DC asakwa na polisi 


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

POLISI Mkoa wa Kinondoni, Dar es Salaam wanamsaka Mkuu wa Wilaya ya Tarime,  John Henjewele kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi mdogo wake wa kike, Rose Henjewele.

Kamanda wa polisi mkoani humo, Charles Kenyela amemtaka DC Henjewele ajisalimishe haraka ili sheria ichukue mkondo wake.

“Nasikia amemjeruhi vibaya dada yake. Hili ni kosa la jinai; tunamtafuta ajibu tuhuma hizi. Tunamtaka ajisalimishe haraka,” alisema Kenyela.

Kenyela alisema taarifa za awali zinasema kwamba mkuu huyo wa wilaya, akishirikiana na ndugu zake wengine wawili, walitaka kumshawishi mama yao kuuza nyumba; lakini Rose hakutaka hilo lifanyike.

Kwa mujibu wa Rose, hilo lilitokea Ijumaa iliyopita, Mbezi Salasala, Dar es Salaam, baada ya DC kufika nyumbani kwa Rose, kutekeleza kilichoitwa mipango yake ya kuwanyang’anya nyumba yenye thamani ya Sh. 72 milioni.

Tuhuma hizo zimeripotiwa katika kituo cha polisi Kawe, jijini Dar es Salaam na kuandikishwa kwa taarifa Na. KW/RB/2442/2012 ya Machi 16, mwaka huu.

Kutokana na kipigo hicho, Rose aliyeumizwa usoni na kuvimba macho na shingoni, ametibiwa katika hospitali ya Mwananyamala kwa kudungwa sindano na kupatiwa dawa nyingine za vidonge.

Amelieleza MwanaHALISI kuwa chanzo cha kupigwa kwake ni kuingilia kati mpango wa kaka zake wawili, John (DC) na Benedict, wakishirikiana na mwanasheria ambaye hajafahamika, kutaka wachukue nyumba yao waliyonunua kwa ‘fedha za urithi.’

Rose alidai kuwa kaka zake hao, walitaka kumrubuni mama yao mzazi, Benedina Henjewele ambaye ni mzee na hajiwezi, kuwatilia saini, ili ‘kugawa’ nyumba hiyo kwa Benedict, kwa malengo wanayoyajua.

Wakati wanaendelea kumshawishi mama huyo, Rose ambaye anadai alikuwa tayari amesikia mpango wao, alitokea na kumpiga picha mwanasheria huyo na kuanza kuwarekodi kwenye kamera.

“Walipoona hivyo, John alinipiga makofi usoni na Benedict akavuta mkufu na kunijeruhi shingoni, kisha akaninyang’anya kamera na kumkabidhi John. Walishirikiana wote wawili kunipiga,” alisema.

Alipopata fursa ya kuchomoka, anasema alikimbia na kuondoka na viatu vya mwanasheria na Benedict hadi kwenye ofisi ya serikali za mitaa alikopewa barua kwenda kuripoti polisi Kawe.

DC Henjewele hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi kuzungumzia suala hilo, na pale ilipoita haikupokelewa.

Simu ya Benedict ilipokewa na mtu aliyedai imeachwa kwenye chaji, na hata baada ya kuelezwa sababu ya kutafutwa kwake, mtuhumiwa huyo hakujitokeza kujibu tuhuma dhidi yake.

Akizungumzia chanzo cha mkakati wa DC huyo, Rose alisema zilianza vurugu baada ya kifo cha baba yao mzazi, Paul Henjewele, mwaka 2002 na kuwaachia shamba lenye ukubwa wa ekari sita, katika enero la Mbezi Luisi.

Alidai DC Henjewele akishirikiana na ndugu zao wawili, alimrubuni mama yao na kuruhusu shamba hilo kuuzwa kwa kanisa kwa Sh. 12 milioni na kutokomea nazo peke yake.

Kutokana na kitendo hicho, vijana hao waliamua kumfungulia mashtaka, lakini baadaye mama yao aliwashauri wafute kesi kwa kuhofia mwanawe wa pili, John, kupoteza ukuu wa wilaya.

“Mama alitushauri tuachane na kesi, akaahidi kuuza nyumba yake ya Kinondoni na kutugawia kila mtu fungu lake. Aliuza nyumba kwa sh 50 milioni na kutugawia,” alisema.

Kutokana na mgawo huo, vijana wawili, Francis na Stephen walinunua nyumba yao Kinondoni Moscow, na mabinti wanne walinunua ya kwao Salasala kwa Sh. 25 milioni, ambayo sasa ndiyo anadai kaka yao ‘anamezea mate.’

Mabinti walionunua nyumba hiyo na kukaa na mama yao ni Rose, Margareth, Gloria na Sofia, ambaye sasa ni marehemu. Gloria ambaye hivi sasa anadaiwa kushirikiana na kaka zake katika mpango wa kuuza nyumba, amekamatwa na polisi katika kesi hiyo ya shambulio la kudhuru mwili.

Rose ambaye ni kitinda mimba katika familia hiyo, alidai DC huyo alianza fujo zake kwa kuchukua hati za nyumba hiyo yenye majina ya mabinti hao na kutaka kubadili umiliki, lakini akakwama.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)