CUF imekumbatia bundi mzee, itaanguka


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version

KILA sehemu anakopatikana ndege aitwaye bundi, hutambulika na kuhusishwa na imani mbalimbali – nzuri au mbaya.

Barani Ulaya, kwa miaka mingi bundi alitambulika kama “muungu wa hekima.” Wazungu wengi walichukulia kuonekana kwa bundi kama ishara yao ya matumaini.

Wagiriki walikwenda mbali zaidi ya hapo. Walimuona bundi kama bahati ya mtende; kwamba wale waliohitaji ufadhili wa masomo, wataupata haraka.

Kwa Wamarekani, kama ilivyo kwa maeneo mengi ya Afrika na nchi za Mashariki ya Kati, ndege huyu ambaye mara nyingi hutembea na kuonekana usiku tu, alikuwa ishara ya balaa, mkosi na mikasa ya wachawi.

Katika nchi jirani ya Kenya, imani ya Wakikuyu juu ya bundi, haina tofauti na ya makabila mengi nchini petu.

Watanzania wengi kwa miaka mingi wamekuwa wakimtazama bundi kama mkosi, maradhi na hata kifo. Wengi wanamwogopa, wanamkwepa na kuchukulia mlio wake kama uchuro na sababu ya matatizo mengi.

Imejengeka imani kuwa mtu yeyote anayekabiliwa na matatizo mbalimbali yasiyoisha ametembelewa na bundi. Huu umegeuka msemo wa kawaida, ambao sasa unaweza kutumika kuelezea mambo yalivyo kwa Chama cha Wananchi (CUF).

Chama hicho kwa sasa hakijatulia. Kimejaa mabishano, malumbano, kuzomeana na kushtakiana. Waliomo CUF wamekosa uvumilivu, wameanza kuondoka mmoja baada ya mwingine, kundi baada ya jingine na kuna uwezekano chama kikazidi kugawanyika.

Bundi kwa maumbile yake, haoni mchana, lakini usiku anaona vizuri. Ni mwepesi na anaweza kukwepa maadui zake, labda kama ni mzee, goigoi, mgonjwa au asiyejimudu.

Kwa muktadha huu, ni rahisi kusema kuwa bundi aliyeitembelea CUF kipindi hiki ni mzee au mgonjwa asiyeweza kujimudu. Haoni wala kusikia. Hajimudu wala kuhisi maadui wanaomfuata. Hataki au hawezi kuondoka kwenye chama.

Lakini cha ajabu, hata CUF wenyewe, kwa maana ya uongozi wa juu, hawataki kumuondoa. Wameaswa mara nyingi kuwa bundi anawanyemelea. Wamepuuza. Wameshauriwa kutumia busara badala ya hasira kukabiliana na mgogoro unaokiandaman chama chao, hawakusikia.

Kinachoendelea kwa CUF kinatoa picha kuwa huenda wanataka kuendelea na mgogoro huo badala ya kuumaliza. Ninashawishika kuamini kwamba CUF wamemkumbatia bundi mzee, hawataki kumwachia na hakika watakufa naye.

CUF inatakiwa kumsaka bundi huyu mzee. Kumtambua na kutafuta mbinu za kumfukuzia mbali. Busara ya hali ya juu inatakiwa kutumika ili bundi apatikane na kuondolewa.

Asipoonekana, mikosi itazidi kukiandama chama hichi. Kitazidi “kumomonyoka na nyama zake kunyofoka”. Viongozi wasipoangalia chama kitabaki mifupa.

Hii si siri tena, maana hata wale waliodhaniwa ndio nguzo ya chama, kina Said Miraji, kiongozi wa Blue Guard aliyewahi kukaimu unaibu katibu mkuu na Leopold Mahona, aliyegombea ubunge Igunga katika ucahguzi mdogo mwaka jana, nao wameondoka.

Mgogoro unaoiandama CUF si mdogo kama baadhi ya viongozi wake waandamizi wangependa umma uamini. Mara kadhaa wamesikika wakisema wamezoea mawimbi kama haya, wakitaja tukio la kung’olewa kwa mwasisi na mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, James Mapalala kama mfano.

Hata hivyo, kwa wachunguzi wa masuala ya kisiasa, utetezi huu ni wa kujikosha tu. Hata kama aliyeng’olewa wakati huo alikuwa kiongozi mkuu wa chama, migogoro hii miwili ni tofauti sana, sawa na mbingu na ardhi.

Wakati wa Mapalala chama hakikuwa kinafahamika sana nchini. Hata watu waliokuwa wanafuatilia mgogoro huo walikuwa wachache, waliokuwa wamejenga imani na Mapalala walikuwa wachache pia. Na alipotimuliwa, waliomfuata walikuwa wachache au hawakuwapo kabisa.

Sasa mambo yamebadilika. Idadi ya wanachama wa CUF iko juu ukilinganisha na wakati ule, na wengi wameshajenga imani kubwa kwa viongozi wao, wakidhani kwamba hawawezi kufanya madudu, hadi inapotokea vinginevyo.

Pia, mgogoro huu umekikumba chama wakati ambao baadhi ya wanachama walikuwa wameanza kukichoka kutokana kutuhumu viongozi kutosikiliza wanachama wake na kuona hali halisi ya chama kushuka maarufu.

Mathalan, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, kura za mgombea urais wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, zilishuka kutoka zaidi ya 1,300,000 za mwaka 2005 hadi 600,000. Pia katika uchaguzi mdogo wa ubunge majimbo ya Busanda, Igunga na Uzini, tumeshuhudia kuwa mvuto wa chama hicho unazidi kutoweka.

Viashiria hivyo vya chama kupauka, ndiyo sababu ya mgogoro huu kushika kasi na kusambaa kwa haraka. Wengi wa wanachama wanaojiondoa CUF sasa, hawakusukumwa na hatua za kumfukuza uanachama Hamad Rashid Mohamed, mbunge wa Wawi, bali wanaona kuna tatizo katika wenendo mzima wa uendeshaji wa chama. Wapo wanaoona chama kinayumba kimaamuzi na hakina mwelekeo.

Mfano, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Vijana taifa aliyejiengua hivi karibuni, Omar Costantine alisema amekerwa na kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Ismal Jussa Ladhu, kuwa chama kimeshindwa uchaguzi mdogo wa Uzini kwa kuwa jimbo hilo lina Wakristo na Wabara wengi.

Wengine wanataja chama kutojijenga Bara badala yake kinaimarisha nguzo zake na raslimali zake kifedha kujikita Zanzibar pamoja na umwinyi wa viongozi wa kitaifa.

Kama ulivyo msemo wa Kiswahili kuwa “Kamba hukatikia pabovu,” mgogoro wa sasa kati ya CUF, Hamad Rashid na wenzake, ndio sehemu yake nyembamba. Huu ndio utambi unaowasha moto wa kuisambaratisha CUF.

Laiti kama viongozi wake wangesikiliza ushauri wa Watanzania wengi mapema, kuwa ikae meza moja na kumaliza mgogoro na Hamad Rashid bila timuatimua, huenda haya mambo mengine yangeepukwa.

Muda ungalipo kabla ya jahazi kuzama. Linahitaji kunusuriwa. Mbali na suala hili, viongozi waandamizi wanapaswa kuachana na tabia ya kufunika matatizo makubwa kwa kuyaona madogo na kuyapuuza.

Vilevile viongozi wakuu waache kusemasema kwa kila jambo. Pakitokea tatizo basi viongozi wakutane kulijadili katika vikao vya ndani badala ya kuanzisha malumbano hadharani kupitia vyombo vya habari.

Viongozi wa CUF wanajulikana kwa ujasiri wa kutetea hoja na misimamo ya chama kama walivyofanya chama hicho kilipopakaziwa na chama tawala kuwa ni cha udini au kinaamini ugaidi. Tuhuma zile zikaishia.

Wana nafasi ya kujieleza kwanini walilazimika kukubaliana na CCM kuunda serikali ya umoja wa kitaifa upande wa Zanzibar. Hii ni hatua iliyoidhinishwa na chama, haiwezekani viongozi washindwe kuitetea.

Uzito wa viongozi kujibu hoja hadharani mpaka kulalamikiwa, ndio bundi mzee anayeiandama CUF. Bundi mzee lazima adhibitiwe na hapa ndipo hasa ulipo wajibu wa Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa CUF ambaye anatarajiwa kupata mapokezi makubwa Jumapili baada ya kuwa nje ya nchi kwa miezi mitano sasa. Ni muhimu akinusuru chama na anguko la kihistoria.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: