Dawa ni kuwapa haki wafanyakazi


editor's picture

Na editor - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete juzi alizungumza na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioko mkoa wa Dar es Salaam kuhusu mambo mawili.

Kwanza, mkutano wa Kiuchumi wa Dunia, ambao utahudhuriwa na viongozi wa kimataifa. Pili, tishio la mgomo wa wafanyakazi.

Kuhusu mkutano huo wa kimataifa, Kikwete alisema kwamba utakuwa na manufaa kwa Watanzania.

Kuhusu mgomo wa wafanyakazi uliotangazwa na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (TUCTA) kuanza leo nchi nzima, rais alisema akiwa mwajiri mkuu wa watumishi serikalini anapiga marufuku mgomo huo.

Hatutaki kuhoji kama rais ana uwezo kisheria, kwa mujibu wa katiba kupiga marufuku mgomo, lakini tumesikitishwa na namna alivyoamua kuzungumza na wazee wa CCM wengine wakiwa hawana kazi kutoa vitisho vya kutumia polisi kujeruhi wafanyakazi.

Tulitarajia rais angekaa na kuzungumza na wafanyakazi. Lakini rais anapotumia vitisho na lugha isiyofurahisha ya kuwaita viongozi wa TUCTA waongo, wanafiki, wazandiki na vigeugeu anakaribisha malumbano, kejeli na mvutano wa muda mrefu. Hizi ni dalili za kukosekana hekima katika utatuzi wa migogoro.

Rais amesema pia kwamba hawezi kutoa ahadi ya kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa vile pesa hizo hazipo. Lakini si yeye aliyeahidi kupitia kaulimbiu yake Maisha Bora kwa Kila Mtanzania?

Si yeye aliyeahidi kabla na baada ya kuingia madarakani kupitia upya mikataba ya kinyonyaji ya madini, kupunguza viwango vya umeme, kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi na kurekebisha mishahara yao? Mbona leo anafanya kinyume chake?

Imerekebisha mishahara ya wanasiasa; mbunge huondoka na mshahara wa Sh 7 milioni kwa mwezi na posho ya Sh 150,000 kwa siku. Maeneo mengine yaliyoboreshwa ni majeshi ya ulinzi na usalama, na taasisi za fedha —mabenki, TRA, mashirika ya hifadhi ya jamii.

Aidha serikali imewakumbatia walarushwa, wezi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Imegoma kuchunguza kampuni za Deep Green, Kagoda Agriculture na imezima mjadala wa Richmond.

Je, tujue kwamba serikali yake imeshindwa? Ni muhimu rais akafahamu kwamba njia aliyochagua kumaliza tatizo hili si nzuri, haina tija kwake binafsi na hata kwa chama chake.

Badala yake, hatua hiyo aliyoichukua itazidi kumjengea chuki kwa wafanyakazi, jamii na kulimega taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: