Dk Hoseah apime nafasi yake TAKUKURU


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 29 December 2010

Printer-friendly version

MWANAFALSAFA wa China aliyeishi karne ya 6 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo aliwahi kunena kwamba kuna vitu vitatu ambayo daima haviwezi kufichika; jua, mwezi na ukweli.

Ni kweli, katika miaka ya mwanzo ya 1970, Richard Milhous Nixon, Rais wa 37 wa Marekani, alijitahidi sana kuthibitisha kwamba kamwe hakuhusika na kashfa ya Watergate iliyokuwa ikimwandama, pale alipokuwa akijigamba: “Hakuna kitu cha kuficha ndani ya White House (Ikulu) yangu.” Baadaye kila mmoja alikuja kubaini ukweli wa kuhusika kwake.

Aidha katika karne ya 19, Arthur Conan Doyle, Mwingereza mtunzi wa riwaya za kipelelezi akimtumia ‘kachero’ wake maarufu Sherlock Holmes, alitoa tafsiri yake kuhusu neno ‘ukweli.’ Alisema, “baada ya kuondoa kisichowezekana, chochote kile kinachosalia, hata kama hakikubaliki, ndiyo ‘ukweli’ wenyewe.

Utangulizi huu unatia nguvu msemo maarufu usemao kwamba ‘katika rundo la uongo, ukweli hujitenga’ au msemo mwingine usemao ukweli huuma, ndiyo maana wengi huuogopa au kuukwepa.

Katika dunia ya utandawazi unaoletwa na Intaneti, televisheni za satelaiti na mawasiliano mengine ya kielektroniki, ni vigumu kuficha ukweli, iwe katika ngazi za kiserikali au kimataifa.

Kwa mfano serikali haiwezi kudanganya bei halisi ya mashangingi inayonunua kutoka Japan wakati mtu yeyote anaweza kupata bei hiyo kwa sekunde chache kupitia Intaneti.

Lakini kikubwa zaidi ni kwamba hata mambo mengine yanayozungumzwa na wakubwa nyuma ya pazia sasa yanaanikwa hadharani na kuwaumbua wakubwa hao mbele ya wananchi wao.

Hayo ndiyo yaliyowakuta Rais Jakaya Kikwete na Dk. Edward Hoseah, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wiki iliyopita.

Mazungumzo yaliyofanywa nyuma ya pazia kati ya Dk Hoseah na Purnell Delly, mwanadiplomasia wa Marekani hapa nchini ambaye anatajwa kuwa ni jasusi yalinaswa na kufichuliwa na mtandao wa Wikileaks.

Hoseah alinukuliwa akilalamika kwa mwanadiplomasia huyo kwamba bosi wake (Kikwete) ndiye kizuizi kikubwa cha jitihada zake za kuwafikisha mahakamani vigogo wa serikali wanaobeba tuhuma za ufisadi, wakiwemo rais wa zamani na waziri mkuu.

Mazungumzo baina ya wawili hao yaliyofanywa miaka mitatu iliyopita yalifanyika faragha na hivyo si Hoseah wala Delly aliyekuwa na hata chembe ya shaka kwamba yangeweza kuja kuwekwa hadharani baadaye.

Hali hiyo ilitengeneza mazingira huru kwa kila mmoja wao kutoa mawazo yake, na hivyo hakuna shaka yoyote kwamba kilichozungumzwa na Hoseah na kunukuliwa na Delly kilikuwa cha kweli, kweli tupu.

Kwa hili angalau Hoseah amesema kilicho cha ukweli, ambacho wengi wamekuwa wakihisi kwa muda mrefu. Kitu cha kujiuliza ni kwa nini Hoseah amekuwa aking’ang’ania nafasi aliyonayo pamoja na kuwapo kwa pingamizi kubwa dhidi ya utendaji wake?

Kwa tafsiri yoyote ile, hii ni kashfa kubwa sana kuikumba serikali pengine kuliko hata ile ya EPA. Na swali kubwa linalojitokeza mara moja ni nani kati ya wawili hawa, Hoseah na bosi wake (Kikwete) ambaye ameumbuka zaidi kutokana na uvujaji wa habari hii?

Hakika ni Kikwete. Kwanza, kashfa hii imemweka Rais moja kwa moja kwenye mstari wa mbele kwamba ndiye kikwazo kikubwa cha vita dhidi ya ufisadi nchini, pamoja na matarumbeta mengi majukwaani kutoka viongozi mbalimbali wa serikali hiyo.

Ukweli ni kwamba Kikwete hajawahi kuwa mpiga tarumbeta mzuri dhidi ya ufisadi. Tangu pale alipolazimika kusimama bungeni mapema Agosti 2008 na kutoa ‘ufafanuzi’ na ‘hukumu’ kwa watuhumiwa wa uchotaji wa mapesa ya EPA, haikumbukwi lini tena alishika tarumbeta kulaani ufisadi bila ya kutafuna maneno. Na hata katika kampeni za uchaguzi uliopita, ufisadi haukuwa agenda katika hotuba zake.

Bali miaka minne iliyopita, Kikwete alionekana hadharani akitetea hoja ya kutowachukulia hatua watuhumiwa vigogo wa ufisadi – hususan wakuu wa nchi (marais) waliomtangulia.

Sababu aliyotoa kuhusu kauli hiyo ni kwamba eti utamaduni wa kuwafikisha mahakamani huwafanya baadhi ya marais walio madarakani kubadilisha katiba ili kuendelea kun’gang’ania madarakani.

Hakika sababu hii, ingawa ina kiasi fulani cha ukweli ndani yake, haikuwa na mantiki au tija yoyote, achilia mbali kwamba ni uthibitisho mwingine wa utawala mbovu usiokuwa na maadili na uwajibikaji.

Angalau Kikwete angetaja kifungu cha Katiba kinachowakinga marais wastaafu kutochukuliwa hatua za kisheria kwa makosa walioyofanya wakiwa madarakani, kifungu ambacho wanasheria wengi wamesema kina utata mkubwa katika tafsiri yake. Hisia ni kwamba hakukitaja kwa vile kina utata.

Pili, kashfa hii imethibitisha kukosekana umakini katika uteuzi wa watendaji wakuu wa serikali yake. Ukweli Dk Hoseah amepwaya sana katika nafasi aliyonayo na hii imethibitishwa na si mwingine bali yeye mwenyewe (Hoseah).

Mara mbili amejikuta anatoa taarifa za kuwasafisha watuhumiwa wakuu wa ufisadi, kwanza mwishoni mwa mwaka 2007 kuhusu Waziri mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa kutokana na kashfa ya kampuni ya Richmond, na hivi majuzi tu kuhusu mwanasheria Mkuu wa serikali wa zamani, Andrew Chenge, katika kuhusika kwake na kashfa ya ununuzi wa rada.

Mara zote hizi mbili Hoseah alijikuta anaumbuka pale ukweli ulipodhihirika baada ya muda mfupi. Kwa hali ya kawaida, mara zote mbili alitakiwa ajiuzulu, lakini hakufanya hivyo kwa madai aliyemteua bado ana imani naye.

Na kama hatajiuzulu kutokana na kashfa hii ya Wikileaks au kuondolewa na bosi wake, basi maadili na uwajibikaji katika serikali hii umekwenda chini kwa kiasi cha kutisha. Na Kikwete ndiye wa kubeba lawama.

Kama Hoseah alijisikia huru kuzungumzia masuala nyeti na mwanadiplomasia huyo kutoka taifa la nje, sembuse kuhusu mazungumzo yake na watu wengine wa humu humu ndani?

Je, anaweza vipi kuwalinda watoa taarifa za ufisadi? Si anaweza kuwafichua kwa watuhumiwa? Au analifanya suala zima la ufisadi ni mchezo wa kuigiza na hivyo kuwa dhihaka kubwa?

Inawezekana analifanya kuwa dhihaka. Mwishoni mwa mwaka 2007, katika mkutano wake na waandishi wa habari Hoseah alibanwa kwa kushindwa kwake kuwafikisha mahakamani vigogo wa serikali waliokuwa wanatuhumiwa katika ufisadi wa Mwananchi Gold, Meremeta, Deep Green Finance, maghala ya NSSF ya Ubungo na ufisadi mwingine.

Akijibu hoja hiyo alisema anangojea washerehekee sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa amani na utulivu kwani anajua wengi wao wana maradhi ya moyo na shinikizo la damu.

Alisema baada ya sikukuu atawashukia bila huruma. Hakufanya hivyo kwa sababu hakuwa anazungumzia ukweli na hivyo kulifanya suala zima kuwa dhihaka.

Lakini ukweli wa dhihaka hii ulikuwa haujabainika. Ukweli ulikuwa umejificha ndani yake na Wikileaks uliomweka peupe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: