CUF inavyozama huku ikidhoofisha upinzani


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba

CHAMA cha Wananchi (CUF) chaweza sasa kuwa kinatoka usingizini? Lakini wapo wanaosema, “Kinatafuta shuka wakati tayari kumekucha.”

Kwa lugha ya uzazi wa mpango tungeweza kusema, “Wamekumbuka kuvaa mpira wakati tayari ni wajawazito.”

Wiki mbili zilizopita, Baraza Kuu la uongozi la CUF liliwatema katika nafasi mbalimbali za uongozi baadhi ya viongozi wake wa juu akiwamo aliyekuwa naibu katibu mkuu Zanzibar, Juma Duni Haji.

Wengine ni aliyekuwa kiongozi wa wabunge wa chama hicho katika Bunge la Muungano, Hamad Rashid Mohammed na Mnadhimu wake, mbunge wa Gando, kisiwani Pemba, Khalifa Sulemani Khalifa.

Nafasi ya Hamad imechukuliwa na mbunge wa Mkanyageni, kisiwani Pemba, Mohamed Habib Mnyaa, huku mbunge wa viti maalum mkoani Tabora, Magdalena Sakaya amekuwa katibu wa kambi ya CUF na mbunge wa Chambani Pemba, Hemed Salim akifanywa mnadhimu mkuu wa kambi hiyo.

Duni, Hamad na Khalifa ni miongoni mwa vigogo waandamizi wa chama hicho. Mabadikiko yeyote ya kuwaondoa sharti yaambatane na maelezo yenye kukidhi mahitaji ya wanachama na wananchi.

Akisoma maazimio ya chama chake, mwenyekiti wa taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema mabadiliko hayo ya uongozi yamelenga kurejesha hadhi ya chama mbele ya wananchi.

Hata hivyo, kila mwenye akili timamu ameona kuwa mabadiliko yaliyofanywa si ya sera, mbinu, mpango mkakati, wala kauli mbiu. Ni mabadiliko ya sura, ambayo yametoa mwanya wa kujadiliwa na pengine hata kutiliwa shaka na wanaokitakia mema chama hicho.

Kwa mfano, kuondolewa kwa Juma Duni kwa kisingizio ni waziri katika serikali ya umoja wa kitaifa, lakini nafasi yake akakabidhiwa Jussa ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe, kisiwani Unguja.

Kuondolewa kwa Duni ambaye ndani na nje ya CUF, anajulikana kutokana na msimamo wake usioyumba, ushupavu wake katika kutetea maslahi ya wananchi na mtu mwenye dhamira ya dhati ya kuifanya CUF kuwa chama tawala Zanzibar, badala ya mshiriki katika serikali, kunaweza kuchukuliwa kuwa kumelenga kumdhoofisha kisiasa.

Hata katika Jamhuri ya Muungano, mchango wa Duni katika kuijenga CUF si haba. Si mara moja wala mbili, Duni amekiokoa chama chake kwa hatua yake ya kuridhia kuwa mgombea mwenza wa Profesa Lipumba, pamoja na kwamba alijua kuwa nafasi yake ya kushinda ni ndogo.

Katika kutekeleza takwa hilo la viongozi wake, Duni aliamua kuachana na mbio zake za uwakilishi katika jimbo lake la Mji Mkongwe ambako alikuwa na uhakika wa kushinda.

Tokea mwaka 2002 – mara baada ya kutoka gerezani alikokuwa anashikiliwa kwa tuhuma za kutunga za mauaji ya polisi kisiwani Pemba, Duni amekuwa akishinikizwa na wenzake katika chama na hata walionje ya chama kujitosa katika mbio za urais.

Lakini yeye amekataa. Amesema hakuumbwa kugombana na wakubwa wake katika chama – akimaanisha Maalim Seif Sharif Hamad.

Ni nidhamu hiyo ya uongozi ambayo hata wale ambao hawakuwa mashabiki wake wakati huo, wanaonekana sasa kumuona ni kiongozi anayeongozwa na hekima; hivyo kupendekeza kwa siri na wazi kuwa mrithi wa Maalim pale kiongozi huyo atakapostaafu siasa.

Hata kuondolewa kwa Hamad Rashid kuongoza wabunge wa chama chake kupitia mwamvuli wa “kambi isiyorasmi bungeni,” hakuwezi kukisaidia chama hicho.

Sababu ni nyingi. Kwanza , tatizo la CUF ni zaidi ya Hamad.

Pamoja na kwamba nafasi ya kiongozi wa wabunge wa CUF si kubwa sana hasa kwa kuwa CUF kimepoteza uongozi wa Bunge, lakini kwa wanaofuatilia siasa za Bunge, wanafahamu umuhimu wa Hamad katika nafasi hiyo.

Hamad ana uzoefu wa miaka mingi wa shughuli za Bunge kuliko mbunge yeyote wa chama hicho. Anafahamu kanuni za Bunge na muelewa mzuri wa sheria na taratibu zinazoongoza Bunge. Hata chama chake na viongozi wake wanafahamu hilo vema.

Tatizo pekee ambalo Hamad analo, ni kule kushindwa kutenganisha shughuli zake binafsi na masuala ya chama chake.

Kwa mfano, Hamad anajihangaisha mno na biashara. Nyingi ya biashara hizo zinafanywa na serikali au zinahitaji huruma ya serikali kuweza kuzifanikisha.

Hivyo inafika wakati anashindwa kutimiza majukumu yake ndani ya chama.

Anaweza hata kupindisha baadhi ya taratibu. Wanaomfahamu wanadai kuwa aweza hata kumdokeza mapema waziri mkuu, swali ambalo kesho yake amepanga kumuuliza bungeni, ili kufanikisha biashara yake.

Hata hivyo, suala hili la kutanguliza ubinafsi haliko kwa Hamad pekee. Viongozi wengi wa wajuu wa CUF wanadaiwa kutawaliwa na ubinafsi.

Angalia kwa mfano, kila mmoja ndani ya CUF anajua maana ya msamiati wa “kambi isiyo rasmi;” kwamba inaashiria mushkeli katika siasa za upinzani ndani ya bunge.

Lakini hata baada ya kelele nyingi za wadau,CUF imekataa kuungana na CHADEMA kuunda kambi moja ya upinzani bungeni. Kisa: Ndoa ya mkeka kati ya CUF na chama cha NCCR- Mageuzi.

Viongozi wa CUF kwa kujua au bila kujua walikubaliana na matakwa ya Hamad ya kutaka kambi hiyo iundewe na wabunge wote wakiwamo wa NCCR- Mageuzi na hata mwenyekiti wa Tanzania Lebour Party (TLP), Augustine Mrema ambaye tayari amejidhihirisha kuwa ni “rafiki mwaminifu” wa CCM.

Pili, CUF wanajua kuwa James Mbatia, mwenyekiti wa taifa wa NCCR- Mageuzi aliwahi kuthibitisha kutumikia CCM ili kudhoofisha upinzani.

Ni mwaka 2003 Mbatia alipoacha kusaidia mgombea wa ubunge wa chama chake Kigoma Kusini; akajitosa Pemba kuwekea pingamizi wagombea ubunge CUF katika uchaguzi mdogo kisiwani humo.

Wakati Mbatia anafanya haya, alijua kuwa uchaguzi wa wa Pemba ulikuwa wa “ukombozi.” Ulikuja baada ya mauaji ya raia zaidi ya 28 waliopigwa risasi na polisi 26 na 27 Januari 2001, Unguja na Pemba .

Wananchi wengine walijeruhiwa na makumi mengine wanadaiwa kubakwa na kudhalilishwa huku wengine wakigeuka wakimbizi katika nchi jirani ya Kenya.

Mbatia hakujali  “mauaji hayo ya halaiki.” Alitumika kudhoofisha CUF na sauti za wananchi wa visiwani waliokuwa wanadai haki yao ya msingi ya kuheshimiwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Nje na ndani ya Zanzibar, Mbatia alihubiri CUF chama cha kidini; chama cha Wapemba; kinafadhiliwa na mataifa ya Kiarabu na kinatumiwa kuingiza nchi katika machafuko. Hakuna yeyote ndani ya CUF anayeweza kudai kuwa amesahau yote haya.

Si Profesa Lipumba, Maalim Seif, Jussa, Hamad Rashid, Duni wala Mnyaa anayeweza kutetea yaliofanywa na Mbatia. Utetezi pekee ambao wamekuwa wakiutoa ni pale wanaposema,“CUF chama cha kusamehe.”

Lakini ukiwauliza, “Je, wanachama wengine wa kawaida, familia za wahanga na hata wananchi wengine wa kawaida wameulizwa na kusema wamesamehe?” Hawakupi jibu.

Sasa swali la kujiuliza ni hili: Ndoa hii ya Mbatia na CUF imelenga nini? Jibu ni moja. Imelenga kudhoofisha harakati za wanachama na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika kipigania haki za wananchi na kutaka kuiondoa CCM madarakani.

Ndoa ya Mbatia na CUF haikulenga  kuimarisha upinzani, kwa sababu Mbatia ni mpinzani kwa jina, si vitendo. Haikulenga kuisaidia CUF kwa kuwa tayari aliwahi kukisaliti chama hicho. Bali , fungamano hili limelenga kudhoofisha upinzani kwa maslahi ya waliopo madarakani.

Ni katika fungamano hilo jipya, karibu viongozi wote wa CUF wanaimba kuwa CHADEMA ni “chama cha vurugu.” Kwa hili, hata CCM wanachekelea sana kuona CUF wakiiponda CHADEMA kwa msimamo wake wa kudai pasipo kuhesabu gharama.

Tatizo la CUF ni kwamba imeamua kuvaa glovu wakati wa kurusha masumbwi yake kwa CCM, wakati wenzao wanarusha kavukavu.

Lakini ukiondoa hilo, kuna hili pia. CUF haiwezi kusema kuwa imefanya mabadiliko ya uongozi ili kusaidia kupigania upatikanaji wa haki za wananchi.

Hii ni kwa sababu, mengi ya matatizo yaliyopo nchini, chimbuko lake ni uongozi mbovu wa CCM – chama ambacho CUF imekubali kufunga ndoa ya kuendesha pamoja serikali visiwani Zanzibar.

Kama CUF wanataka kurejesha heshima yao iliyopotea, lazima waachane na Mbatia na chama hicho kieleze wananchi kiini na umuhimu wa muungano wake na CCM visiwani.

Jambo hili sharti lielezwe vizuri kwa wananchi; vinginevyo kila uchao CUF itakuwa inahitaji mabadiliko ya uongozi.

Viongozi wakuu wa CUF hawanabudi kurudi darasani kutafuta chanzo cha chama chao kupoteza nguvu ya ushawishi katika siasa za Tanzania Bara. Wajiulize, nini kilichosababisha kupoteza kura nyingi katika uchaguzi uliopita?

Hata hivyo, kwa hapa ambako viongozi wa chama hicho wamekifikisha, kunahitajika kazi ya ziada ya kukirejesha kwenye mkondo wa awali.

Hata kama CUF siku hizi hawataki kusema wazi, lakini ni wazi kuwa “ungangari” wao ndio uliwapa heshima ambayo sasa wameipoteza kwa kukumbatia makombo ya mafisadi ndani ya CCM Zanzibar.

Kwa hakika, itachukua muda mrefu CUF kutambua kuwa ukaribu wao na CCM utazidi kuwatesa kama ambavyo CCM yenyewe inateswa na ukaribu wake na watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini.

CUF imeachana na siasa zake za harakati ambazo Rais Jakaya Kikwete na chama chake wamekuwa wakizitumia kukirushia vijembe chama hicho; siasa ambazo zimeanza kushamiri hata ndani ya CCM yenyewe hivi sasa.

Kila uchao wananchi wanashuhudia kile unachoweza kuita mpambano ndani ya CCM – mithili ya siasa za CUF – “Jino kwa jino,” ambazo CCM wamekuwa wakizitumia kukidhoofisha chama hicho.

Itakuwa ajabu kwa chama cha upinzani kama CUF kuzibeza siasa za harakati na papohapo kutegemea kuheshimiwa na wapigakura wake. Tabaka la watawala limeshika hatamu na kuendelea kunyonya raslimali za taifa.

Haitarajiwi kuwa tabaka hilo litaamka siku moja na kuwaita CUF waende kuchukua ushindi na mabadiliko mezani.

0
Your rating: None Average: 3.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: