Daily News kwazidi joto


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 14 September 2011

Printer-friendly version

MGOGORO unaokabili kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) umezidi kutanuka baada ya kiongozi wa wafanyakazi kufungua kesi mpya dhidi ya menejimenti.

Kesi hiyo imefunguliwa na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa taasisi za elimu ya juu, sayansi, teknolojia, habari na utafiti (RAAWU) Tawi la TSN, Peter Keasi.

Keasi amefungua kesi hiyo kupinga uhamisho wa kikazi aliopewa mwezi uliopita kupitia barua binafsi ya Kaimu Mhariri Mtendaji wa TSN, Mkumbwa Ally.

Katika uhamisho huo, Mkumbwa ambaye ni mmoja wa waandishi wa habari wakongwe nchini, alimjulisha Keasi uhamisho wa kwenda kituo cha TSN Dodoma kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam.

Akiwa Dodoma, Keasi katika barua ya 22 Agosti 2011, ameelekezwa kuwa mwandishi mwakilishi wa mkoa, cheo kisichokuwa miongoni mwa vilivyopo katika muundo wa TSN. Ametakiwa kuripoti kituo kipya 29 Agosti.

Msingi wa kesi aliyoifungua Keasi katika Mahakama ya Kazi na kusajiliwa kwa Na. 61/2011, ni kupinga uhamisho huo akidai kuwa si halali kisheria.

Kesi hiyo itasikilizwa na Jaji Regina Rweyemamu huku Keasi ambaye naye ni mwandishi wa habari mwandamizi, akiwakilishwa na Benjamin Mwakagamba, wakili wa kampuni ya BM Attorneys.

Moja ya maombi ya Keasi katika kesi hiyo, ni kutaka mahakama izuie uhamisho huo mpaka shauri la msingi lililopo Tume ya Upatanishi na Usuluhishi (CMA) litakapoamuliwa.

Shauri hilo lilifunguliwa na uongozi wa RAAWU ngazi ya taifa kwa niaba ya wafanyakazi wa TSN.

Madai ya wafanyakazi yanamgusa moja kwa moja Mkumbwa anayedaiwa kutumia vibaya madaraka ikiwemo kutoa ajira bila ya kufuata kanuni za utumishi na miongozo ya utendaji TSN.

Hatua hiyo imekuja baada ya serikali kuchelewa kutatua mgogoro wa muda mrefu unaohusisha wafanyakazi kwa upande mmoja na menejimenti inayoongozwa na Mkumbwa.

Wafanyakazi wamekuwa wakilalamikia Bodi ya TSN kutochukua hatua muafaka kwa wakati huku duru za taarifa ndani ya kampuni hiyo na wizara ya habari, zikisema kiongozi huyo amekuwa akikingiwa kifua na bodi hiyo.

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Hawa Mmanga alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo dhidi ya bodi, alisema hafahamu lolote kuhusu mvutano kati ya wafanyakazi na menejimenti.

“Sifahamu lolote kama kuna mvutano huo. Naomba unipe muda wa kuzungumza na mwenyekiti aliyepita. Vilevile nipe muda wa kuzungumza na hao viongozi wa RAAWU Tawi la TSN, na baadaye nitakuhitaji tuzungumze ana kwa ana,” alisema kwa njia ya simu juzi Jumatatu.

Hata hivyo, Mmanga ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi aliyokuwepo Wilson Mukama, baada ya kuteuliwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema hakuwepo nchini na kwamba hajapata kukutana na wajumbe wenzake.

“Kwa sasa nipe muda maana sifahamu hayo, lakini baada ya kufuatilia na kukutana na wenzangu katika bodi, tutachukua hatua haraka kwa kuitisha kikao cha bodi tuyajadili,” alisema.

Taarifa zinasema Mkumbwa amekuwa na kawaida ya kulipa posho mbalimbali kwa wajumbe wa bodi wanapomtembelea ofisini kwake kwa maelezo kuwa huwapo katika shughuli zao za bodi.

Mvutano katika TSN umekuwa ukikua bila ya kupatiwa ufumbuzi na kusababisha utendaji usio wa kiwango wa shughuli za kampuni hiyo inayochapisha magazeti ya Daily News, Sunday News na HabariLeo.

Kampuni hiyo imekuwa haijapata kiongozi wake tangu alipomaliza mkataba wake Isaac Mruma mwaka 2009.

Serikali ilimkatalia Mruma kuongeza mkataba wa kazi bila ya kueleza hasa sababu wakati utendaji wake uliinua kampuni hiyo kiuchumi na wafanyakazi walikuwa wakisifia namna alivyokuwa akiangalia maslahi yao.

0
No votes yet