Dk. Lwaitama atunisha msuli


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version

MWALIMU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Feza Lwaitama, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinastahili kupumzishwa ili kipate muda wa kujirekebisha na kujirudi.

Mwanachama wa CCM, ambaye huwa hafichi uanachama wake, ndani na nje ya chuo, Lwaitama sasa anasema, “imetosha.”

“Kwa hakika nimeamini, chama cha CCM kinahitaji kuondolewa kwa amani madarakani; kwani baadhi ya mashabiki wake wamelewa madaraka ya chama chao kuwa madarakani kwa muda mrefu,” anaeleza.

Katika andishi lake la juzi Jumatatu, kwa gazeti hili, Lwaitama anasema, “Hima wana CCM makini; wenye kuamini katika itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea; nendeni kupiga kura ya kukipumzisha chama chenu ili kipate muda wa kujirekebisha na kujirudi.”

Kauli ya Lwaitama inafuatia taarifa za vitisho kwa njia ya simu za mkononi (sms) kwamba atafukuzwa chuoni kama alivyofukuzwa Profesa Mwesiga Baregu.

Dk. Lwaitama anasema amelazimika kutoa msimamao huo kwa kuwa aliyekuwa anatuma ujumbe alikuwa ni mfano wa mashabiki wa CCM, kama chama tawala.

Amsema mashabiki wa aina hiyo “… wana hulka ya kutoa vitisho na labda hata kuwa tayari kuua yule waliyemwona kuwa na mawazo tofauti na yale ya viongozi wakuu wa chama hiki kwa sasa.” 

“Aliyekuwa anatuma ujumbe huu alionyesha wazi ni mtu wa karibu kiasi fulani na watawala, na alionyesha kiburi na jeuri ya kutawala bila kujua mipaka ya kisheria ya watu walio madarakani,” ameeleza Lwaitama.

Alhamisi iliyopita, tarehe 14 Oktoba, Jumuia ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), ilitayarisha mkutano wa kumbukizi za miaka 11 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere, kwenye Ukumbi wa Mihadhara wa Nyerere, pale Mlimani.

Kaimu Mwenyekiti wa UDASA, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa UDASA, Dk. Kitila Mkumbo, ndiye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo wa kumbukizi. 

Lwaitama anasema, “Katika mkutano huo mimi nilitoa mada ya kuchokoza mjadala iliyohusu Dhana ya Umajumui wa Kiafrika na Uzalendo kama inavyoelezeka kwa viojo vya falsafa za Mwalimu Nyerere kuhusu umoja wa taifa la Tanzania na haki na wajibu wa raia wake.”

Miongoni mwa aliyosema ukumbini ni pamoja na kukiri hadharani kuwa yeye ni mwanachama wa CCM aliyesitisha kulipa ada ya uanachama kwa muda mrefu.

Alisema angefufua uanachama wake pale chama hicho kitakapokuwa kimepumzishwa kuongoza dola la Tanzania.

Dk. Lwaitama alisema wakati huo, “viongozi wasiofanana na historia na malengo ya awali ya TANU, na baadaye CCM, watakuwa wamekikimbia na kujiunga na chama au vyama vitakavyokuwa tawala wakati huo.”

Ufananuzi huo wa Lwaitama ulifuatia kauli ya mmoja wa washiriki, Saed Kubenea “…kunibeza hadharani kwa kujinasibu kama mwanachama wa CCM wakati kama huu; ambapo yeye alidhani watu wote wenye kuitakia mema nchi hii walitakiwa kutojinasabisha na chama hiki.”

Vyombo vya habari – televisheni, redio na magazeti, vilitangaza maoni ya Lwaitama kuwa CCM kilistahili kupumzishwa kuongoza dola ndipo atafufua uanachama wake.

“Kwa ulofa wangu, nilidhani nilichokisema pale kingeweza kuwashawishi Watanzania ambao ni wanachama wa CCM, wawe hai au wafu kama mimi, kuendelea kuwa wanachama wa chama hiki,” anaeleza Lwaitama kwa kauli inayoonyesha masikitiko.

Anasema alitoa kauli hiyo “…hata kama katika uchanguzi wa tarehe 31 Oktoba mwaka huu, wanachama wa CCM wangeshawishika kukipumzisha chama chao kwa kumpigia mgombea wa kiti cha urais aliyependekezwa na chama ambacho ni cha upinzani kwa hivi sasa.”

“Kauli yangu hii inaoana hata na ushauri uliotolewa na viongozi wengi wa asasi za kiraia pamoja na viongozi wa dini, hasa KKKT na Katoliki, kuwa wapigakura wachague mgombea kwa uadilifu na umakini wake katika kutumikia watu na uzalendo wake,” anaeleza katika andishi lake.

Anasema wanachama hawapaswi kukwazwa na uchanga au ukongwe wa chama kilichomsimamisha mgombea mwenye sifa hizo.

“Nillikuja kujua kuwa kweli mimi ni lofa nilipopokea ujumbe wa simu ya mkononi ukinituhumu kujidhalilisha na kuwa nilikuwa nimeonyesha chuki binafsi na kukosa uadilifu wa kisomi ambao, eti unatakiwa kujidhihirisha kwa kutotoa maoni yoyote yanayoweza kushawishi watu kutowachangua wagombea wa CCM,” anaeleza.

Dk. Lwaitama anasema, “Picha niliyopata kwa ujumbe wa sms hizi, ni kwamba eti nilikuwa nimepoteza mwelekeo na nilikuwa nimejichanganya kwa vile usomi mahili unajidhihirisha katika msomi kutoa matamshi yenye kukibeba chama hiki tawala!”

“Nilionywa kuwa kwa kuonyesha kutangaza ushabiki wangu wa kiitikadi, sijui labda kwa kusema CCM kipumzishwe ili nijiunge nacho upya, basi wanafunzi wangu chuo kikuu tayari walikuwa wameonyesha wasiwasi wa mimi kuwafelisha,” anasema Dk. Lwaitama.

Amesikitikia wenye mawazo na kauli za aina hiyo akisema, “Sikuelewa hawa wanafunzi ningejuaje kuwa ni wa chama tawala na sikuelewa hii tuhuma ilitolewa kwa kiwango gani na uwezekano wa mwalimu yoyote wa chuo kikuu kumfelisha mwanafunzi kwa vile ni mwanachama wa chama cha siasa.”

“Inaelekea huyu mtu, na watu wa aina yake na washabiki wa CCM ya leo, ni watu wenye uelewa mdogo hata wa sheria na kanuni za serikali yao,” anasema.

Mbali na vitisho vya sms, Dk. Lwaitama anasema watuma ujumbe wanaonekana kutojua vema Waraka wa Utumishi wa Umma wa mwaka 2000.

Anasema waraka haukatazi mwanataaluma kuwa mwanachama wa chama cha siasa kama inavyodaiwa na wengi, wala Prof. Baregu hakunyimwa mkataba mwingine kwa vile alikuwa mwanachama wa chama cha siasa.

“Waraka unasema uanachama ruksa, lakini mwanataaluma asiwe kiongozi wa kuchanguliwa wa chama cha siasa na asichangie mawazo yake kwenye mikutano ya hadhara iliyoitishwa na chama cha siasa.”

Katika hoja hii anasema mkutano ulitaoyarishwa na UDASA, na kufanyika ukumbi wa mihadhara ya chuo kikuu, si mkutano unaozungumzwa katika waraka wa utumishi.

Dk. Lwaitama anasema watu wa ina ya wale waliompelekea sms, wakipewa mamlaka, “ni wepesi kuyatumia vibaya na hata kuwa tayari kukatisha maisha ya wale wenye mawazo wasiyopenda.” 

Ujumbe uliotumwa kwa Dk. Lwaitama ulipitia simu Na. +255 784 758000 saa 2.12 usiku wa 15 Oktoba; na Na. +255 655 558000 saa 5.57 mchana wa tarehe 16 Oktoba na kuendelea kuporomosha vitisho siku nzima. 

Pamoja na mengine, sms zilisema, “Umepandikiza chuki sana kwa wana CCM ambao unawafundisha pale mlimani. Mabalozi wenyewe watapima kama kweli kwa kauli zako utawatendea haki kwenye mitihani wanafunzi wapenzi na washabiki pale mlimani.”

Ujumbe mwingine ulioanzisha mjadala ulisema, “Nasikia Lwaitama jana ameharibu mjadala kwa kuugeuza na kuufanya kampeni ya CHADEMA.”

Mwingine ulisema, “Amejidharirisha sana kwa kuwataka watu waiangushe CCM,” wakati mwingine ulisema, “…aachie chuo akavae magwanda kama Baregu.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: