CUF: Tukishinda, tutaunda serikali shirikishi


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetangaza mipango yake na kimenadi sera. Kimepita kila wilaya na kimeona hamasa ya wananchi kutaka kufanya mabadiliko ya uongozi wa nchi.

CUF, kupitia kwa Said Miraji, meneja kampeni wa mgombea urais wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba, amekipa ushauri Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiwe na ujasiri wa kukubali matokeo.

“Naweza kusema jambo moja tu; Watanzania sasa wako tayari kwa mabadiliko. Hamasa ni kubwa sana kiasi kwamba baadhi yetu tunashangaa. Naomba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiwe na ujasiri wa kukubali matokeo ya wananchi,” anasema.

Miraji anaongeza, “Kama hakutakuwapo na uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2005, CUF, kitapata ushindi katika urais, ubunge na kuunda halmashauri katika wilaya za Tanzania bara.”

Tofauti na kampeni zilizowahi kufanyika nchini tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, uchaguzi wa mwaka huu unafanyika katika mazingira ya hamasa na uelewa mkubwa.

Kwa mujibu wa Miraji, wananchi wameonyesha uelewa mkubwa si tu katika kuvifahamu vyama vyao lakini katika kuwafahamu wagombea na aina ya mabadiliko ambayo wanataka kuyaleta.

Kwa tathmini yao, Miraji ambaye amezunguka nchi nzima na Prof. Lipumba katika kipindi hiki cha kampeni kwa siku 62, anasema hakuna chama chochote kitakachoshinda katika uchaguzi wa mwaka huu kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura.

“Kwa vile washindi tutakuwa ni sisi, tayari tumejiandaa kuunda serikali ambayo itawashirikisha Watanzania wote bila ya kujali tofauti zao za kiitikadi,” anasema.

“Serikali tutakayoiunda itakuwa na watu kutoka vyama vyote na wale ambao hawana vyama. Kwanza jambo moja ambalo liko wazi ni kuwa Watanzania walio wanachama wa vyama vya siasa hawafiki hata asilimia 10 ya watu wote.

“Katika mazingira haya, uteuzi wowote unaofanywa kwa kuzingatia itikadi za vyama unaacha nje asilimia 90 ya wananchi. Na hii ndiyo siri kubwa kwa nini nchi yetu imekuwa maskini ingawa ina utajiri mkubwa wa rasilimali.

“Kuna watu wana uwezo mkubwa sana wa uongozi lakini hawana chama cha siasa. Kuna watu ni wabovu sana lakini wanapewa madaraka kwa vile ni wanachama wa CCM. Hii si haki kama kweli tunaangalia maslahi ya taifa,” anasema.

Meneja huyo wa kampeni anaamini kwamba wananchi wa Tanzania hawakuwa na mtu wa kumwamini kuchukua nafasi ya CCM lakini safari hii wamefahamu kuwa mtu huyo ni Prof. Lipumba.

Kuhusu matarajio yao kuhusu wabunge, Miraji alisema CUF inataraji kupata wabunge zaidi ya 60 Tanzania bara pekee mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu.

Alisema mwaka 2005, wakati wa Uchaguzi Mkuu, CUF ilishinda katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi nchini lakini kutokana na uchakachuaji uliofanyika, hakikupata mbunge hata mmoja Tanzania bara.

“Nitakupa mfano. Profesa Lipumba mwenyewe alimpigia kura diwani wa CUF kata ya Kunduchi, lakini matokeo yakaonyesha diwani huyo alipata kura sifuri. Katika eneo la Buguruni, CUF ilishinda katika mitaa minne lakini ikakosa diwani. Ule haukuwa uchaguzi mkuu bali ulikuwa uchakachuaji mkuu,” anasema.

Akifafanua, Miraji amesema chama chake kimeyapanga majimbo ya uchaguzi nchini katika madaraja makuu matatu ambayo ni daraja A, daraja B na daraja C.

Katika daraja A, kuna majimbo 27 ya uchaguzi Tanzania bara ambayo CUF ina uhakika mkubwa wa kuyatwaa katika uchaguzi utakaofanyika kesho.

Daraja B linahusisha majimbo ya uchaguzi ambayo chama chake kina uhakika wa zaidi ya asilimia 50 wa kuyatwaa katika uchaguzi huo. Daraja hili lina majimbo 33 ya uchaguzi.

Katika daraja C, anasema CUF inazungumzia majimbo 15 ambayo chama hicho kinaweza kushinda iwapo kitakaza kamba na kuziba mianya yote inayoweza kukifanya isishindwe.

“Utaona kwamba katika mchanganuo huo, chama kina uhakika wa walau majimbo 60 ya uchaguzi Tanzania bara. Hapo sijakwambia majimbo 25 ya Zanzibar ambayo tuna hakika nayo. Ukijumlisha unapata majimbo 85. Hapo hujazungumzia viti maalumu,” anasema.

Ndiyo maana, anasema hakuna uwezekano wa chama kimoja kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 50 katika uchaguzi huo, ukizingatia kwamba CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vitapigania viti vilivyobaki.

“Kama uchaguzi huu kweli utakuwa huru na wa haki, hakuna chama kitakachopata zaidi ya asilimia 50 ya kura. Ni muhimu kwa taifa na vyama kujiandaa kwa uwezekano wa serikali ya umoja wa kitaifa,” anasema.

Anasema kama vyama vya upinzani vingesimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi huu, CCM isingeweza kufua dafu kwa namna yoyote ile kwa vile wananchi wanataka mabadiliko.

“Watu wasifikiri kwamba sisi viongozi wa upinzani hatutaki kuungana, la, tunataka sana kuungana. Lakini tatizo ni kuwa kwa mujibu wa katiba yetu, mtu hawezi kugombea kama si mwanachama wa chama chochote cha siasa.

“Kwa maana hiyo, ili uungane na CUF au CHADEMA ni lazima kwanza uue chama chako. Hamuwezi kuungana na kila mtu akaendelea kuwa na chama chake. Kwa wenzetu wa Kenya hali ni tofauti. Katiba yao inaruhusu watu wa vyama tofauti kuungana huku kila mmoja akiendelea na chama chake,” anasema.

Miraji anasema vyama vya upinzani vinapigania kuwapo kwa Katiba mpya kwa sababu ile iliyopo inasaidia katika kukandamiza demokrasia badala ya kuishamirisha kama inavyotakiwa.

Miraji anasikitishwa na ukweli kwamba CCM imeshindwa kabisa kujitofautisha na dola katika ufanyaji wa kazi za siasa hususani katika kipindi hiki cha kampeni.

“Yaani watumishi wa umma wanakandamiza upinzani ili waonekane ni waadilifu kwa CCM jambo ambalo linarudisha nyuma sana maendeleo ya nchi yetu. Uwanja wa siasa hauko sawia baina ya washindani,” anasema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: