Dhahabu: Utajiri katikati ya umasikini


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 17 March 2010

Printer-friendly version
Gumzo

KILOMETA nne kutoka geti la mgodi wa dhahabu wa Geita – Geita Gold Mine (GGM), kuna wananchi wanaoishi katika mahema.

Hii ni kambi ya Watanzania walioswagwa kutoka kijiji cha Nyamalembo, kitongoji cha Mine Mpya ili kupisha uchimbaji madini.
Wananchi hawa wanakumbuka kilichotokea 31 Julai 2007. Ulikuwa usiku wa saa tisa. Polisi wenye silaha, baadhi ya watu walioitwa maofisa wa GGM na vijana kadhaa wa mitaani, walivamia Mine Mpya.
“Tuliwaambia muhame; ninyi mmekaidi. Sasa mtaondolewa kwa nguvu,” amesimulia katibu wa waathirika, Jonaa Saidi akikariri kauli za msemaji wa polisi usiku huo.
Kilichotokea kinaelezwa vema katika barua ya wananchi wa Mine Mpya kwa Jaji Mkuu wa Tanzania ya 20 Aprili 2008:
“…tulivamiwa saa 9 usiku huku nyumba zetu zikichomwa moto, mashamba na vitu vyote vikiparuriwa na katapila za mgodi; kampuni (GGM) ilitupeleka na kutuweka katika jengo la serikali lililokuwa likitumika hapo awali kama mahakama ya wakoloni…” inaeleza barua.
Wananchi kutoka familia 86 hawakuenea katika jengo hilo. Wengi walibaki nje, tena kwa muda mrefu. Ni baadaye mwaka 2008, Kanisa la African Inland (AIC) liliwafadhili mahema.
“Tupo hapa. Tunaishi kama wakimbizi. Huwezi kuamini kuwa tulikuwa na majumba yetu, mashamba yetu, mali zetu, hadhi zetu, ah…..” anasimulia Bi. Mwajuma Hussein ambaye anavuta kanga yake haraka na kuanza kufuta machozi yaliyoanza kuchuruzikia mashavuni.
Ni miaka mitatu sasa tangu Bibi Mwajuma (75) na wenzake watupwe hapa. Kwa kadri anavyopata taabu kuelezea yaliyomsibu, unadiriki kufikiri kuwa anakandamizwa na tani nyingi za majonzi, zilizobebana na chuki na hasira dhidi ya aliyewaondolea maisha yao ya awali.
Kuna taarifa kwamba mwaka 2003, serikali ikishirikiana na uongozi wa mgodi wa GGM, walifanya tathmini kwenye mashamba na nyumba katika kitongoji cha Mine Mpya kwa nia ya kufidia wananchi ambao wangehamishwa kutoka eneo hilo.
Lakini hakuna aliyewalipa mpaka walipovamiwa usiku wa 31 Julai 2007, tena bila taarifa, na kuondolewa makazini mwao.
“Hapo ndipo nilipoona jeuri ya fedha na kuamini usemi wa ‘masikini hana haki, kwani kitendo cha kutuondoa kwetu kilifanyika wakati tunasubiri uamuzi wa mahakama ya rufaa,’ ” anaeleza Jonaa Saidi, katibu wa waathirika.
Wakazi wa mahemani wanaeleza kuwa wanapomfuata mkuu wa wilaya (DC), Philemon Shelutete, anawajibu hana cha kuwasaidia kwa sababu kesi iko mahakamani.
“Tunamshangaa DC anaposema hawezi kusaidia chochote kwa sababu kesi yetu bado iko mahakamani. Lakini ni yeye aliyewaachia GGM, wakitumia polisi wake, kutuondoa huku akijua kuwa kesi iko mahakani,” anasema Jonaa.
“Huwezi kuamini kama upo katika nchi huru. Hata haya mahema tumepewa msaada na AIC,” anasema Bartazal Emmanuel, mwenyekiti wa kaya 86 za waathirika.
Hata hivyo, haya yamebaki makazi ya wazee na watoto wadogo chini ya miaka10. Vijana wa umri wa kati na mkubwa, wameshindwa kustahimili kile wanachoeleza kuwa “manyanyaso tuliyoletewa na serikali na GGM.”
“Watoto wetu wengi hawajulikani walipo. Hatujui kama wapo hai, ukiachilia mbali wachache waliokimbilia kwa ndugu zetu,” anaeleza Bi. Immaculata Joseph mwenye umri wa miaka 61.
Katika barua yao kwa jaji mkuu, wakihimiza kesi yao isikilizwe haraka, na hata kabla ya kufadhiliwa mahema, waathirika wanalalamika, “Mheshimiwa Jaji Mkuu, kutokana na kulala kwetu nje… tunakuomba utuonee huruma shauri letu lisikilizwe ili tujue hatima yetu.”
“…Tunateseka sana, tunakosa chakula kwa kuwa hatujalima… Pia baadhi ya wenzetu wamekufa kutokana na njaa na baridi kali,” inaeleza barua kwa jaji mkuu.
Aidha, taarifa zimeenea hapa kuwa GGM iliishatoa fedha za fidia kwa waathirika lakini “zimeliwa na watumishi wa serikali.”
Angalau mfanyakazi mmoja ndani ya mgodi anasema fidia kwa waathirika iilishatolewa, bali fedha hizo “zimeliwa.”
Katibu tawala wa wilaya Geita, Marco Bakebula alikataa kuzungumzia mgogoro huo kwa madai kuwa bado uko mahakamani.
Alipobanwa kueleza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ambaye hakuwepo ofisini na alisemekana kuwa Dar es Salaam kikazi, juu ya lini wananchi watalipwa haki zao,
alisema, “Wale wananchi walikuwa wavamizi, halikuwa eneo lao.”
Alipoombwa kufafanua kwa nini serikali inasema wananchi ni wavamizi na wakati huohuo inapima maeneo yao kwa ajili ya kufanya tathimini ya kuwalipa fidia, Bakebula aligeuza kibao.
“Nimeshakwambia siwezi kulizungumzia suala hilo kwa undani kwa kuwa bado liko mahakamani; wewe subiri maamuzi ya mahakama.” Ndimi mbili.
Madai hayo yanapingwa na diwani wa kata ya Mtakuja, Suzana Mashala (CCM), ambaye anatajwa na wananchi wa Geita kuwa mtetezi wao pekee miongoni mwa viongozi.
Suzana anasema wale ni wakazi halisi waliokuwa wanamiliki maeneo yao kihalali. “Kitongoji cha Mine Mpya walichotolewa kipo ndani ya kata yangu, nami najua kuwa wao ndio waliokuwa na mashamba kihalali,” anasisitiza Suzana.
“Mimi mwenywe nimefika mpaka Dodoma kumuona waziri wa nishati na madini Ngeleja (William) kushughulikia suala hili. Na aliniahidi kushughulikia haraka malipo ya wananchi,” Suzana anaeleza kwa uhakika.
Anasema pamoja na Ngeleja kumuahidi kushughulikia malipo, pia alimwambia wanafanya mazungumzo na uongozi wa GGM ili uwajengee nyumba wale waathirika wa Mine Mpya waliotolewa kwenye kata yake.
“Sasa kama serikali haiwatambui, kwanini waziri anidangaye?” anauliza Suzana.
Afisa uhusiano wa GGM, Clement Msalangi alikataa kumruhusu mwandishi kuingia kwenye aneo la mgodi. Pia alikataa kujibu maswali ya mwandishi kwa madai ya kutokuwa msemaji wa kampuni.
Alipotumiwa ujumbe wa simu ili atoe ufafanuzi wa barua mbili zenye saini zake tofauti, ndipo alipopiga simu na kujibu baadhi ya maswali.
Kuhusu wanaokaa katika mahema, Msalangi alisema wamejitakia wenyewe na yeye haoni tatizo.
"Sikiliza bwana, Watanzania wana maisha tofauti. Wengine wanaishi kwenye majumba ya kifahari na wengine wanaishi kwenye vibanda na wapo wanaoishi maisha ya kubahatisha na wengine mabaya zaidi ya wale unaowasema,” alieleza Msalangi.
Alisema wale wanaoishi katika mahema wameamua wenyewe kwenda kuishi pale, hivyo haoni tatizo. “Waache waendelee kuishi. Maisha popote,” aliongeza Msalangi ambaye mshahara wake GGM uko kwenye skeli ya Level I (kuanzia Sh. 5 milioni kwa mwezi).
Alipobanwa kueleza wamependa vipi kuishi mahemani wakati mgodi ndio uliowaondoa kwenye maeneo yao, alisema asingeweza kuingia undani wa suala hilo kwa kuwa liko mahakamani.
Malalamiko dhidi ya GGM yameenea katika vijiji vya Kalangalala, Nyakabale, Nyamalembo, Mgusu, Salagulwa na Mpovu vilivyoko karibu na mgodi huu unaoendeshwa na kampuni ya AngloGold Ashanti ya Afrika Kusini.
Kwa mfano, mwaka 2006 wananchi 576 wa kitongoji cha Katoma, kijiji cha Kalangalala walitakiwa waondoke ili kupisha shughuli za mgodi.
Taarifa za wanakijiji zinasema kaimu mkuu wa wilaya (DC) wakati huo, Esther Marieta, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Sengerema alitumia vitisho kutathmini ardhi na mali za wananchi na kuagiza wananchi wakubali “malipo yoyote watakayolipwa na mgodi.”
Hata hivyo, wakazi 23 walikwenda mahakamani kumshitaki. Miongoni mwa waliothaminiwa kwa vitisho, kuna aliyelipwa kwa hundi Sh. 13,000. Diwani wao, Saidi Mahuma anasema “hawakutendewa haki.”
Lakini wengine hawakulipwa chochote. Jackson Manyero, mwenye eneo la eka mbili za migomba, mibuni, miembe, michungwa na milimau, anatoa ushahidi.
“Tulipomuuliza Afisa Uhusiano msaidizi wa GGM, Simon Shayo kwa nini hawalipwi, alijibu kuwa hakuna tunachokidai kwa kuwa hakuna mali yoyote ya mwananchi iliyoharibiwa na mgodi,” anaeleza Manyero.
Wakati huo wananchi waliishaondoka na kupisha mgodi. Bali pamoja na GGM kugoma kulipa, wakidai malipo kwa walalamikaji 23 yalikuwa makubwa kuliko waliyofanya kwa wakazi 253 mwaka 2006, wenye maeneo hawajui hata wanachopaswa kulipwa.
Hii inatokana na serikali, iliyofanya tathmini kwa kushirikiana na GGM, kukataa kuwashirikisha wananchi katika zoezi hilo na kukataa pia kuwaambia thamani halisi ya maeneo na mali zao.
Hata hivyo, Saidi Mahuma, mwenyekiti halmashauri ya mji mdogo wa Geita anasema GGM inadai kuwa mwaka 2006 ililipa fidia ya Sh. 1 bilioni kwa wakazi 553 lakini hivi sasa wadai 23 wanataka Sh. 3 bilioni.
“Kwa vyovyote vile, wananchi wanapaswa kulipwa kwa sababu mazao yapo ndani ya mashamba yao na sheria inawalinda,” anasema Mahuma.
Walioondolewa kwenye makazi yao ni wengi. Wale ambao mali zao zilithaminiwa lakini hawakulipwa ni wengi. Ambao mali zao zilithaminiwa lakini wakalipwa kiduchu, ni wengi.
Mahuma anakadiria zaidi ya wananchi 2,000 katika eneo hilo wana mgogoro na GGM.
Kwa mfano, wakazi wa kijiji cha Nyamalembo wangali na mgogoro. Aliyekuwa DC mwaka 2006, Albert Mnali anadaiwa kuwaambia kuwa malipo yao hayajawahi kufanywa na GGM, lakini mgodi unaendelea kudai kuwa uliishafidia wahusika.
Diwani Suzana Mashala anasema mwaka 2006 alipofuatilia mgogoro huo, afisa uhusiano GGM wakati huo, aliyemkumbuka kwa jina moja la Msendo, alimwambia takwimu za mgodi zilikuwa zinaonyesha malipo yalishafanyika kwa watu 51 wa kitongoji hicho.
Imeelezwa na viongozi wa vijiji kwamba ni DC Mnali aliyesimamia tathmini ya kaya 44 na kuahidi mali za kaya saba zingetathminiwa wiki moja baadaye. Wiki hiyo haijafika hadi leo.
Katika kitongoji cha Nyamalembo, kuna wale ambao mali zao zilithaminiwa, kuna waliolipwa kwa shuruti ya DC na bila kujua thamani halisi ya mali zao; na bado kuna kaya saba ambazo mali zake hazijathaminiwa.
Juu ya yote haya, mnamo tarehe 28 Novemba 2006 wananchi wengi, hasa wa kitongoji cha Katoma walipata madhara makubwa kutokana na ulipuaji baruti uliofanywa na mgodi bila kuzingatia kuwepo kwa wakazi.
Barua ya wananchi 140 ya tarehe 4 Januari 2010 kwa Rais Jakaya Kikwete, ndiyo inafafanua hali halisi.
“Kuna waliolazwa hospitili ya wilaya, nyumba nyingi zimepasuka na nyingine kuanguka. Viongozi wetu walijua hili lakini walibeba mgodi na kutuacha wananchi tukipata taabu,” barua inaeleza.
Katika hali hii, mahakama ni muhimu ingawa haziwezi kutabilika; bali kilio cha wananchi kwa rais ndio kimbilio la mwisho.
Kuna suala la haki ya wananchi lakini pia kuna suala la wajibu na utashi wa rais kuondoa utawala wake katika tope la unyang’anyi wa mali na haki za wananchi.

0
No votes yet