Diallo akana kughushi vyeti


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 03 March 2010

Printer-friendly version
Mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo

WIMBI la kujisafisha la watuhumiwa wa kile kinachoitwa “ufisadi wa elimu,” limepamba moto, imefahamika.

Wiki hii, mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo ameibuka na kusema, “Sikughushi vyeti.”

Amesema kinyume na inavyodaiwa, yeye ana vyeti halali na kwamba madai kuwa ana vyeti feki “ni ya kipuuzi na hayana msingi.”

Mwanasheria mmoja ambaye ametokea kujiita “mwanaharakati wa kupambana na ufisadi katika elimu,” kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, amekuwa akituhumu viongozi mbalimbali kwa kuwa na sifa bandia zinazohusiana na elimu.

Hivi karibuni, mwanasheria huyo, Kainerugamba Msemakweli, amechapisha kijitabu ambamo anaorodhesha majina 10 ya watu binafsi, wakuu wa mikoa, wabunge na mawaziri ambao amedai, ama wana sifa za kughushi au vyeti bandia.

Mmoja wa watuhumiwa ni Diallo, aliyewahi kuwa waziri wa maliasili na utalii na sasa anaendesha biashara, pamoja na nyingine, kampuni ya Sahara Communications ambayo inasimamia kituo cha televisheni cha Star TV, Radio Free Africa, radio Kiss FM na gazeti la Msanii Afrika.

Kainerugaba anadai, katika kijitabu chake kuwa, Diallo amewahi kuonyesha kuwa ana “digrii nane, stashahada mbili na diploma moja,” na kwamba ni “mchafu kama kaniki, tajiri kupindukia, amedanganya kielimu…”

Hata hivyo, Diallo amesema yeye amesomea Chuo Kikuu cha Phoenix, nchini Marekani, Chuo Kikuu cha Newcastle na Chuo Kikuu cha Havard. “Nimesomea katika vyuo vikuu vinavyoheshimika duniani,” anaongeza.

Diallo alikuwa akijibu swali la MwanaHALISI lililolenga kupata ukweli na kutaka kujua hatua gani amepanga kuchukua kusafisha jina lake.

Wiki mbili zilopita, mbunge wa Same Magharibi na naibu waziri wa kilimo Dk. David Mathayo, aliorodhesha sifa zake kitaaluma na kukanusha madai ya Kainerugaba kuwa yeye ni “fisadi wa elimu.”

Diallo amesema, “Kwa sasa, sijapanga kufungua kesi ya kuchafuliwa jina. Si kwa sababu nimedharau madai haya bali naendelea kutafakari na kutafuta taarifa sahihi za huyu mtuhumu,” anasema.

Akifafanua, Diallo amesema, “Unaweza kwenda mahakamani ukashitaki mtu ambaye hana hata uwezo wa kulipa gharama za kesi pale utakapokuwa umeshinda.”

Kijitabu cha Msemakweli kiitwacho “Orodha ya Mafisadi wa Elimu,” kimesheheni tuhuma za kughushi vyeti na sifa za elimu za baadhi ya viongozi wa serikali.

MwanaHALISI limebahatika kuona lundo la vyeti vya Diallo vinavyoonyesha kuwa alivipata katika vyuo mbalimbali duniani, ikiwemo shahada ya uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Newcastle, Uingereza.

Tatizo kuu lililoko katika kijitabu hicho, hata hivyo, ni kwamba kinanukuu zinazoitwa sifa za muhusika na kulundika tuhuma tu.

Hakina mpangilio wa nani anadai alisomea wapi na iwapo utawala wa chuo anachodai kusomea umethibitisha kutokuwepo jina la mtuhumiwa katika orodha ya wahitimu wake na masomo aliyochukua.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: