Darasa elekezi kwa wana Igunga


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 17 August 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

JIMBO la Igunga limerudishwa chumba cha mtihani wa uchaguzi. Wananchi watapewa makaratasi ya mtihani mpya baada ya walimu wababaishaji (CCM) kutoa siri za mshindi wa Oktoba 2010 kuwa ni gamba.

CCM, wanaojiita walimu wa siasa na walezi wa demokrasia, kupitisha jina la Rostam Aziz kwa mbwembwe, walipiga kampeni wakidai ni chaguo sahihi. Lakini Febrauri mwaka huu, wakaanzisha falsafa ya ‘kujivua gamba’ na kuitumia kumkana mbunge huyo tangu mwaka 1994 aliporithi kiti cha Charles Kabeho aliyefariki dunia.

Kamati Kuu inayoongozwa na Katibu Mkuu Wilson Mukama na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi Nnape Nnauye, ikazunguka nchi kuhimiza wabunge iliowaita Mapacha Watatu, akiwemo Rostam, wajiondoe kwenye chama.

Walimu hawa wanadai mapacha hao wamesababisha chama kukosa ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliopita. Magamba.

Duniani kote mwalimu mbabaishaji ni hatari maana huwa hana uhakika wa anachofundisha, hana uhakika na majibu ya maswali anayotoa na hujaza visingizio juu ya matokeo mabovu. CCM ni mfano wa mwalimu wa siasa mbabaishaji.

Septemba 15, 2007 CHADEMA ilitaja majina ya watu 11 maarufu nchini iliodai ni magamba kwa uchumi wa nchi. CCM ikakanusha na ndiyo maana iliwapitisha hata Mapacha Watatu kuwania ubunge.

Rais Jakaya Kikwete ndiye aliwapigia debe, akinyanyua mikono yao ili kuwauza.

Wakazi wa Igunga, wakiwa na imani kubwa na rais wao na Mwenyekiti wa CCM, walimwamini wakampa kura yeye, mbunge wao Rostam bila shaka na madiwani – mtindo wa mafiga matatu.

Mukama na Nape wasifiche nyuso zao, waende Igunga. Wakawafafanulie tangu lini mbunge wao akawa gamba?

Maana kama wakati wa uchaguzi alikuwa safi, magamba aliyopachikwa leo yangesababishaje chama kushindwa kule? Ikiwa magamba yaliota tangu 2010, walimpitisha kwa sifa gani?

Isitoshe, kama Rostam ni gamba mbona alishinda kwa kishindo? Mbona walioshindwa ni kutoka maeneo ambako CCM haikuwa inatilia shaka? Nani gamba, wale walioshindwa au aliyeshinda?

Wakati anatangaza kuachia ubunge na nafasi zote alizokuwa anashikilia katika chama, Rostam alijiweka miongoni mwa wanachama walioasisi falsafa ya kujivua gamba, kwa lengo la kujitathmini.

Alisema kutokana na chuki na siasa uchwara zilizoingia CCM, hakuona njia nyingine bora ya kulinda heshima na hadhi yake isipokuwa kujiuzulu.

Uamuzi huu ndio unawarejesha wana-Igunga kwenye chumba cha mtihani ili kuweka tiki tena baada ya mtihani wa kwanza kuharibiwa na walimu walewale waliodai Rostam alikuwa jibu la matatizo yote Igunga lakini baadaye wakadai ni gamba.

Kwa maelezo mengine, CCM iliwaingiza mkenge Igunga. Mwalimu akitoa majibu yasiyo sahihi kisha yeye mwenyewe akakiri hivyo hawezi kuaminika tena. Hii ndiyo moja ya sababu za kushamiri kwa twisheni ‘rasmi’ na huchangia ufaulu.

Majimbo yaliyong’ang’ania mafunzo ya walimu wa CCM ndiyo yenye wabunge wanaopiga usingizi au wenye magamba. Majimbo yaliyozingatia twisheni au mafunzo mbadala ndiko tunashuhudia wabunge motomoto ambao wanatoka CUF, CHADEMA na NCCR- Mageuzi.

Hiyo ni mifano michache ambayo Igunga wanaweza kujifunza katika darasa elekezi. Wakazi wake wakifika kwenye kampeni watajifunza mambo mengi – fursa ya masahihisho baada ya majibu batili waliyopewa na CCM.

Watajifunza kwamba kufanya kosa si kosa ila kurudia kosa; kwamba CCM bado wanajivua magamba huenda na chaguo lao akawa gamba. Igunga wazinduke!

0
No votes yet