Digrii za Nchimbi, Kamala 'zaota mbawa'


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 November 2009

Printer-friendly version
Sasa waamua kurejea darasani
"Maprofesa" kibao nao wavuliwa wasifu
"Dokta" Emmanuel Nchimbi

MAWAZIRI wawili wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, miongoni mwa sita waliotajwa kujipa wasifu wa elimu wasiyokuwa nayo, wameanza kutekeleza mkakati wa kujisafisha.

Tayari imethibitika kuwa Diodorus Kamala, waziri wa ushirikiano wa Afrika Mashariki na Emmanuel Nchimbi, ambaye ni naibu waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa (JKT), hivi sasa wanasomea shahada ya uzamivu ya falsafa (Ph.D) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro.

Kamala na Nchimbi ambao walikuwa wakiitwa na kujitaja kwa kiambishi cha Dk., walisajiliwa na chuo hicho mwaka jana. Kamala ni mbunge wa jimbo la Nkenge, mkoani Kagera kupitia CCM. Kabla ya kuwa waziri alikuwa mkufunzi chuoni hapo.

Nchimbi ni mbunge wa Songea Mjini, mkoani Ruvuma. Wote wawili wanafanya mafunzo yao chini ya wakufunzi watatu tofauti.

Wakati Kamala anasimamiwa na Profesa Joseph Kuzilwa, Nchimbi anasimamiwa na Dk. Benedict Lukanima aliyemaliza shahada yake ya juu nchini Uingereza mwaka huu.

Dk. Lukanima anasaidiana na Dk. Matiku “kumfua” Nchimbi. Mafunzo hayo yanafanywa kwa mtindo wa utafiti, MwanaHALISI imegundua.

“Kama waliogopa au walizembea kusoma na kuamua kujipa sifa ambazo hawana, unadhani hivi sasa watasoma kweli?” ameuliza mwanafuzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambaye aliomba kutotajwa jina.

Nchimbi alipoulizwa na MwanaHALISI kwa nini ameamua kusoma shahada hiyo ya juu wakati yeye tayari anatajwa na kujiita mwenye shahada ya uzamivu (Dk), alikataa katakata kuzungumzia suala hilo.

“Mimi siwezi kuzungumza na wewe, mwambie bosi wako…(Kubenea, Saed) anipigie simu na kuniuliza,” alisema Nchimbi.

Alisema, “Sizungumzi na kila mtu. Nazungumza  na marafiki zangu, hapo kwenu rafiki yangu ni Kubenea…,” alisema na kukata simu.

Chuo Kikuu cha Mzumbe kimekwenda mbali zaidi katika kuwashughulikia wenye vyeti vyenye utata kwa kuwakana na kuwavua wasifu wa elimu waliothibitika kutokua nao.

Wakufunzi 12 wamevuliwa wasifu wa shahada ya uzamivu katika fani mbalimbali.

Pamoja na Kamala aliyekuwa mkufunzi kwenye  chuo hicho kabla hajawa waziri, kitabu cha maelezo ya chuo kikuu hicho, “Prospectus” cha mwaka 2007/2008, kinaonyesha kuwa walikuwa na shahada za uzamivu lakini katika vitabu cha mwaka 2008/2009 inaonyeshwa kuwa wamevuliwa.

Awali Kamala alitambuliwa na chuo hicho kuwa ana shahada ya uzamivu kutoka chuo kikuu huria cha Commonwealth. Hivi sasa ameishia kuwa na shahada mbili na kurejea kwenye uanafunzi.

Haijafahamika serikali inaweza kuchukua hatua gani kuhusu taarifa zao za muda mrefu kuwa wana shahada za uzamivu; bali wachunguzi wa mambo wanasema, katika mazingira ya kisiasa, mawaziri hao wamekumbwa na kashfa inayoweza kuwapokonya nafasi zao.

“Itategemea Rais Kikwete analionaje hilo; lakini anastahili kulichukuliwa kwa uzito unaostahili kwani linaathiri hadhi yake na ya serikali yake. Hao tumewasikia; je, wamo wangapi wa aina hiyo,” ameeleza Profesa Mshiriki kutoka chuo kikuu cha Mzumbe.

Katika mkakati wa kutambua na kuchukua hatua zinazostahili, Chuo Kikuu cha Mzumbe kimeonyesha kutotambua shahada za uzamivu za baadhi ya wakufunzi.

Miongoni mwao ni Profesa Moses Warioba ambaye alitambuliwa kuwa na shahada ya uzamivu ya utawala, sasa “shahada” yake hiyo haitambuliwi, imeeleza prostectus ya chuo.

Christopher Sotta, alitajwa kuwa ni Dk. mwenye shahada ya uzamivu ya utawala lakini sasa imekanwa.

Dk. Raphael Habi alitambuliwa kuwa na shahada ya uzamivu ya uongozi tofauti na sasa ambapo hatambuliwi hivyo na chuo hicho. `

Awali Arstarch Kiwango alitambulishwa kuwa na shahada ya uzamivu ya uchumi. Sifa hiyo sasa imeondolewa. Naye Dk. Colman Riwa, aliyekuwa anajitambulisha kuwa na shahada ya uzamivu ya utawala, amenyang’anywa hadhi hiyo.

Mwaka 2007/2008, chuo hicho kilimtaja Leonard Shio kuwa ni Profesa mwenye shahada ya uzamivu ya utawala. Siku hizi hatambuliwi hivyo.

Wengine waliotajwa na chuo hicho kuwa wana shahada za uzamivu bila kutaja vyuo walikozipata ni pamoja na Mujwahuzi Njunwa. Shahada yake ya uzamivu ilielezwa kupatikana nchini Marekani. Kwa sasa “imefutika.”

Prosper Ngowi alitajwa kuwa na shahada ya uzamivu ya Uchumi na Biashara; sasa haitambuliki; wakati Benard Nsana aliyetambulishwa na chuo kuwa ana shahada ya uzamivu, sasa hatambuliwi kuwa nayo.

Gabriel Elisante alikuwa anatajwa kuwa na shahada ya uzamivu ya masoko (Marketing) kutoka nchini Finland; sasa hatambuliwi hivyo.

Naye Didas Mrina alinadiwa na kujinadi kuwa ana shahada ya uzamivu ya biashara kutoka nchini Marekani, lakini sasa hanadiki hivyo tena.

Swali kubwa ambalo wengi wanajiuliza ni kwa nini imechukua muda mrefu kugundua hivyo. Aidha, ni kwa nini walimu wanapoomba kazi, hawaelezi vyema vyuo walikosomea na lini ili utawala uweze kufuatilia mkondo wa elimu yao.

“Mwanaharakati” Kainerugaba Msemakweli, amekuwa akitoa hadharani orodha ya majina ya watu, wakiwemo mawaziri, ambao anadai hawana digrii wanazodai kuwanazo.

Msemakweli anadai amepata taarifa hizo kwa njia ya utafiti na kwa msaada wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: