Darasa la busara la Rais Kikwete


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

TULIMSHUHUDIA Rais Jakaya Kikwete mwaka 2006, akishika chaki na kuwapiga msasa mawaziri katika kipindi cha kwanza cha awamu yake.

Alianza darasa kumwelekeza kila waziri majukumu yake, kisha akawakusanya wote katika ‘chumba cha mtihani’ wa semina elekezi katika hoteli ya kitaliii ya Ngurdoto, Arusha.

Baadhi walifeli, lakini aliendelea nao. Siku chache baadaye waliofeli mtihani wa uadilifu, walikumbwa na kashfa ya ufisadi iliyosababisha serikali yake kuvunjika Februari 2008 huku mwingine akikiri kuweka vijisenti benki za nje.

Semina elekezi haikusaidia sana. Rais Kikwete alimaliza ngwe ya kwanza ya uongozi huku mabehewa yaliyobeba mawaziri yakigongana ovyo.

Ameanza ngwe ya pili umaarufu wake ukiwa umeshuka sana na anatumia staili ileile; kuandaa darasa kwa kila wizara na kutoa maelekezo. Hakuna fununu kama wataingizwa wote kwenye chumba cha mtihani wa semina elekezi. Tusubiri.

Katika wizara za mawaziri wazoefu, rais hakuishia kusikiliza hotuba zao, aliwakatisha mara kwa mara aliposikia maelezo aliyoona yana ukakasi masikioni na kujibizana nao. Halafu akatoa maelekezo au maagizo anataka nini kifanyike katika kipindi hiki cha uongozi wake.

Ujumbe mwafaka kwa wakati huu, ambao ndio msingi wa makala hii, aliutoa alipotua Wizara ya Ujenzi inayoongozwa na Dk. John Pombe Magufuli na naibu wake, Dk. Harrison Mwakyembe.

Rais Kikwete alimwambia Waziri Magufuli kwamba wakati wa kubomoa nyumba za watu waliojenga kwenye hifadhi ya barabara, iangaliwe historia ili wale waliojenga nyumba kabla ya ujenzi wa barabara walipwe fidia, lakini waliokuja baadaye wakumbwe na maumivu.

“Wakati mwingine ni lazima moyo wa huruma wa kibinadamu uwepo, msitumie ubabe. Maeneo mengine angalieni historia; waliojenga kabla ya barabara kupita walipwe fidia, lakini kuna wengine walijenga baada ya barabara kupita, hawa wabomolewe,” alisema.

Rais ameingiwa na moyo wa huruma kuhusu wananchi wake akamtaka Waziri Magufuli atumie busara kusimamia sheria hiyo ya kubomoa nyumba kwenye hifadhi ya barabara.

Bila shaka rais amegundua kwamba hakukuwa na busara katika utungaji wa baadhi ya sheria, hakuna busara katika utekelezaji wake na kwa hiyo hakuna ubinadamu.

Maswali yanakuja ukosefu wa busara, moyo wa huruma au ubinadamu ni katika uvunjaji wa nyumba zilizojengwa katika hifadhi ya barabara tu?

Kama ni suala la kutazama historia ni waliojenga katika hifadhi ya barabara tu? Sheria iliyotungwa bila busara ni katika barabara tu? Vipi maeneo mengine ambayo wananchi wanalalamika kuvunjiwa na kuchomewa nyumba, kuhamishwa kwa nguvu bila fidia?

Kwa kuwa ushauri wa mkubwa ni sawa na amri, serikali ipitie, kwa kuzingatia historia na busara, sheria zote zilizokwishaumiza watu kama katika upanuzi wa hifadhi ya wanyama, madini na uwekezaji mwingine.

Serikali ilijali vipande vya fedha vya wawekezaji, ikakosa busara, ikagawa maeneo bila kujali historia, hivyo wananchi hawakulipwa fidia.

Mathalani, serikali haikujali historia wala busara kuangalia haki ya wakazi wa kijiji cha Kakola ulipo mgodi wa madini ya dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa sasa na African Barrick Gold ya Canada.

Serikali inadai eneo hilo hadi kufikia mwaka 1994 kulikuwa na miti na ndege tu, lakini aliyekuwa Mbunge wa Msalala, Bhiku MS Bhiku aliliambia Bunge mjini Dodoma 26 Julai 1996 kwamba Kakola ilishasajiliwa kuwa Kijiji cha Ujamaa mwaka 1974.

Bhiku katika taarifa yake bungeni alikusudia kupinga taarifa ya serikali iliyowasilishwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Shija akisema kijiji hicho kilisajiliwa mwaka 1994 na ikapewa Kampuni ya Kahama Mining.

Ili kutekeleza azma hiyo, mkataba waliotiliana saini kati ya serikali na kampuni ya kwanza iitwayo Kahama Mining Corporation Limited (KMCL), kwa mujibu wa Bhiku unaonyesha kuwa, Kakola hakukuwa na watu, walikuwepo ndege katika misitu mikubwa. KMCL ni kampuni tanzu ya Sutton Resources ya Canada.

Ili wasiumbuke, mkuu wa mkoa Tumaniel Kihwelu alifika Kakola na kuwataka waondoke katika muda wa saa 24 tu zibaki sauti za ndege tu. Kwa bahati mbaya haikuwezekana kuondoa umati wa watu wapatao 10,000 kwa muda mfupi; magreda ya mwekezaji chini ya usimamizi wa polisi yakafika kusawazisha na kufukia eneo hilo na waliokuwa chini wakichimba walifia ndani.

Ukweli utabaki, hata kama wachimbaji hawakuwa na leseni na hata kama Kakola hakikusajiliwa kama kijiji, kulikuwa na maelfu ya watu waliokuwa wanachimba dhahabu kwa kutumia nyenzo duni.

Ndiyo maana Kihwelu alikuwa anakuta watu wa kuzungumza nao, siyo ndege. Hivi watu walioanza kuchimba dhahabu mwanzoni mwa 1970 serikali ilitumia busara mwaka 1994 kudai watu hao ni wavamizi ila mmiliki halali ni KMCL?

Kwa vile rais amesema historia ya mahali iangaliwe na busara itumike, hii ndiyo fursa adhimu ya kufidia wakazi asilia waliohamishwa kiubabe na kuwakosesha mashamba yao na maeneo ya uchimbaji.

Maeneo yanayopaswa kupitiwa upya kwa kuzingatia historia ni yote yanayozunguka migodi kama Bulyanhulu, Geita, North Mara, Buzwagi, Tulawaka, Nzega ili walioathirika walipwe haki zao.

Maeneo mengine yanayopaswa kuangaliwa upya ili wahusika walipwe stahili zao ni watakaothirika kama Mkuju River (Ruvuma) na Bahi watakaohamishwa kupisha uchimbaji wa madini ya uranium.

Vilevile historia iangaliwe katika maeneo kama ya Chanika, Ilala na kata ya Msangaji, Mbarali waliohamishwa kwa nguvu tena nyumba zao kuchomwa moto bila fidia ili kupisha eneo la hifadhi ya wanyama.

Hivi serikali inapata faraja gani wananchi wanapolialia huku mwekezaji aliyeachiwa eneo akila tambuu kwa raha zake? Serikali inajisikiaje kuhamisha watu kila siku wakati kutokana na zoezi hilo, wengi wanatumbukia katika umaskini?

Tayari Rais Kikwete, japo bado anakabiliwa na matatizo mengi, ameonyesha njia kwa kurejesha baadhi ya nyumba za serikali katika maeneo nyeti ambazo ziliuzwa kwa watu binafsi.

Ametumia busara kwa kuwaelekeza wanasheria wa serikali wapambane katika mahakama kuu kuhakikisha tozo ya Sh. 94 bilioni iliyopewa kampuni ya Dowans dhidi ya TANESCO hailipwi.

Busara itumike kuandaa katiba ili itoe na kulinda haki za kila mwananchi kuishi popote, na ikitokea serikali inalihitaji eneo, kama Bahi kwa uchimbaji wa uranium, wananchi watakaohamishwa kupisha mradi huo mkubwa kwa uchumi wa nchi, walipwe fidia inayostahili ili wakaanze maisha sehemu nyingine bila usumbufu wala malumbano na serikali.

0658 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: