CUF inao au haina mgogoro?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 December 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

“CHAMA chetu hakina mgogoro,” anasema Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, katika kuelezea mvutano ulioibuka ndani ya chama hicho.

Maalim Seif, mmoja wa wanasiasa wa enzi nchini walioanzisha CUF mwaka 1992, anasema kwa kuwa chama ambacho yeye ni kiongozi mtendaji mkuu, hakina mgogoro wowote, anatarajia kama lipo tatizo linalokihusu lipite kwenye vikao halali.

Kwa sababu yale yanayohojiwa hayajapita kwenye vikao, anasema “kamwe sithubutu kuendesha malumbano na mtu yeyote. Mtu yeyote hata yeye mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed.”

Maalim Seif anamtaja Hamad Rashid, mbunge wa Wawi, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, kwa sababu akiwa mmoja wa waanzilishi wenzake wa CUF na pia kiongozi mwandamizi, ndiye aliyejitokeza waziwazi kuanzisha mvutano katika chama.

Tena, anayevutana naye wala si mwingine, ni mwenyewe Maalim Seif kama katibu mkuu; mwanasiasa wa asili ya eneo la Mtambwe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba na mtu anayeonekana mhimili mkuu wa siasa Zanzibar .

Hata kabla ya kufanya mahojiano maalum na wahariri wa MwanaHALISI, Jumatatu ya wiki iliyopita akiwa hotelini jijini Dar es Salaam, Maalim Seif alishaapa siku mbili kabla, hatokaribisha malumbano na Hamad Rashid.

Bila ya kutarajia au alitarajia, alilazimika kujibu kiu ya waandishi wa habari waliochomekea maswali kuhusu hali ya mambo CUF kwenye mkutano maalum aliouitishaili kuelezea mafanikio ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyotimiza mwaka mmoja tangu kuundwa.

Alikuwa Kulthum Ali, mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) aliyepata nafasi ya kwanza kuuliza maswali na kuchokonoa hisia za Maalim Seif kuhusu mvutano katika CUF. Mkutano huo uliofanyikia ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Zanzibar , tarehe 17 Disemba.

Kulthum alitaka msimamo wa kiongozi huyo kuhusu “kauli tata” za Hamad Rashid ambaye siku za karibuni amekuwa akiporomosha tuhuma binafsi dhidi ya Maalim Seif kiasi cha kuwa kivutio kikubwa cha vyombo vya habari nchini na vya kimataifa.

Hapo, ilikuwa ni baada ya waandishi kumsikiliza Maalim Seif akisoma taarifa ndefu ya alichokiita “mafanikio ya SUK,” serikali iliyoundwa na Rais wa Zanzibar , Dk. Ali Mohamed Shein ambaye alimteua yeye kuwa makamu wa kwanza wa rais.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliyofanyiwa marekebisho ya 10 Julai mwaka jana, serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi mkuu wa rais na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, itakuwa ya umoja iwapo kuna vyama vimepata asilimia inayotakiwa ya kura halali ili kushirikishwa katika serikali hiyo. CUF na Chama Cha Mapinduzi (CCM) atokacho Dk. Shein, ndivyo pekee vilivyotimiza sharti hilo la kikatiba.

“Chama ni taasisi, inaendeshwa kwa mujibu wa taratibu na katiba. Katika CUF hatuna utamaduni wa kushindana kwenye magazeti. Hilo hatufanyi kabisa. Wala mimi sipo tayari kufanya malumbano na Hamad Rashid au mwanachama mwingine yeyote,” alisema.

Wakati maelezo hayo yakitoka kinywani mwa Maalim Seif, ambaye kitaaluma ni mwalimu na mtaalamu mahiri wa siasa-jamii, usoni kwake alionekana asiye na utulivu. Ilikuwa ni ishara ya wazi kuwa kinachotendwa na kutokea katika chama kinamsononesha.

Kwa muda sasa, Hamad Rashid amekuwa akisikika kushawishi kampeni ya mabadiliko; akijenga hoja kuwa tangu Maalim Seif ateuliwe makamu wa kwanza wa rais amekuwa akitumia muda mwingi kwa shughuli za kiserikali na kusababisha utendaji wake katika chama kuzorota.

Kwa hivyo, mbunge huyo anadai, wakati umefika aachie ngazi ya ukatibu mkuu ili nafasi hiyo akabidhiwe mwanachama atakayerudisha utendaji imara wa kazi za chama hicho hasa upande wa Bara ambako, anasema, “chama kimepoteza mvuto.”

Lakini, Hamad Rashid ana ujumbe maalum kwa suala hilo . Anataka nafasi ya Maalim Seif aishike yeye. Anasema hadharani: “Ndio, mimi ni mwana-CUF na nina sifa za kushika wadhifa huo.”

Anaongeza, “Nataka kugombania nafasi hii ili kuondokana na utamaduni wa kuufanya ukatibu mkuu kwenye chama chetu kama utume. Ifike wakati ukatibu mkuu uwe utumishi, badala ya kuwa utume….”

Kama Hamad ameweka nia ya “kugombania” ukatibu mkuu, hilo si tatizo kwa Maalim Seif ambaye anasema, “Hiyo ni haki yake kabisa kama ilivyo haki kwa mwanachama yeyote wa CUF. Lakini lazima kila mmoja apitie utaratibu tuliojiwekea katika chama.”

Anasema wakati uchaguzi mkuu wa chama utafanyika 2014, mwanachama anaweza kueleza nia yake ya kugombea nafasi anayoitaka, lakini asubiri utaratibu na utaratibu wa uchaguzi upo miaka mitatu ijayo. “Sasa jamani, njia anayoitumia ni sahihi,” anahoji.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo kwa namna ya kujitoa katika kueleza moja kwa moja kuwa labda njia anayoichukua Hamad Rashid katika “kupigia debe mabadiliko ya uongozi ndani ya CUF” si halali kiutaratibu.

“Mimi sitaki kuwa muamuzi wa suala hili. Kama ni sahihi au laa, tuachie Baraza Kuu la Uongozi ndilo litaamua wakati ukifika,” anasema.

Baraza Kuu la Uongozi (BKU) ni chombo cha juu katika chama hicho. Na hapo ndipo hupelekwa ajenda za mipango na maendeleo ya chama ikiwemo mapendekezo ya kufanya mabadiliko katika katiba kabla ya mambo hayo kufikishwa mkutano mkuu kwa ajili ya kupitishwa rasmi. Maamuzi ya mkutano mkuu ndiyo ya mwisho kichama.

Maalim Seif anasema kwa roho radhi anamkaribisha ”mwanachama anayejiamini kuimudu nafasi hiyo, mwenye ubavu wa kushindana na mimi. Kwanza sijasema kama mimi nitaondoka. Nani nimemwambia nitaondoka?

“Mimi wala sijatangaza. Mara zote wapo walioingia kugombea. Sasa mimi nasema, kwa yule mwanachama anayetaka, agombee, na mimi nitagombea kwa hivyo tutakutana huko kwenye mkutano mkuu ambako wanachama wataamua.”

Hapo, Maalim Seif alionesha tabasamu la nguvu lililoashiria kwamba labda anajua fika “atambwaga tu atakayejitokeza.” Anatambia nguvu kiuongozi alizonazo na imani ya watu anayoendelea kujivunia.

Hamad Rashid anamtuhumu Maalim Seif kushindwa kusimamia matumizi mazuri ya fedha za chama na kuimarisha chama kiasi cha kukikosesha kura katika uchaguzi mkuu wa 2010 wa rais, wabunge na madiwani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

Kuhusu tuhuma dhidi yake, Maalim Seif anasema anaendelea kufanya kazi zake vizuri, akitekeleza maagizo ya BKU. “Hatuna tatizo lolote katika chama chetu. Tena juzi tu tulifanya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kwa mafanikio makubwa. Ni kielelezo cha utulivu ndani ya chama.

“Lakini kama kuna malalamiko dhidi yangu mie nayasubiri yafikishwe kikaoni niulizwe, katibu mkuu kuna hili na hili nitaeleza. Mimi nimekuwa nikihojiwa mambo mengi na nayatolea maelezo kwa sababu sina shaka na ninayoyatenda kama kiongozi,” anasema.

Hamad Rashid amezidi kutanua wigo wa mvutano katika CUF kwa kuanza kuzunguka mikoa kadhaa ya Bara akikutana na viongozi wa ngazi za wilaya na matawi. Wiki iliyopita alisikika akiwa mkoani Tanga ambako kwa mara ya pili alisema hana kosa lolote maana yeye ni mwanachama mwenye haki ya kueleza anayoyaona hayaendi sawa.

Alianza mkoani Dar es Salaam ambako haikuchukua muda kugonga mwamba pale ziara yake ya matawi ya Manzese na Mabibo iliposababisha mapigano ya wanachama. Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alinukuliwa akithibitisha kutuma walinzi wa chama kuhoji uhalali wa ziara hiyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: