Demokrasia ya kweli na hofu ya mabadiliko


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 03 June 2008

Printer-friendly version

KAMA wafanyabiashara katika soko huria wanashindwa kuelewa taifa moja linaweza kuneemeka kwa gharama ya taifa jingine, hatushangai kuona tabaka moja nchini linavyoweza kujineemesha kwa gharama ya wananchi.

Haya ni maneno au msimamo wa mwanafalsafa wa Kirusi, Karl Marx aliyeishi katika karne nyingi zilizopita.

Nchini Tanzania pamejengeka matabaka – likiwepo la wenye fedha na wasionazo. Ni vigumu kwa maskini kushika nafasi ya uongozi, licha ya milango ya mabadiliko kufunguliwa.

Mwalimu Julius Nyerere, 2 Oktoba 1969 kwenye Chuo Kikuu cha Toronto, Canada alipotoa mada ya "Utulivu na Mabadiliko barani Afrika" alisema:

"Ingawa utulivu wa kisiasa na kijamii ni muhimu kwa uhuru wa kweli wa taifa na watu binafsi, ndivyo ilivyo muhimu kuwapo mabadiliko katika hali yetu ya sasa."

Wanafalsafa wanaamini "mabadiliko hayaepukiki." Maendeleo katika jamii yoyote ile, huchochewa na mabadiliko.

Mwalimu alikuwa kiongozi si mtawala.

Licha ya uzoefu wa miaka 16 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, bado baadhi ya viongozi wanahofia mabadiliko.

Pakidaiwa katiba mpya na marekebisho ya sheria za uchaguzi, wanakasirika licha ya kujua tupo katika mfumo wa siasa za ushindani.

Wao wanaamini ni haki mfumo huo uongozwe na Katiba na sheria zilezile zilizokuwepo kabla ya 1993. Wanataka kulinda himaya zao.

Bila ya shaka walichukia Mwalimu Nyerere aliporuhusu mjadala wa vyama vingi wakati anaachia ngazi kama kiongozi wa taifa.

Katika nchi zilizokomaa kidemokrasia, kushindwa kwa muswada wa serikali kunatosha kuiondoa madarakani. Basi serikali huwa macho inapoandaa muswada kwa kupima kwanza nini kinaweza kutokea ukifikishwa bungeni.

Wataalamu hupewa kazi ya kuchunguza athari zinazoweza kutokea muswada huo ukipelekwa kujadiliwa.

Hutafuta hakika iwapo wananchi bado wataiona serikali ni ya watu, badala ya watu kuwa wa serikali; na kwa serikali kuwajibika kwa watu, badala ya watu kuwajibika kwa serikali.

Hii ndiyo tafsiri sahihi ya "demokrasia" kwa mujibu wa waasisi wake, Wayunani wa kale. Tunakwenda kinyume.

Chini ya Ibara 63(1), Rais ni sehemu ya Bunge. Muswada ukipita unahitaji ridhaa yake kuwa sheria (Ibara 97(2)) na kwamba Bunge likikataa muswada wa serikali anaoutaka Rais, aweza kulivunja ili uje uchaguzi mpya (Ibara 97(4).

Kinachoonekana hapa si nguvu ya demokrasia ya uwakilishi bali ni ubabe na mapambano kati ya wananchi (Bunge) na utawala (Rais) ambayo yanachochea kuiua demokrasia.

Rais anapohutubia Bunge au kupeleka taarifa ikasomwa bungeni na Waziri Mkuu (Ibara 91), huwa anaelekeza Bunge cha kufanya. Maana yake Rais ni mhimili wa Bunge.

Na kwa uwezo aliopewa wa kutenda baadhi ya kazi za Bunge (kutunga sheria, kulielekeza), ni wazi Rais ndiye Bunge na Bunge ndiye Rais. Hapa, demokrasia ya uwakilishi inauawa.

Kama utungaji sheria ni kazi mojawapo kuu ya Bunge, iweje asipewe Spika mamlaka ya kusaini sheria iliyotungwa na Bunge?

Kama ambavyo mawakili watetezi hawawekewi mipaka wanapotetea wateja wao mahakamani, ila tu kwa misingi ya sheria, isingekuwepo sababu ya kufungia hoja za wabunge kwenye sanduku la Kamati; vinginevyo zipewe madaraka zaidi, si ya kupitia tu mapendekezo ya serikali na kushauri, bali pia kuwasilisha maoni yake kupitia miswada ya sheria Bungeni.

Ipo changamoto nchini petu: kujenga demokrasia na heshima kwa haki za raia, ndani ya hali ya hofu inayokabili tabaka la viongozi na wafanyabiashara wanaoogopa mabadiliko.

Tofauti na enzi za itikadi ya Ujamaa iliyounganisha Watanzania kama ndugu, changamoto ya leo ni kuunganisha jamii inayogawanyika na kupindishwa kwa haki za msingi na tabaka la wachache.

Watu wataendelea kudai haki za kikatiba kwenye Mahakama bila ya kuogopa kama wanatangaza vita na watawala wanaojitahidi kutumia ujanja kupuuza maamuzi ya mahakama.

Wanakumbuka sheria ya takrima ilivyogeuzwa badala ya kutambuliwa kuwa ni rushwa. Wameona namna uamuzi wa kuridhia mgombea binafsi ulivyopingwa na watawala mpaka Mahakama ya Rufaa. Wameona pia makali ya dhamana ya Sh. 5 milioni kwa anayetaka kupinga matokeo ya uchaguzi.

Katiba, katika Ibara ya 125, inatamka kuwepo Mahakama ya Katiba kwa ajili ya kutanzua migogoro ya kikatiba. Ni mahakama hii ingesikiliza malalamiko ya kupindwa kwa mkataba wa Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika.

Haijawahi kuundwa wala watawala hawaoni haja yake, licha ya kuwepo kero nyingi za Muungano.

Rais Aboud Jumbe Mwinyi wa Zanzibar, alilazimishwa kujiuzulu nyadhifa zote za Chama na Serikali, kwa sababu tu mwaka 1984, alitaka mahakama hiyo iitwe ili kutoa msimamo juu ya mfumo wa Muungano uliopo.

Umadhubuti wa mahakama zetu ni changamoto nyingine katika kujenga demokrasia ndani ya watawala wenye hofu ya mabadiliko.

Tupendekeze Katiba ianzishe Mahakama ya Katiba ya kweli (si Mahakama pambo) ambayo, mbali na kushughulikia migogoro ya Muungano, idhibiti pia ukiukaji wa Katiba unaofanywa na watawala, mtu binafsi, taasisi za umma na Serikali yenyewe.

Kazi ya Mahakama ya Katiba iwe ni pamoja na kutafsiri, kulinda na kushinikiza utekelezaji na kuzingatiwa kwa matakwa ya Katiba na kila mtu bila ya upendeleo.

Madhumuni ya mfumo wowote wa uchaguzi ni kutoa haki ya mtu kupiga kura kwa uhuru. Uchaguzi huru na wa haki ni ule uliompa kila raia haki ya kuchagua atakacho na maamuzi ya wengi yakaheshimiwa na wote.

Katiba yetu inaridhia haya lakini tatizo ni watawala wanaohofia mabadiliko. Wanatumia vibaya madaraka kupindisha maamuzi ya wengi.

Kuzuia wagombea binafsi ni kunyima wananchi uhuru na haki ya kuchagua mtu wamtakaye au wenye imani naye. Cha muhimu si chama, bali mtu mwenye uwezo kuwaongoza.

Kuondolewa kwa "uchama" katika kugombea, kutatoa fursa kwa raia wasiopendelea kuwakilisha chama katika kugombea uongozi.

Hata wale waliozuiwa kisheria kushabikia vyama, mfano maafisa Mahakama (Ibara 113A) na maafisa wa Serikali (Waraka wa Serikali Na. 1 wa Juni 2000) wataingia.

Tume za uchaguzi zilizoanzishwa chini ya Ibara ya 74 (Katiba ya Muungano) na Ibara ya 118 (Katiba ya Zanzibar) zipate wajumbe adilifu ambao, wakikiuka sheria, wanabanwa.

Hatuoni sababu kwa nini viongozi wa Tume waendelee kuwajibika kwa Rais ambaye naye huwa ni mgombea uchaguzi. Basi mahakama zingepewa mamlaka ya kuthibitisha matokeo ya uchaguzi.

Tume zimekuwa zikiyumba mara zote na zimekuwa chanzo cha vurugu na migogoro isiyokwisha, mfano mzuri visiwani Zanzibar.

Yote haya ni matokeo ya hofu ya mabadiliko kwa watawala. Kwa nini hofu ya tabaka la wachache iruhusiwe kuangamiza haki na uhuru wa wengi?

0
No votes yet