CUF na kiherehere cha ikulu


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version

NIMEJITOSA kujadili hatua ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kujipeleka ikulu kuonana na Rais Jakaya Kikwete. Kwangu mimi hatua ile ya CUF naiona kama ni kujikanyaga.

Naomba nithibitishe kwa nukuu zifuatazo kutoka kwenye kumbukumbu za bunge (Hansard) za wabunge wa chama hicho, wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 bungeni.

Kwanza, Mhe. Khalifa Suleimani Khalifa (Gando - Pemba):

Mheshimiwa spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya pili katika jambo hili muhimu kwa mustakabali wa taifa letu. Mimi kama mbunge niliyekuja bungeni hapa kupitia Chama cha CUF leo ni miongoni mwa siku ambayo nimefurahi sana.

Nimefurahi kwa sababu chama changu kimekuwa mstari wa mbele kuiomba serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wa nchi hii kuandaa mazingira ya kupatikana katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Makofi).

Mheshimiwa Spika, sisi tulifanya hivyo kwa madhumni ya kuwasaidia Watanzania. Chinua Achebe anasema; “he who paves the way to the great paves the way to his own greatness.” Tulifanya vile ili heshima hii ikipatikana inarudi kwetu wenyewe. Huo ulikuwa utangulizi (Makofi).

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana umefanya juhudi kubwa kwa niaba ya bunge hili kuhakikisha kuwa muswada huu unapata nafasi inayostahili ya kujadiliwa. Lazima tukubali ulipokuja mara ya kwanza ulikuwa na matatizo mengi lakini kwa juhudi zako umelisaidia bunge letu kuweza kuwa katika mazingira mazuri ya kuujadili (Makofi).

Pili, napenda nishukuru hatua zote zilizochukuliwa na upande wa pili wa Muungano kwa ushirikiano na viongozi wa Zanzibar katika kufanikisha muswada huu. Ushirikiano umekuwa zaidi ya asilimia 95 hiyo ni +A. Sasa unapofikia hapo binadamu lazima uone kuwa wenzako wamefanya juhudi (Makofi).

Pili, Mhe. Hamad Rashid Mohammed (Wawi- Pemba):

Mheshimiwa Spika, sisi katika Chama cha Wananchi (CUF), Naibu Katibu Mkuu wetu, Ndugu Mtatiro (Julius Mtatiro) alifanya maandamano kupeleka rasimu ya katiba katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), tukidai mabadiliko ya katiba; ni sisi tuliofanya hili, mbona wao hawakufanya? (Hapa alikuwa anazungumzia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Hatukuwaona wakifanya hilo, tumeandamana kwa hili kwa kudai katiba, leo Rais (Rais Jakaya Kikwete) ambaye ana mamlaka kabisa kwa mujibu wa katiba yetu, angesema anaunda tume bila ya kuja bungeni na tume ikasimama na ikafanya kazi bila ya kutushauri.

Lakini amefanya busara ametuletea muswada huu ili tuujadili na tuupitishe hapa, lakini watu wanakataa wanasema kuna udikteta. Udikteta gani zaidi ya kwamba madaraka aliyonayo akayakasimu mwenyewe, akayaleta kwenye bunge (Makofi).

Mheshimiwa Spika, tunataka nini? Eti leo tukatembee nchi nzima kwa kupeleka tena muswada huu, tunachotaka kupeleka kule ni fujo, sisi tunakataa, sisi tunakataa kupeleka fujo!

Kama ni mawazo yametoka na yametoka kikamilifu. Wakati tunaingia kwenye kamati wenzetu walikuwa hawaji kwenye kamati, mimi nikakaa nao, nikawaambia kama tuna mawazo kwanini tusije kwenye kamati tukazungumza? Leteni mawazo yenu tuyachambue yenye maana tutayakubali, ndiyo baadaye wakaanza kushiriki.

Mheshimiwa Spika, mimi ningeomba sana ndugu zangu, the Nation has to remain as a Nation, hatuwezi kuwa na taifa lenye vipande vipande na mawazo potofu, tubaki na taifa na taifa litapatikana kama mchakato huu wa katiba tutakwenda nao kwa salama na amani, kwa utulivu kwa kuaminiana na kwa busara na kuheshimiana.

Hiyo process (utaratibu) ndiyo itatusaidia kupata taifa lililotimia na ndiyo lengo la rais kwamba sasa jamani baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara, baada ya miaka 46  ya Mapinduzi hebu tukae tujitazame upya chombo ambacho tunakitumia kuendesha nchi kiweje?

Hayo ndiyo madhumuni makubwa. Sasa mimi nafikiri busara ikitaka kutumika turudi tukae kitako.

Tatu, Mhe. Habibu Mnyaa (Mkanyageni, Pemba):

Mheshimiwa spika, …leo nina furaha kusema kwamba marekebisho haya ya serikali ambayo wameleta haya, schedule of amendment, yamechukua asilimia kubwa ya haya ambayo chama changu walitaka yawemo (Makofi).

Kwa nukuu hizo za bunge, ni ukweli uliyowazi kwamba viongozi na wabunge wa CUF walikubaliana na sheria iliyopitishwa kwa asilimia miamoja. Hili linathibitishwa na nukuu yao iliyosema, “Tulikubaliana kabla ya kuja hapa kupitisha muswada huu kwa kuwa ni mzuri na unakidhi mahitaji ya taifa.”

Hizo ndizo kauli kuu za wabumnge wa CUF. Sasa kama walikuwa wanakubaliana na sheria iliyopitishwa, kipi kiliwasukuma kwenda kwa Rais Kikwete? Kama walikuwa na hoja tofauti na ile waliojadili bungeni, mbona mpaka sasa, hawajatoa waraka walioupeleka ikulu kwenye majadiliano yao na serikali?

Aidha, aliyeweka msingi wa mjadala wa CUF kwenye muswada bungeni, ni Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary. Ni yeye ambaye ni mwandishi wa sheria na mwanasheria mkuu wa zamani wa Zanzibar, aliyenukuliwa akisema yote ambayo chama hicho kimekuwa kikiyapigania kwa miaka yote tokea kuwepo kwake, yamezingatiwa katika sheria hiyo.

Sasa kama yote ambayo CUF imeyapigania yametekelezwa kikamilifu, safari ya ikulu ililenga nini kama siyo kumchosha kiongozi wa nchi?

Au ni kweli kwamba CUF wamekwenda ikulu baada ya kuona wenzao CHADEMA wamekutana na rais? Uthibitisho ni kauli ya Celina Kombani, waziri wa sheria.

Alisema, “Mheshimiwa spika, kwa moyo mkunjufu kabisa napenda kumshukuru mheshimiwa Aboubakar Khamis Bakar, waziri wa katiba na sheria wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa ushauri wake na ushirikiano alionipa katika kipindi cha kuandaa muswada huu.”

Kwenda kwao kukutana na rais kunaweza kutafsiriwa kuwa ni mojawapo ya njia ya kutaka kuwaonyesha wananchi kuwa CUF ya sasa imekuwa chama cha kukurupuka bila ya kupanga hoja zake.

Ukipitia sheria iliyopitishwa na serikali na kupigiwa vigelele na wabunge wa CUF, utabaini kuwa bado kuna mapungufu mengi ya kimsingi hasa kwenye kifungu cha 9(2) ambacho hakitambui kuwepo kwa serikali tatu kama ulivyo msimamo wa CUF kwa miaka yote tangu kuanzishwa kwake.

Badala yake, sheria inaeleza, “Mfumo wa Muungano utaendelea kama ulivyo,” jambo ambalo litaendelea kuinyima nafasi Zanzibar katika jumuiya za kimataifa kama vile, umoja wa mataifa (UN), umoja wa Afrika (AU), umoja wa nchi za Kiislamu (OIC) na nyinginezo likiwamo shirika la soka la kimataifa (FIFA).

Sasa katika mazingira hayo, nani anaweza kusema hatua ya CUF kushiriki mjadala bungeni na kisha kwenda kumuona Rais Kikwete ilikuwa ni mujarabu? Bila shaka hakuna.

Ndiyo maana hata viongozi wenyewe wa CUF wanashindwa kueleza kilichowasukuma kwenda ikulu.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: