CWT wakomboeni walimu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Mtazamo

TISHIO la walimu takriban wote wa mkoa wa Kigoma la kujitoa uanachama katika Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kile wanachoamini kuwa ni “dhulma” dhidi ya maslahi yao, linatoa changamoto nzito kwa uongozi wa chama hicho.

Ni changamoto inayotishia umoja na mshikamano kati ya uongozi na wanachama wake nchi nzima.

Walimu wanasema wazi wamechoka kufanya kazi kwa kipato kidogo, tena bila kupandishwa madaraja na mshahara. Isitoshe, wamechoka kuona CWT yenyewe inaishi kwa kutegemea mapato ya asilimia mbili kutoka mishahara midogo ya walimu.

Wamekuwa wakiuliza swali bila ya kujibiwa. Kwamba ni lini utaratibu wa kukatwa mishahara yao bila ya ridhaa utakoma. Wanahoji inakuaje mwalimu anaanza kukatwa mshahara wake mara tu akishaajiriwa hatua iliyo kinyume na sheria?

Wanataka makato ya asilimia mbili kwenye mishahara yao yasitishwe, na fedha walizokwishakatwa warejeshewe. Bila hivyo, wameapa kuanzisha mgogoro mahakamani.

Hapa ndipo kibarua kwa uongozi kilipo. Wanayo safari ndefu ya kuelimishana wajibu wa vyama vya wafanyakazi na namna vinavyoendeshwa.

CWT hawapaswi kuchukulia kuwa walimu wote wanajua umuhimu wa vyama vya wafanyakazi na sababu ya kuanzishwa kwake. Kwa baadhi yao kutaka kujitoa inaonyesha kuna tatizo mahali fulani.

Je, ni kutoshughulikiwa maslahi yao? Ni kukosekana fursa ya kukutana sehemu zao za kazi na kujadili kero zinazowakabili hivyo kutegemea tu hatua zinazochukuliwa na makao makuu?

Kama walimu huzuiwa kutumia haki yao ya kidemokrasia kukutana na kujadili masuala yanayohusu maslahi yao, ni nani anayewasikiliza? Wakuu wa shule au vyuo ambao ni wawakilishi wa mwajiri?

Kweli, kama wananyimwa fursa ya kukutana sehemu zao za kazi ili ‘kubwaga mioyo yao’ kwa vyovyote vile hawawezi kuona faida ya kujiunga na CWT.

  Lakini ni kweli walimu wote wa mkoani Kigoma hawanufaiki na CWT? Au ni kweli hawajui kwa nini baada ya kumaliza masomo vyuoni waliingizwa moja kwa moja kuwa wanachama wa CWT?

Inawezekana tabia ya viongozi wakuu wa kitaifa kutotembelea wanachama mikoani ili kusikiliza kero zao imechangia.

Baada ya kuazimia kujitoa, walimu wamekaa wakatulia na kuanzisha au kujiunga na chama kingine au wamebaki huru ‘kila mmoja na lwake?’

Inawezekana chama hakijatekeleza mambo ambayo walimu wote nchini yanawasumbua. Au tuseme CWT imeteleza? Vyovyote iwavyo, ni busara walimu kufikiria upya tishio lao la kujitoa CWT.

Kwamba ‘bifu’ yao na CWT inamnufaisha nani, wao au mwajiri mkuu ambaye angependa kuona vyama vyote vya wafanyakazi vinafutika ili dhulma izidi pasina kikwazo?

Kujitoa CWT wanamkomoa nani hasa? Viongozi wa makao makuu au wao wanaohitaji chombo madhubuti cha kuwatetea? Wafikirie kama kweli mwalimu mmoja mmoja atakuwa na ubavu wa kukabiliana na waajiri wakorofi ambao wanasukumwa lakini bado ni wajeuri?

CWT ni miongoni mwa vyama vyenye nguvu kubwa dhidi ya mwajiri mkuu – serikali. Mwaka 2008 iliitisha mgomo nchi nzima kushinikiza serikali ilipe malimbikizo ya mishahara, posho mbalimbali, nauli na nyongeza za mishahara.

Mwaka 2009 iliitisha tena mgomo lakini serikali ikatenga fungu la fedha na kuanza kulipa madai ya walimu ikiwemo kupandisha madaraja waliostahili.

Kufikia sasa, CWT inajivunia mafanikio iliyoyapata katika kuibana serikali kwani Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imebaki kushughulikia masuala ya uratibu tu baada ya kufanya kazi kubwa ya kuhakiki madai yao.

Hatua iliyobaki ni wajibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Jukumu la CWT sasa liwe kupigania pamoja na mambo mengine hadhi, heshima, staha na murua wa walimu waheshimike na kuthaminiwa.

0776 383 979
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)