CUF yapania kufuta vidonda vya zamani


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

KIPINDI cha kampeni kimeanza Zanzibar. Chama kikuu cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF),kimefungua pazia la kutafuta ridhaa ya kuongoza serikali kwa mara nyingine.

Mgombea wake wa kiti cha urais, Maalim Seif Shariff Hamad, ameanza kutoa ahadi kwa wananchi kwa yale anayokusudia kuyatekeleza pindi akipewa ridhaa ya kuongoza chini ya mwamvuli wa chama hicho ambacho tangu mwaka 1995 kimekuwa kikimaliza uchaguzi kwa malalamiko kwamba kinaporwa ushindi.

Zanzibar inafanya uchaguzi mkuu wake wa tatu tangu mfumo wa vyama vingi uliporudishwa kwa sheria ya bunge ya mwaka 1992, ambayo ilijumuisha suala la siasa kama la muungano kinyume na ilivyokuwa awali Zanzibar ikiendesha siasa zake mbali na Tanzania bara.

Wazanzibari wanatarajiwa tarehe 31 Oktoba mwaka huu, kupiga kura ya kuchagua rais wao, wajumbe wa baraza la wawakilishi na madiwani wanaounda mabaraza ya madiwani kwenye halmashauri zake kumi.

Uchaguzi huu unafanyika wakati mazingira yakiwa tulivu sana Unguja na Pemba.

Hali hii imetokana na jitihada za viongozi wakuu wa CUF na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hususani makamu wake, Amani Abeid Karume, ambaye anamaliza muhula wake wa pili wa miaka mitano wa kuiongoza Zanzibar.

Dhamira ya maridhiano iliyojengwa na pande hizi mbili, ni moja ya ajenda muhimu katika manifesto ya CUF kwa ajili ya uchaguzi ujao. CUF inaahidi kuwa itajenga uongozi mwema, unaojali haki za binadamu na unaofuatana na dhamira ya siasa za maridhiano chini ya utawala wa haki na sheria.

Kwa kuwa chama hiki kilishatangaza tangu mwaka 2005 kuwa kikipata ridhaa ya wananchi kitaunda serikali ya umoja wa kitaifa, kinaendelea kusisitiza kuwa serikali yake itaheshimu ridhaa hiyo ya wananchi.

Katika ilani yake, CUF inaahidi hakutakuwa na mtu yeyote aliye juu ya sheria kwani chini ya mfumo wa demokrasia sahihi ya vyama vingi, si rais wala kiongozi mwingine ataruhusiwa kutumia mamlaka aliyopewa kisheria kukandamiza watu wengine.

Kwa mantiki hiyohiyo, serikali ya CUF itatunga sheria mpya kuepusha utumiaji mbaya wa madaraka ya umma. Itaanzisha taasisi mahsusi ya mfano wa TAKUKURU ya Tanzania Bara ili kuzuia na kupambana na tatizo hilo.

Sheria zote kandamizi ikiwemo ya magazeti ya mwaka 1984 zitafutwa na kutungwa sheria ambazo zinatunza uhuru na misingi ya demokrasia na haki za biandamu.

Kwa kutambua ukweli kwamba wananchi wengi wa Zanzibar wamekuwa wakiishi na maumivu makali yanayotokana na kudhulumiwa kwa aina mbalimbali, ikiwemo kudhalilishwa na kuteswa chini ya mwamvuli wa dola, CUF inaahidi kufungua ukurasa mpya wa maelewano kwa kuwataka wananchi wote kusameheana na kusahau mabaya waliyotendeana katika kipindi chote cha siasa chafu.

Kwenye eneo la haki za binadamu, CUF inaahidi kurudisha heshima ya haki hizo pamoja na ulinzi wake kwa kutekeleza kikamilifu tamko la ulimwengu la haki za binadamu na kuanzisha ofisi mahsusi ya haki za binadamu itakayokuwa na jukumu la kuchunguza malalamiko dhidi ya wananchi na kuchukua hatua dhidi ya waliolalamikiwa.

Ni ahadi ya CUF kwamba serikali itakayoiunda italinda na kuuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari kwa kuondoa aina yoyote ya udhibiti wake ili kuviwezesha kukua na kuwa jukwaa la kutumikia wananchi.Hata uhuru wa kuabudu utalindwa sawasawa.

CUF inakusudia kuanzisha elimu ya haki za binadamu katika mitaala kuanzia shule za msingi kama hatua ya kuzijenga haki hizo kwenye akili za watoto.

Katika kukomaza maridhiano ya kisiasa yaliyopo sasa nchini, serikali ya CUF inakusudia kuheshimu na kutekeleza kikamilifu mambo yote yaliyokubaliwa kupitia maridhiano hayo.

Kadhalika, itatekeleza mapendekezo mengine yaliyotokana na muafaka wa kisiasa wa mwaka 2001, yakiwemo yale yanayohusu urekebishaji wa mifumo ya utendaji iliyojikita katika vyombo mbalimbali vya serikali ambayo inajulikana inavyobagua watu kwa misingi ya kisiasa.

Chama hicho pia kinaahidi kutambua maumivu waliyonayo baadhi ya wananchi ambao kutokana na msimamo wao wa kisiasa, wameathirika kwa njia mbalimbali.

Wapo watu katika kipindi cha siasa chafu zilizoibua mgogoro wa kisiasa, walivunjiwa nyumba zao; walifukuzwa kazi serikalini; walisababishiwa ulemavu kwa kuteswa wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola. Hawa CUF inaahidi itawaangalia.

Ingali kwenye kumbukumbu kwamba baadhi ya watu walikufa kutokana na mishtuko waliyoipata baada ya kuvunjiwa nyumba walizozijenga.

Nakumbuka mwandishi wa habari aliyefariki dunia siku chache baada ya nyumba yake mpya aliyoijenga eneo la Mtoni Kidatu kuvunjwa kwa tingatinga la serikali wakati wa utawala wa Dk. Salmin Amour Juma.

Mwalimu Omar aliyekuwa mtumishi wa serikali na kutumikia kwa muda mrefu katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, alipata mshituko wa moyo na kulazwa hospitali ambako alikata roho baadaye. Waathirika wa mfano wake ni wengi.

Lakini wapo watumishi wengi wa serikali walifukuzwa kazi au kujengewa mazingira yaliyowalazimu kuacha kazi kwa sababu tu walionekana hawashabikii CCM. Baadhi yao walinyimwa fursa ya kustaafu na kupata mafao yao baada ya kufanya kazi ya serikali kwa zaidi ya miaka 30 na umri wao ukiwa tayari lala salama.

Kulingana na makubaliano yaliyomo katika muafaka wa 2001 uliosainiwa na viongozi wakuu wa CCM na CUF kwenye viwanja vya Ikulu ya Zanzibar, wote hawa walipaswa kulipwa kifuta jasho na serikali.

Hakuna kilichofanyika hadi sasa zaidi ya viongozi wa serikali ya CCM kuendelea kutoa visingizio mbalimbali ikiwemo kudai hakuna serikali ya nje iliyotimiza ahadi ya kusaidia fedha.

Pamoja na mengine, Ilani inaelezea pia maeneo yahusuyo Uchumi, Biashara, Kilimo, Elimu, Afya na Ukimwi, na Kuendeleza makundi maalum.

Hata baada ya Zanzibar kurudishiwa utawala wa kikatiba mwaka 1980, haikupata tena kuongozwa vema kwani hakuna viongozi waliothubutu kuongoza kwa kujali misingi ya uongozi bora na uongozi uliotukuka – ukiacha kipindi kifupi cha mwaka mmoja (1984-1985) ambapo serikali ya mapinduzi Zanzibar ilishikwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: