CUF wapoteza mwelekeo wa upinzani


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version

UPINZANI ni kitu cha msaada mkubwa sana katika siasa na maendeleo ya demokrasia ya nchi. Lakini katika nchi nyingi hii imebaki nadharia tu, katika uhalisia upinzani unaonekana kuwa ni uadui mkubwa dhidi ya chama tawala.

Vyama tawala huendelea kushikilia madaraka kupitia chaguzi za kiinimacho na hivyo kuepuka mifarakano ya kuibuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ili na chenyewe kibakie kwenye dola.

Huingia katika mikataba na chama kikubwa cha upinzani kuunda serikali ya pamoja. Hili limetokea Kenya na Zimbabwe na kwa kiwango fulani, Tanzania Visiwani.

Pamoja na malengo yake kutajwa kuwa masilahi ya nchi, hiyo inasababisha ukinzani katika uwanja mzima wa shughuli za upinzani.

Siasa za upinzani katika nchi maskini, zikiwemo baadhi ya zile zinazoendelea huwa shughuli pevu. Watu wanazoziendesha shughuli hizo wanahitaji ujasiri mkubwa; kwa maneno mengine wawe na mioyo ya jiwe.

Ukiachilia mbali Afrika ya Kusini wakati wa utawala wa kidhalimu wa ubaguzi wa rangi, kuna baadhi ya nchi katika Bara la Afrika ambako wapinzani wameuawa kikatili kabisa kwa maagizo ya walio madarakani kwa kosa tu la kuwa mpinzani kwao.

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU sasa AU), Diallo Telli wa Guinea, alionekana tishio kwa serikali ya Rais Sekeu Toure. Aliwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka na akafia gerezani kwa kunyimwa chakula.

Na huko Rwanda, rais wa kwanza wa nchi hiyo, Gregoire Kayibanda aliyekuja kupinduliwa na Jenerali Juvenal Habyarimana (mwaka 1973) alifia jela, yeye na mkewe baada ya kuswekwa ndani. Inasemekana walikufa kwa kunyimwa chakula na wakaanza kula magodoro yao ya sponji.

Tanzania ni nchi ambayo kwa kipindi cha takriban miaka 30 kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1960, upinzani haukuruhusiwa kikatiba, na waliokuwa wakijaribu kuendesha shughuli hiyo, kwa uwazi au hata kwa siri, walijikuta wanashughulikiwa vilivyo, ingawa siyo kwa namna ya nchi zilizotajwa hapo juu.
Mifano ya Tanzania, kwa upande wa Bara ni yale yaliyowapata akina Oscar Kambona, Kasanga Tumbo na Joseph Kassela-Bantu. Kule Visiwani hali ilikuwa mbaya zaidi kwa wapinzani walikouwa wanajitokeza.

Hata baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa mwaka 1992, chama tawala – CCM – kiliendelea kuvigandamiza vyama vya upinzani vilivyosajiliwa. Kwa mfano, Chama cha Wananchi (CUF) kilipata usajili wake kwa maiumivu makubwa na kilikuwa cha mwisho kusajiliwa katika kundi la vyama vya awali vilivyopata usajili.

CUF ilionekana tishio kwa chama tawala kwani, ikilinganishwa na vyama vingine kilikidhi kwa kiwango kikubwa sharti muhimu la kutaka chama kuwa chama chenye ‘utaifa’ – yaani kuwa na ufuasi kutoka pande zote mbili za muungano.

Hakuna chama kilichowahi kupata misukosuko mikubwa kutoka kwa utawala wa CCM kama CUF.

Kilianza kupata machungu mwaka mmoja baada ya kusajiliwa pale mfuasi wake mmoja alipopigwa risasi na polisi huko Shumba Mjini, Unguja wakati akikataa amri ya DC ya kutopandisha bendera ya chama chake katika tawi alilolianzisha. Na wote wanafahamu yaliyotokea miaka saba baadaye huko Pemba.

CUF ndiyo imekuwa ikiongoza kambi ya upinzani bungeni tangu baada ya uchaguzi wa mwaka 1995, na chenyewe kilikuwa kinanyakua viti vingi hasa kutoka ngome yao kuu kisiwani Pemba.

Aidha CUF imekuwa ikiunda kambi hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya vyama vingine vya upinzani.

Lakini sasa upinzani Tanzania unaonekana kuingia katika hali ya ukinzani mkubwa kuliko awali. Hali hii isiyo ya kawaida imechangiwa na vitu viwili vikubwa:

Mosi ni maridhiano yaliyofikiwa baina ya CUF na chama tawala CCM huko Visiwani baada ya miaka mingi ya siasa za uhasama na hivyo kupelekea kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya kubadilishwa Katiba.

Pili, na pengine hili halikutarajiwa na CUF, ni hali iliyojitokeza baada ya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi uliopita.

Chama kingine cha upinzani, CHADEMA, kilizoa viti vingi katika Bunge kuliko kawaida, hivyo kufanya idadi ya viti vyake vya ubunge kuzidi maradufu ya CUF.

Kikanuni, CHADEMA ilipata haki ya kuunda kambi ya upinzani bungeni, kwa mara ya kwanza kikiwa na wabunge wengi kutoka Tanzania Bara kufanya hivyo.
CHADEMA inashikilia kwamba itaunda kambi ya upinzani kwa kushirikisha vyama inavyoendana navyo katika malengo yao na siyo vyama vyote kama wanavyotaka CUF.

Ingawa haikuwekwa bayana, CHADEMA imekuwa ikivishuku vyama vingine kutumiwa na chama tawala, dai ambalo si wengi wanaoweza kulipinga.

Lakini pia lipo suala la ‘uswahiba’ uliopo kati ya CUF na CCM kutokana na maridhiano yaliyounda serikali ya pamoja Visiwani.

Wanaotoa tuhuma hizo hawasiti kutaja kwamba kuzidiwa kwake na CHADEMA katika kura za urais kunatokana na uswahiba huo. Wengi wamekihama wakikiona kuwa siyo tena chama cha upinzani kama kilivyokuwa hapo zamani.

Inadaiwa wakati wa kupiga kura kumtafuta Spika wa Bunge jipya, wabunge wa CUF walimpigia yule mgombea wa CCM. Hali hii ilijirudia katika kura ya kumwidhinisha Waziri Mkuu.

Ipo minong’ono kutoka baadhi ya wafuasi wa CUF huku Bara kutaka kujitenga na kuanzisha kitu kiitwacho ‘CUF-Bara’ ili kiendeleze mikakati ile ile ya upinzani halisi.

Wanataka uswahiba wa CCM na CUF uliopo kule Visiwani usidumaze upinzani huku Bara kwani hali ya kisiasa katika pande mbili hizi ni tofauti.

Wanadai kwamba hata CCM yenyewe imekuwa katika mivutano mikubwa baina ya uongozi wake wa kule Visiwani na wa huku Bara.

Baadhi ya wapinzani wanaoona CUF imejikita zaidi katika kusimamia masilahi ya watu wa Visiwani kuliko wa huku Bara na hivyo wanaokiona CHADEMA kama chama pekee kikubwa kinachoweza kusimamia kikamilifu masilahi ya watu Bara.

Wanaona kwa CHADEMA kushika rasmi kambi ya upinzani bungeni ni kama ‘ukombozi’ kwani sasa hivi kinaweza kuibana CCM kwa nguvu zaidi katika masuala kama vile ya kusimamia rasilimali za nchi na ufisadi.

Aidha wanadai kwamba katika Bunge lililopita kwa mfano, ni wabunge wa CHADEMA ndio walikuwa wakitoa hoja nzito nzito kuhusu masuala hayo.

Jambo la msingi ni kwamba mivurugano yoyote ndani ya upinzani, baina ya vyama au ndani ya chama, huwa inanufaisha upande mmoja tu—upande wa chama tawala.

Na kutokana na hili, itakuwa sahihi pia kusema kwamba chama tawala huanzisha au kuchochea mivurugano hiyo, kwa kutumia njia mbali za siri na za bayana.

Swali: CHADEMA ambacho sasa hivi ndicho cahama cha upinzani chenye nguvu na ufuasi mkubwa, kinaweza kujifunza kutokana na yaliyotokea kwa NCCR katika miaka ya 1990, au hata yaliyotokea kwa CUF baada ya uchaguzi wa mwaka 2000? Hadi sasa inaonekana hawajajifunza kitu kutokana na historia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: