CUF yajiandaa kuvuruga upinzani bungeni?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
Hamad Rashid Mohammed

CHAMA cha Wananchi (CUF) kinaonekana kupumbazwa na “ndoa ya mkeka” kiliyofunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM)?

Hivi sasa kimeacha kusimamia misingi yake ya asili, badala yake, kimejivisha joho la uwakala wa kuvuruga upinzani bungeni. Mara hii katika bunge la Jamhuri.

Iko wapi ile CUF iliyokuwa ikijitambulisha mbele ya wananchi kuwa ni chama cha kutetea haki za wanyonge “kwa gharama yeyote,” ikibidi hata “jino kwa jino” na “ngangari kinoma?”

Wako wapi wanachama na mashabiki wa chama hiki, waliokuwa mstari wa mbele kutetea chama chao dhidi ya dhuluma, uonevu na manyanyaso, kutoka kwa viongozi wa CCM na wale waliowaita “vibaraka wao?”

Kwa zaidi miaka 18, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, CUF kimejitambulisha mbele ya jamii na jumuiya ya kimataifa kuwa ni “chama imara” cha upinzani, Bara na Visiwani.

Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba aliwahi kusema, bila kutafuna maneno, kuwa chama chake kitaendelea kupigania “haki sawa kwa wote, katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.”

Hakuishia hapo: Alimtuhumu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame kuwa “goigoi” na ambaye alisema atastaafu akiwa hana la kukumbukiwa.

Lakini hata kabla ya katiba mpya kupatikana; tume huru kuundwa na haki sawa kwa wote kupatikana – katikati ya “haki sawa kwa wachache” – CUF tayari kimebadili mwelekeo wake.

Sasa kinatuhumiwa kudhoofisha upinzani – hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndani na nje ya bunge.

Kauli za viongozi wake wakuu, Maalim Seif Shariff Hamad na Hamad Rashid Mohammed, zinaonekana machoni mwa wengi kuwa zimelenga kutetea “ndoa” yao na CCM na siyo mabadiliko kwa manufaa ya umma wa Tanzania.

Ndoa ya CUF na CCM ilifungiwa Zanzibar ambako Maalim Seif na Rais Amani Abeid Karume walifikia “makubaliano” ambayo yameweka vyama hivyo viwili katika kapu moja la utawala wa “mashaka” – Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Hadi leo, kilichojadiliwa hadi kulegeza na hatimaye kuua mishipa ya fahamu ya CUF; na kufikia mwafaka, hakijawekwa wazi kwa wanachama, wananchi na dunia kwa jumla.

Wachunguzi wa siasa za Tanzania wanasema mwafaka unaweza kuwa umeelekezwa na moja ya mambo mawili: mchoko wa viongozi wa CUF au tamaa ya kuwa serikalini kwa gharama yoyote ile, hata kuacha misimamo yao ya awali.

Bali sasa CUF imeanza kukunjua makucha ambayo haikuwa nayo hapo awali. Inayaelekeza kwa chama kikuu cha upinzani kilichochukua nafasi yake bungeni.

Kwanza, chama cha CUF kinalaani hatua ya wabunge wa CHADEMA kutoka bungeni wakati Rais Jakaya Kikwete anazindua bunge la 10, tarehe 18 Novemba 2010.

Kinasema hatua hiyo, ni fedheha kwa CHADEMA, viongozi wake, wanachama na mashabiki. Tangu lini CUF imekuwa na maoni ya aina hii? Tumezoea kauli hizi kutoka vinywani mwa viongozi wa CCM.

Historia inaumbua. Ni viongozi hawahawa wa CUF walioshinikiza chama chao kutotambua matokeo ya urais mwaka 1995; na hata rais mwenyewe Zanzibar. Hizi zilikuwa enzi za utawala wa Dk. Salmin Amour.

Kipindi hicho, CUF iliagiza wawakilishi wake katika Baraza, kususia vikao. Nao viongozi wakuu wa CUF waliamua kususia sherehe zote za serikali, hasa sherehe za Mapinduzi, 12 Januari 1964.

Katika chaguzi mbili zilizopita – ule wa mwaka 2000 na 2005, CUF iliendelea kutotambua matokeo ya uchaguzi na rais aliyetangazwa mshindi.

Zaidi ya hayo, CUF kilihamasisha wanachama wake kuandamana. Ni katika maandamano hayo, makumi ya raia walifariki dunia baada ya polisi kutumia silaha za moto kuzima maandamano hayo.

Kwa mara ya kwanza, matukio haya yaliingiza taifa katika historia nyingine. Baadhi ya raia walikimbilia nchini Kenya na hivyo Tanzania kupoteza sifa yake ya asili ya kuwa taifa linalopokea wakimbizi na kuwa taifa linalozalisha wakimbizi.

Katika mazingira haya, nani – kati ya Maalim Seif na Hamad Rashid –
anapata dhamira ya kweli ya kusema CHADEMA wamekosea kwa hatua yao ya kutoa kilio chao kwa taifa na dunia nzima, tena kwa njia ya ustaarabu?

Inawezekana kabisa kuwa kwa matamshi haya ya viongozi wa juu wa CUF, ni kweli kwamba chama hiki kimekuwa kikishinda uchaguzi kila mara.

Lakini wenzao wa CCM wanawafahamu kwamba hawana msimamo wa pamoja katika kutetea maslahi ya nchi. Ndiyo maana wameamua kuwapora ushindi wao kama wanavyodai wenyewe kila uchaguzi mkuu unapomalizika.

Pili, kwa CUF kupinga njia yoyote ile ya amani ya kudai katiba mpya, tume huru ya uchaguzi na kuondolewa kwa sheria kandamizi, chama hicho kinadhihirisha kuwa kimeridhika na hali ya sasa ya utawala wa CCM.

Aliyaona mapema Fatma Maghimbi, mbunge wa CUF, aliyekuwa kiongozi wa upinzani bungeni, aliyeamua kuhamia CCM mara baada ya viongozi wakuu kufikia muwafaka.

Haya yanafanyika wakati Profesa Lipumba mwenyewe hajajua jinsi gani kura zake katika uchaguzi wa mwaka 2005 “zilivyohama” na hadi kupachikwa jina la kura za “kichinachina.”

Kila aliye makini anajua kuwa madai ya CHADEMA ni madai ya Watanzania na wapenda mabadiliko duniani kote. Hatua waliyochukua ni ile iliyomo katika uwezo wao lakini kuelelezea utashi, hisia na haki zao na jamii yao.

Hakuna shaka kwamba uchaguzi ulivurugwa. Wizi wa kura uligundulika. Matokeo ya baadhi ya majimbo yanafanana kwa kila kitu na majimbo mengine.

Mfano hai ni hatua ya NEC kubadilisha kura za mgombea ubunge wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema katika jimbo la Vunjo, wiki mbili baada ya kutangaza matokeo. NEC ilisema kulikuwa na kasoro katika ujumlishaji wa kura. Ikarejesha karibu kura 6,000 kwa Mrema.

Tatu, CUF wamegoma kuungana na CHADEMA kuunda kambi moja na yenye nguvu ya upinzani bungeni.

Hapa CUF wanasingizia kuwa CHADEMA wamekataa kuingiza chama cha NCCR- Mageuzi, na kwamba wao hawawezi “kuchaguliwa marafiki.”

Hivyo ndivyo Hamad Rashid, mbunge wa Wawi, kisiwani Pemba na kiongozi wa zamani wa upinzani bungeni, anavyonukuliwa akisema.

Hamad anasema, makubaliano yaliyofikiwa na vyama vyote vya upinzani, kabla ya kufungwa kwa mkutano wa tisa wa bunge, ni kuundwa kwa kambi moja itakayoshirikisha vyama vyote. Hili lina utata.

Hoja ya Hamad inavunjika kwa urahisi. Upinzani bungeni ni “ngome” moja. Hili halina ubishi. Lakini siku zote kuna chama kiongozi cha upinzani huo.

Hata kama vyama vingine havikuingia kwenye uongozi wa juu wa “kambi rasmi ya upinzani” – yaani wale wanaosubiri kuingia kwenye utawala – bado wako chini ya mwavuli wa kiongozi wa upinzani.

Lakini vyama vya upinzani haviwezi kufikia makubaliano ya aina anayosema Hamad wakati vyama vyote vilitoka bungeni na kuingia katika uchaguzi kwa shabaha moja kuu: Kushinda uchaguzi na kutwaa madaraka ya nchi kila kimoja lwake.

Kwa msingi huo – wa kila chama kuingia katika uchaguzi kwa lengo binafsi la kushinda na kutwaa madaraka – nani ambaye angeweza kuingiza chama kilichopo ikulu katika makubaliano ya kuunda upinzani? Hamad ana mizaha.

Je, Hamad anataka kusema kwamba kwa kuwa kulikuwa na makubaliano ya aina hiyo, CHADEMA wangeshinda uchaguzi wangewashinikiza kutekeleza makubaliano ya kuunda upinzani bungeni? Je, ingekuwaje kama CUF ingeshinda uchaguzi?

Au kwa mfano, CCM kingeshindwa uchaguzi, wangewalazimisha kuunda kambi kwa makubaliano waliyoingia wao – CUF na CHADEMA?

Ukweli ni huu. Kambi rasmi ya upinzani inakufa mara baada ya bunge kuvunjwa na mikataba yote iliyofungwa ya maandishi na kauli – kama kweli ilikuwepo – inakufa na bunge lililovunjwa.

Ni hivyo kwa sababu, kambi rasmi ya upinzani bungeni, si taasisi ya kudumu. Inabadilika kutokana na matokeo ya uchaguzi kwa kumtoa mpinzani kuwa mtawala na mtawala kuwa mpinzani; au mpinzani mmoja kubaki nje na mwingine kuongoza kambi.

Nne, kwa mazingira ya sasa, wenye uwezo wa kuingiza chama katika uongozi rasmi ni CHADEMA; siyo CUF. Hamad anajua kuwa kambi ya upinzani bungeni sasa, iko chini ya CHADEMA. Hawa ndio wenye uwezo wa kumuingiza wamtakaye na kumuondoa wasiyemtaka.

Hamad anajua vema kwamba mwaka 1995, chama chake kiliungana na UDP kuunda upinzani bungeni. Wakati huo, UDP ilikuwa na wabunge wanne ambao wengi hawakuwa mabingwa katika mijadala ya ndani na nje ya bunge.

Viongozi wakuu wa CUF waligoma kuungana na NCCR iliyokuwa na wanasiasa waliobobea na wasomi wa aina mbalimbali.

Wala CUF haikuona haja ya kuungana na CHADEMA ambayo wabunge wake walikuwa ni pamoja na Dk. Willibrod Slaa.

Hata mwaka 2005, CUF walianza kuunda kambi ya upinzani pekee yao. Walilazimika kuingiza vyama vingine baada ya kubanwa na kanuni za bunge kwamba sharti wawe na asilimia 12.5 ya wabunge wote.

Je, madai ya sasa ya CUF yanatoka wapi? Inapata wapi mabavu ya kulazimisha CHADEMA kuingiza NCCR katika chama kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani? Je, CUF inadhani wananchi hawakumbuki kile ambacho ilikuwa ikifanya?

Tano, hata hicho ambacho Hamad anajaribu kukitengeneza – urafiki kati ya NCCR na CUF – kimejaa utata. Ni ghiliba, hata kama katika siasa kuna usemi kuwa hakuna adui wala rafiki wa kudumu.

Ni James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR, aliyejitosa kuwekea pingamizi wabunge wa CUF kisiwani Pemba katika uchaguzi mdogo wa Pemba baada ya mauaji ya 26 na 27 Januari 2001, Unguja na Pemba,

Katika uchaguzi huo wa marudio na pingamizi la NCCR ya James Mbatia, ndimo ulizaliwa msamiati mpya wa “kura za maruhani.”

Hadi leo, Mbatia hajaeleza wanachama wa CUF, nani alimtuma kufanya kazi ile. Kazi chafu ya Mbatia ndiyo ilisababisha majimbo saba ya uchaguzi kisiwani Pemba kuchukuliwa na CCM.

Hadi sasa haijafahamika iwapo Mbatia alikuwa anajituma au alitumwa na wale ambao leo hii ndio wandani wa CUF katika serikali ya umoja wa kitaifa (CCM).
Wala siyo kweli kwamba Hamad ana mapenzi makubwa kwa NCCR. Anataka kuitumia kwa manufaa ya CUF na labda hata kuisajili katika muwafaka wake na CCM.

Kisichofahamika kwa wengi ni kwamba tangu mwaka 2005 Hamad amekuwa kiongozi wa upinzani ndani ya bunge. Kwa nafasi yake hiyo, serikali ilikuwa inampa gari, nyumba na marupurupu mengine.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka bungeni, kila mwaka kiongozi wa upinzani hutengewa na serikali karibu Sh. 200 milioni.

Baadhi ya wafanyakazi wa Bunge wanadai kuwa hakuna mahali popote katika kumbukumbu zao, panapoonyesha fedha hizo kutumiwa kwa kazi ya kuendesha shughuli za kambi ya upinzani.

Ni Hamad na maofisa wa bunge pekee wanaoweza kuzungumzia kwa ufasaha matumizi ya fedha hizo.

Sasa uchaguzi wa mwaka huu, umemuondoa Hamad katika kiti chake. Umechukua gari lake. Umebomoa nyumba yake. Umehamisha marupurupu yake.

Huo ndio msingi wa Hamad kutaka kuungana na NCCR. Anataka kulazimisha kuundwa “kambi ndogo” ambayo, kwa msaada wa CCM, anataka itambuliwe bungeni ili aendelee kupata marupurupu kwa “dirisha la banda la uwani.”

Je, Ofisi ya Spika itakuwa tayari kuingia katika gharama ambazo ziko nje ya bajeti ili kumfurahisha Hamad? Je, serikali iko tayari kuingia katika kinachoelekea kuwa aina fulani ya ufisadi kimatumizi?

Je, Spika Anna Makinda anaweza kujiingiza katika mchezo mchafu wa kusaidia kubadilisha kanuni za bunge ili kuibeba CUF na kuitia hasara serikali? Hekima inasema, “Hawezi.” Hawezi kukubali kufadhili mradi huu binafsi wa Hamad au CUF.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: