Dhahabu yote ile, Kahama haina sekondari !


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

KAHAMA ni miongoni mwa maeneo kadhaa nchini yaliyobarikiwa kwa utajiri wa madini. Kuna migodi miwili mikubwa ya dhahabu; Bulyanhulu na Buzwagi ambayo ina historia chafu.

Mgodi wa Bulyanhulu ulianzishwa katikati ya shutuma kwamba wachimbaji madini wapatao 50 walifukiwa wakiwa hai katika ili kupisha mwekezaji. Pia mgodi wa Buzwagi ulikumbwa na kashfa ya waziri kutia saini katika mazingira ya kutatanisha. Migodi yote miwili inamilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold Mines.

Hata hivyo, pamoja na utajiri wake huo, wilaya hiyo ya mkoani Shinyanga haina shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita inayomilikiwa na serikali hadi leo.

Hiyo ni moja ya sababu zilizomfanya Charles Dotto Lubala, aamue kuwania ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

“Hebu fikiria, utajiri wote huu wa Kahama halafu hakuna hata shule moja ya sekondari ya kidato cha tano? Dhahabu yote inayovunwa pale inapelekwa wapi? Hili halikubaliki hata kidogo,” anasema Lubala katika mazungumzo yake na MwanaHALISI jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Alisema kutokuwapo kwa shule hiyo ni mojawapo ya matatizo makubwa ambayo akipata ridhaa ya kuwa mbunge wa Kahama, atajitahidi kuayaptia ufumbuzi katika miaka yake mitano ya kwanza ya ubunge.

Akimzungumzia mpinzani wake, James Lembeli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lubala alisema mbunge huyo ameshindwa kuwafanyia chochote wananchi wake.

Alisema tatizo kubwa la mbunge huyo aliyemaliza muda wake (Lembeli) ni kwamba alikuwa na ugomvi ndani ya chama chake (CCM), na hivyo hakuwa na mahusiano mazuri na wenzake.

Matokeo yake akawa anatumia muda mwingi nje ya jimbo na kupambana na maadui zake wa kisiasa badala ya kupambana na matatizo ya wana Kahama. Wananchi hawakumchagua apambane na watu, walimchagua awaletee maendeleo.

“Ombi langu kwa wana Kahama ni kumpumzisha Lembeli ili apambane na maadui zake anavyotaka. Sisi atuachie Kahama yetu tuiendeleze. Ninaomba wanipe fursa ya kuwatumikia,” anasema.

Lubala anasema tatizo kubwa la Kahama ni kuwapo kwa viongozi wa kiserikali na kichama, hususan wale wa CCM, ambao kazi yao kubwa ni kujinufaisha wenyewe badala ya wananchi.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Lubala kuwania ubunge; alifanya hivyo mwaka 1995 katika jimbo la Sumve kupitia chama cha Tada na mwaka 2005 kupitia chama hichohicho katika jimbo la Ilemela mkoani Mwanza.

Anasema mwaka huu ameamua kuwania ubunge jimbo la Kahama kupitia CHADEMA baada ya kuhama Tadea.

Kwa nini alihama Tadea, Lubala anasema ni kutokana na rais wao kukosa msimamo na kushabikia mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete.

“Rais wa chama chetu, John Lifa Chipaka, alitutangazia wanachama kuwa yeye anamuunga mkono mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

“Kwa maoni yake, alisema Kikwete ametekeleza ahadi zake kwa asilimia mia moja na yeye hana sababu za kumpinga. Akasema wale wanaopinga hilo, wanaweza kufanya maamuzi yao. Mimi nikaona hapa bora niondoke tu maana sikubaliani na mawazo hayo,” anasema.

Lubala alifanya tathmini na kuona Kikwete hajafanya kitu katika masuala mengi na hasa madini. Anasema zaidi ya utajiri huo wa madini ya dhahabu, Kahama pia imejaaliwa ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo lakini wakulima wametelekezwa na viongozi.

“Bila hata ya dhahabu, Kahama ingeweza kuendelezwa kwa kilimo tu. Tunalima pamba na tumbaku ambayo ni mazao muhimu ya kibiashara achilia mbali yale ya chakula,” anasema.

“Kahama ingepata bahati ya kuwa na viongozi makini na wenye kuona mbali, leo Kahama ingekuwa na sura nyingine kabisa. Tatizo la jimbo langu ni uongozi tu na mimi nataka kuonyesha hilo,” anasema.

Lubala anasema ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye uchaguzi huo wa Oktoba 31 mwaka huu, akisema CHADEMA ina ushawishi wa kutosha kushinda uchaguzi huo.

Anasema ingawa zamani CHADEMA haikuwa na nguvu sana Kahama, juhudi za waliokuwa wabunge wa chama hicho kama vile Zitto Kabwe na mgombea urais wa CHADEMA, Willibrod Slaa, kwenye kutetea maslahi ya wachimba madini, zimeongeza mvuto kwa wananchi.

“Jambo lingine la maana kulizungumzia ni operesheni Sangara. Pengine watu hawajui umuhimu wake lakini operesheni ile imeongeza mno nguvu ya CHADEMA kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini,” anasema.

Akieleza mipango yake mingine kwa jimbo hilo, Lubala anasema atahakikisha jumuiya za kuwezesha wananchi kiuchumi za SACCOS na VICOBA zinashirikisha watu wa jinsia zote, dini zote na itikadi zote tofauti na sasa ambako kuna upendeleo.

Pia, anasema atahakikisha Kahama kunajengwa stendi mpya ya mabasi ya kisasa, kulingana na hadhi ya mji huo ambao unakua kwa kasi katika miaka ya karibuni.

Katika huduma za kifedha, Lubala anasema haifurahishi kuona Kahama ambayo ina sifa zote za kuwa manispaa, kuwa na benki nne tu zinazofanya kazi, jambo linalopunguza maendeleo ya eneo hilo.

Kuhusu elimu, afya na utolewaji wa huduma za jamii, Lubala anasema atatekeleza ilani ya taifa ya CHADEMA, inayosema kuwa elimu itatolewa bure kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu.

Hata hivyo, mimi ni miongoni mwa watu wanaoumizwa sana na ugonjwa wa malaria. Watu wengi sana wa hapa Kahama wanakufa au kudhoofishwa na ugonjwa huu.

“Dhamira yangu ni kuhakikisha tunatokomeza malaria hapa Kahama katika kipindi changu cha ubunge. Ninaumizwa sana na ugonjwa huu,” anasema.

Lubala ni veterani wa siasa za upinzani nchini, akiwa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) kilichoongozwa na marehemu Chifu Abdallah Fundikira katika siku za awali baada ya Tanzania kurejesha siasa za vyama vingi mwaka 1992.

0
No votes yet