maisha ya wananchi kuzidi kushuka.

Takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka mzima, jitihada za serikali za kupunguza kiwango cha umasikini zimetoa watu wawili tu kutoka kundi kubwa la mafukara na kuwa wenye kipato afadhali, kati ya Watanzania 100 wanaoishi kwa kipato cha siku kisichozidi Sh. 1,300 (dola moja ya Marekani).

Mbali na kulegalega katika ukomeshaji wa rushwa, serikali haijaelekeza ipasavyo raslimali kwa mambo yanayogusa maslahi ya watu.

Watu hawajabadilika kimtizamo kuhusu tatizo la rushwa. Wengi wanaendelea kuamini haki haipatikani bila ya kuhonga.

Hili limeshtua wafadhili kama linavyoumiza wananchi walalahoi. Unakuta wakati familia inapata mlo kamili wa siku kwa shida, inalazimika pia kuhonga ndipo mtu wake atibiwe. Tunazungumzia kundi kubwa la watu wanaotegemea tiba serikalini.

Mwenendo wa serikali unapokuwa kinyume na matarajio ya nchi wafadhili ambazo siku hizi huitwa washirika wa maendeleo, maana yake washirika hao wanavunjwa moyo katika kusaidia Watanzania.

Inakera kuona utendaji wa serikali haujawa ule unaoleta matumaini kwa wafadhili na zaidi kwa wananchi wenyewe.

Bali ni wazi serikali haionyeshi kujali lawama na shutuma inazotupiwa na ushahidi ni kule kutobadilika.

Hivi ni nini kama siyo jeuri ya madaraka kukuta serikali inashindwa kurekebisha kasoro mbalimbali katika matumizi ya fedha za umma kama zinavyobainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)?

Ripoti zake za karibuni zimesema wazi utoaji wa huduma kwa wananchi kwa maeneo kadhaa hauridhishi.

Hiyo inajenga picha kwamba uongozi wa juu wa serikali umefika mwisho. Hauwezi kujisimamia na kusimamia viongozi walio chini yake.

Uongozi unaposhindwa kujisimamia inaashiria umefeli. Hakuna dawa na ndio kusema tuna serikali iliyoshindwa kuleta matunda. Haiwezi kuleta mabadiliko.

Ukweli, mustakbali wa taifa upo shakani na panahitajika mabadiliko makubwa ya haraka kabla ya taifa kusambaratika.

0
No votes yet