Demokrasia ya vitisho, wizi wa kura


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version

MTU yeyote anayejitokeza kuwa kiongozi au mfuasi wa chama cha upinzani Tanzania ni lazima ajiandae kupata changamoto nyingi kama kutengwa na kuchafuliwa.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachotawala kitatumia dola, hila na wakati mwingine nguvu kuzima upinzani na kuwadhoofisha viongozi wake. Na hii ndiyo sababu ya wapinzani kupigwa mabomu, mikutano yao kuzuiwa na kuambiwa wazushi. Hiyo ndiyo gharama ya kuwa mpinzani.

Historia inaonyesha kwamba waliojitokeza kuendesha siasa zenye changamoto kwa chama tawala kuanzia enzi za Tanganyika African National Union (TANU) mwaka 1958 hadi kilipoasisiwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wapinzani walidhalilishwa na kushughulikiwa kwa nguvu.

Zuberi Mtemvu, Abdallah Fundikira, Oscar Kambona ni baadhi tu ya wanasiasa walioshughulikiwa hadi ama wakarudi Tanu au kwenda uhamishoni.

Hao walishughulikiwa kwa kuanzisha vyama au kuwa na fikra pinzani na Mwalimu Julius Nyerere. Mtemvu alikuwa mtu wa kwanza ndani ya Tanu kuhitilafiana na Nyerere kuhusu kura tatu katika uchaguzi mkuu enzi za ukoloni.

Baada ya kuona mawazo yake hayaheshimiwi, Mtemvu alijitoa na kuanzisha African National Congress (ANC) lakini alibanwa, akafitinishwa, akadhoofishwa na chama kikakosa nguvu. Baada ya kuangushwa vibaya katika uchaguzi mkuu, aliamua kurudi Tanu.

Kassanga Tumbo pia alihitilafiana na Mwalimu Nyerere akaamua kuanzisha chama cha Tanganyika Democratic Party lakini hata kabla hakijajikita sawia, kikanyongwa kwa hila.

Chama hicho kilikufa rasmi baada ya Mwalimu Nyerere kufuta mfumo wa vyama vingi na kuacha Tanu kuwa chama pekee. Uamuzi huo uliwaaudhi mawaziri kadhaa akiwemo Abdlaah Fundikira aliyeamua kujitoa.

Miaka miwili baadaye, baada ya kuanzishwa Azimio la Arusha, Kambona alipinga waziwazi na kwa hofu ya ‘kupotezwa’ alikimbilia uhamishoni Uingereza.

Mateke

Hakika shukrani za punda ni mateke. Kambona ndiye aliyefanya juhudi kipekee kuwashawishi askari walioasi Januari 1964 waweke silaha chini wakati Nyerere na Makamu wa Rais, Rashid Mfaume Kawawa walipokuwa wamehifadhiwa sehemu ya usalama.

Baada ya uasi huo kuzimwa kwa msaada wa majeshi ya Uingereza, Nyerere alimshukuru Kambona kwa  kazi ya kuzima hatari. Lakini baada ya kuanzisha Azimio la Arusha bila kufanya majaribio kwanza, alihitilafiana na rafiki yake huyo aliyemwokoa mwaka 1964.

Kwa hiyo, waliojitokeza na mawazo tofauti, walibinywa kimya kimya. Hata uliporejeshwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, bado hakukuwa na uwanja sawa wa uchaguzi.

Mabomu

Serikali ya CCM imekuwa ikihakikisha kwamba chama hicho hakitolewi madarakani hivyo imekuwa ikifanya ushawishi na kutumia nguvu kudhibiti upinzani.

Augustine Mrema alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, alitishia kumtia ndani Kambona aliyeamua kurudi nchini baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi akidai ni raia wa Malawi. Hata hivyo alishindwa.

Lakini Mrema alipohamia upinzani akateuliwa kuwania urais kupitia chama cha NCCR-Mageuzi mwaka 1995 alionja ukatili wa serikali ya CCM kwani alipigwa mabamu, mikutano yake ilizuiwa kwa madai hakupewa kibali na hila mbalimbali.

Katika uchaguzi ule, Mrema ndiye alionekana tishio hivyo ukatili wote wa serikali ulilenga kuzima uwezo, ushawishi na fursa zake kumwaga sera kwa wananchi.

Ukatili huo wa serikali ya CCM ulijitokeza tena mwaka 2000 dhidi ya wagombea wenye nguvu—Mrema akiwa kwenye chama kipya cha Tanzania Labour Party na Prof. Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF).

Mwaka huu, chama kilichokumbana na mkono mbaya wa serikali ya CCM ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho mgombea wake, Dk. Willibrod Slaa alizuiwa kufanya mikutano na alipigwa mabomu.

CCM inaposhindwa inatumia vitisho, polisi, majeshi kuzima wapinzani na upande wa pili inatumia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwanasheria mkuu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo inapika matokeo.

Siku chache kabla ya kuanza kampeni za “uchafuzi” mkuu, NEC ilidai kwamba imerekebisha Daftari la Kudumu kwa Wapigakura kwa kuondoa majina yakiwemo ya waliokufa.

Ilidai awali kulikuwa na wapigakura zaidi ya 21milioni lakini wamebaki 19.6milioni. Oktoba 5, 2010 wakati wa kumtangaza mshindi, NEC ilishtua watu kwa kusema waliojiandikisha walikuwa 20,137,303.

Uko wapi umakini wa NEC katika taarifa zake? Halafu idadi ya wapigakura ni chini ya kura alizopata Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005. Mwaka huo alipata kura 9,123,952 sawa na asilimia 80.28 lakini safari hii wapigakura walikuwa 8,626,283 asilimia 42.8 ya waliojiandikisha.

Uzushi

Kambona alipokimbia nchi, huku nyuma alizushiwa kwamba amekwapua mamilioni ya shilingi, lakini wale waliomwona Uingereza, walisema alikuwa anaishi maisha ya dhiki.

Baada ya serikali kwanza kurejesha mfumo wa vyama vingi na pili kufuta Azimio la Arusha mambo mawili yaliyosababisha aondoke nchini, Kambona alirudi na alipokewa na umati mkubwa wa watu ambao walikuwa na shauku ya kumjua.

Huku akikumbuka alivyozushiwa mwaka 1967 akasema atataja akaunti za fedha za kigeni za Mwalimu Nyerere. Aliposhindwa kufanya hivyo katika mikutano yake akawa amejimaliza kisisa na chama chake cha Tanzania Democratic Alliance (Tadea), hakikuwa na nguvu.

Mrema pia alipohamia upinzani alizushiwa kwamba aliondoka na mamilioni ya shilingi, lakini serikali hiyo iliyozusha haikumkamata.

Ndiyo maana katika uchaguzi mkuu mwaka huu CCM ilikuja na uzushi wa udini, ukabila, vyama vingi ni vita, vyama vingi havina uongozi wa kuaminika, wapinzani ni majuha na matusi. Hiyo ndiyo demokrasia chini ya CCM.

Kikwete

Kazi nzuri iliyofanywa na vyombo vya habari kutoa elimu ya uraia kwa wapigakura iligeuzwa kwa makusudi na CCM kwamba ni uchochezi.

Serikali ya CCM ikashupalia, ikatishia kuchukua hatua dhidi ya asasi za kiraia na MwanaHALISI vilivyojaribu kukemea uchafuzi huo katika uchaguzi mkuu.

Lakini Oktoba 5, baada ya NEC kumtangaza kuwa rais baada ya kujikusanyia kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17 Kikwete alibadilika na kuviomba vyombo vya habari visaidie katika kampeni za kuponyesha majeraha yaliyotokana na uchaguzi mkuu. Baada ya kuapishwa Jumamosi akasema “yaliyopita si ndwele tungange yajayo”.

Sawa, lakini hivi Kikwete hakuwa anajua madhara ya kuwaita wapinzani kuwa majuha wa siasa au katibu mkuu, Yussuf Makamba hakuwa anajua madhara ya kuwaita wapinzani wahuni?

Hivi hawakuwa wanajua madhara ya kupiga mabomu ya machozi dhidi ya wafuasi wa vyama vya upinzani? Ni kweli kwamba CCM hawakuwa wanajua wanajenga ufa kwa kubambikia udini, ukabila kwa wapinzani wakati chimbuko liko ndani ya CCM?

Kwa nini Kikwete, Makamba na msomi wa kiwango cha juu, Dk. Gharib Bilal waendeleze kampeni chafu dhidi ya wapinzani kama walikuwa wanajua “wanajenga nyumba moja hivyo wasigombanie fito?”

Hivi ni haki kumwibia mtu kura halafu kesi imalizike kwa kusema yaliyopita si ndwele? Je, hiyo inafuta ukweli kwamba Kikwete anaongoza wana CCM na majuha wa kisiasa?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: