Dhahabu inapokuwa Karaha, Balaa na Matanga


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 16 March 2011

Printer-friendly version
Hatujui faida ya dhahabu Tulawaka

WAKAZI wa kijiji cha Mavota, ambacho sehemu yake ni machimbo ya dhahabu ya Tulawaka, hawajui faida ya dhahabu inayozalishwa kijijini mwao.

Kijiji cha Mavota kipo kata ya Kaniha, tarafa ya Lusahunga wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

Wakazi wa kijiji hicho wamepanga kuandamana, mwisho wa mwezi huu, kwenda kwenye mgodi wa dhahabu wa Tulawaka, kuonana na meneja utawala wa mgodi huo, kupata ufafanuzi juu ya utekelezaji wa huduma za jamii walizoahidiwa.

“Kuna ahadi nyingi tulizopewa na viongozi wa mgodi; bado hazijatekelezwa. Sasa sisi tutakwenda kumuona meneja, kujua kama bado wana lengo la kutekeleza ahadi yoyote,” ameeleza mzee Josephat Mwombeki.

Mwombeki (56) anasema wameshataarifu uongozi wa kijiji kuhusu nia yao ya kuandamana na lengo la maandamano yao.

Mtendaji wa kijiji cha Mavota, Ferdinand Manumba anasema amepokea taarifa za wanakijiji hao kutaka kuandamana na kuongeza, “Hatuna sababu ya kuzuia maandamano yao kwa kuwa madai yao ni ya msingi.”

Anataja orodha ya madai tisa ya wananchi wanayotaka kupeleka kwa uongozi wa mgodi ili kupata ufafanuzi.

Kwanza, wanataka kujua kama mgodi una bajeti yoyote unayotenga kwa mwaka kwa ajili ya huduma za jamii katika kijiji hicho. Hivi sasa hakuna huduma wanazotoa.

Pili, wanataka kufahamu iwapo ujenzi wa barabara kutoka kijijini Mavota hadi Mbaba, ambayo mgodi uliahidi kujenga miaka minne iliyopita itaanza lini kujengwa.

Tatu, wanataka kujua hatma ya mabwawa ya kunyweshea mifugo na kumwagilia bustani za mboga ambayo waliahidiwa. 

Nne, wanataka kujua mpango wa ujenzi wa nyumba tano (5) za walimu walioahidiwa utatekelezwa lini.

Tano, lini ahadi ya ujenzi wa maabara itaanza kutekelezwa.

Sita, lini ahadi ya kupatia zahanati ya Mavota gari la wagonjwa itatekelezwa.

Saba, kulalamikia malipo kiduchu ya shilingi elfu tatu (3,000) kwa siku ambazo wanalipwa vibarua wanaotoka kijijini humo.

Nane, hatua iliyofikiwa ya maombi ya kuchimbiwa visima vya maji kwa kila kitongoji?

Tisa, utekelezaji wa ombi la kugharimia wanafunzi wanaoshi katika mazingira magumu. 

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Daudi Donasian anasema ahadi nyingi zilizotolewa na uongozi wa mgodi hazijatekelezwa.

Akiongea mbele ya mtendaji wa kijiji hicho na wenyeviti watatu wa vitongozi vya kijiji chake, Daudi anasema kijiji chake hakioni faida ya mgodi wa dhahabu kuwa katika eneo lake.

“Hebu fikiri ndugu mwandishi, mgodi umo katika vijiji vya Mavota na Mkukwa. Vijiji vyote hivi vinatumia zahanati moja na shule moja ya msingi. Zahanati ina mganga mmoja na manesi wawili tu. Sasa dhahabu ina faida gani kwetu?” anauliza Daudi.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mavota, Lucas Chakupewa akimuunga mkono mwenyekiti wake anasema, “tena zahanati yenyewe haina hata mafuta ya taa, mgonjwa akienda katika zahanati hiyo wakati wa usiku anatakiwa kwenda na taa, tochi na maji.”

“Huwezi kuamini kama zahanati ipo kilometa tano kutoka mgodini ambako maji yanamwagika na umeme unawaka saa 24. Angalau basi wangefanya utu; wakatuwashia wakati wa usiku tu,” anaeleza Chakupewa.

Mgonjwa akizidiwa katika zahanati ya Mavota anapelekwa hospitali ya wilaya Biharamulo ambako kuna umbali wa zaidi ya kilometa 90.

Kijiji cha Mavota kina wakazi 4,433, wakiwa wanaume 2,014 na wanawake 2,419, ambao wamegawanyika katika vitongoji sita vya Mavota, Mlinda, Karamata, Kabingo, Katoma na Ilelema.

Kijiji hiki kina wageni wengi kuliko wakazi kutokana na shughuli za uchimbaji madini na wote wanahudumiwa katika zahanati moja yenye mganga mmoja na nesi wawili.

Mgodi wa Tulawaka umo ndani ya hifadhi ya taifa katika wilaya ya Biharamulo, kaskazini mwa kijiji cha Mavota.

“Ingawa mgodi umejenga vyumba sita vya madarasa katika shule ya msingi Mavota, lakini shule haina madawati na watoto wengi wanakaa chini,” anaeleza mtendaji wa kijiji, Ferdinand Manumba.

Manumba anasema pia mgodi umechimba visima viwili katika kijiji chake na umejenga zahanati na nyumba moja ya mganga, lakini wagonjwa wanatibiwa kwa ‘ramli’ kwa kuwa zahanati haina uwezo wa kupima hata malaria.

Kijiji kizima cha Mavota ambacho kimejaliwa madini ya dhahabu na watu zaidi ya 4,400, kina visima viwili (2) tu vinavyotumiwa na wanakijiji kwa ajili ya maji ya kunywa.

Inalazimu asilimia themanini (80%) ya wanakijiji kutembea hadi kilometa tano kufuata maji.

Mwenyekiti analalamikia pia ajira kwa vijana wa kijiji chake. Anasema vijana wa kijiji hicho kilichopo kwenye mgodi hawapati ajira ya kudumu katika mgodi.

Anasema wafanyakazi karibu wote walioajiriwa katika mgodi wa Tulawaka ni kutoka nje ya kijiji hicho. Utawala wa mgodi unasema matangazo ya ajira hutolewa kwenye intaneti, wakati kijiji hakina hata umeme wala kompyuta.

Afisa uhusiano wa mgodi, Bahati Mwambene anakana baadhi ya tuhuma za viongozi wa vijiji. Kwa mfano anasema matangazo ya kazi huwekwa pia magazetini na kwenye ubao kijini.

Mwambene anasema wanatoa ajira za kufyeka nyasi na ulinzi kwa vijana, “tunalipa kodi zote za serikali; sasa tuwasaidieje?”

Lakini mwenyekiti wa kijiji anasema hizo ajira ndizo hasa wanalalamikia. Anasema kazi za kufyeka na ulinzi wa sungusungu sio ajira za kudumu, bali ni kazi wanazopokezana vijana wa vijiji viwili.

Mfanyakazi mgodini ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, anadai kuwa ajira hutolewa kwa upendeleo. “Hata kama kazi ni ndogo, utaona mtu anaitwa kutoka Dar es Salaam na anaanza kazi,” anaeleza.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kambingo kilichopo katika kijiji cha Mavota, Josephat Masapala anasema, wamepeleka matatizo na malalamiko yote ya wananchi kuhusu mgodi huo kwa viongozi wa wilaya lakini hakuna mabadiliko.

Anasema hata viongozi wa wilaya, mkoa na taifa wanapokwenda mgodini hawafiki kwa wananchi kusikiliza matatizo yao. 

“Huku hakuna waandishi, wachache wanaokuja wamebebana na viongozi; wakitoka mgodini wanatoka nao. Kesho yake unaweza kuwasikia wanatangaza  habari za uongo za kijiji hiki na wananchi wake hata bila kuwasikiliza. Hajawahi kutokea mwandishi akafika kijijini tukakaa naye kama wewe ulivyofika,” anasema Masapala.

Watoto wa kijiji hiki na vijiji vya jirani wanatembea kati ya kilometa 16 na 28 kufuata shule ya sekondari ya Kata.

Diwani wa kata ya Kaniha, Edward Mashauri (CCM) anasema katika miaka mitano, mgodi umejenga madarasa matatu tu katika shule ya kata, wakati kata hii ilipaswa kung’ara kwa maendeleo.

Mashauri anasema hata mishahara ya wafanyakazi ambayo ingesaidia kuongeza mzunguko wa fedha katika vijiji, imebanwa kwani wafanyakazi wanazuiwa mgodini.

“Humu kaka ni kama jela; mfanyakazi haruhusiwi kutoka nje ya geti la mgodi kwa muda wa miezi miwili, baada ya hapo anapewa likizo ya mwezi mmoja. Ni utumwa mtupu humu ndani,” ameeleza mfayakazi.

Afisa uhusiano wa mgodi, Mwambene amethibitisha madai hayo. “Ni kweli wafanyakazi wanaishi humu na mimi nikiwepo, lakini tunataka kubadilisha utaratibu ili wafanyakazi wakae wiki nne ndani ya mgodi kisha wapewe likizo ya wiki mbili.”

0
No votes yet