Dk. Migiro: Urais si saizi yake


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Dk. Asha-Rose Migiro

KUNA haja ya kutoa onyo kwa wasiokuwa na nia njema kwa Dk. Asha-Rose Migiro. Waache njama za kutaka “kumwangamiza.”

Wanachombeza chinichini. Wanasema ndiye anastahili kuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015.

Nionavyo, hana ubavu.

Dk. Migiro alirejea nchini wiki iliyopita akitokea Umoja wa Mataifa (UN) ambako amekuwa Naibu wa Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa umoja huo kwa miaka mitano na nusu.

Nafasi ya Migiro makao makuu ya UN ilikuwa ya “kumsaidia” Ban Ki-Moon.

Ni kama Rais Ali Hassan Mwinyi alivyotaka msaada akaunda nafasi ya “naibu waziri mkuu.” Alimwita Augustine Mrema na kumchomeka.

Sasa Migiro amerejea kwa mbwembwe za kuwa na “uzoefu kibao” katika mambo mbalimbali.

Hapo ndipo wachombezaji wanapomdaka na kupeperusha kile kilichokuwa kikisikika kimyakimya kuwa “huenda akagombea urais 2012.”

Hawaulizi kwanini Migiro hakumaliza ngwe yake pamoja na yule aliyemteua – mwaka 2016. Hawaulizi.

Hawataki kuuliza ni kazi gani ambazo zimempa uzoefu mkubwa. Hawaulizi “uzoefu mkubwa” upi na wa kufanyia kitu gani.

Wanachosema ni kwamba katoka UN na sasa anaweza kugombea urais. Wanajua vema kwamba urais haupatikani kwa uzoefu wa kufanya kazi alizokuwa akipewa na Ba Ki-Moon.

Kwa msisitizo, urais hautoki nje ya nchi. Hakuna uzoefu unaoongoza katika kuwa rais. Huwezi kupata uzoefu wa kuwa rais kabla hujawa rais.

Ni vema tu kukubali kwamba Dk. Migiro ana bahati. Nafasi aliyokuwa nayo kwa Ban Ki-Moon haimo katika mfumo wa UN. Ni ya matakwa ya aliyeshika nafasi ya ubosi wa umoja huo.

Nafasi hiyo, ndani ya ofisi ya katibu mkuu, ni tofauti na zile za kuongoza mashirika ya UN.

Chukua mfano wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UNHABITAT) lililokuwa likiongozwa na Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji.

Hapa, ili uwe mkuu wa shirika kama hilo, sharti uchekechwe; upigiwe kura na mataifa katika Baraza la Umoja wa Mataifa. Kufahamika tu kwa katibu mkuu hakusaidii na hakuthaminiwi.

Hata ukipata nafasi hiyo, kama hukuonyesha matunda unatupwa nje. Yako mataifa, kwa mfano ya nchi za Nordic, ambayo yana akinamama mahiri kweli na wasiohitaji kuteuliwa bali kushindana na kushinda.

Dk. Migiro amekuwa karibu na akina mama hao. Atakuwa ameona jinsi wanavyochapa kazi.

Huku nyumbani atakuwa ameona mwananchi mwenzake, Prof. Tibaijuka alivyoendesha shirika la UNHABITAT kwa mihula yote miwili kwa ustadi na mafanikio ambayo yanatishia yule aliyeshika nafasi yake sasa.

Bali tunaweza kukubali kuwa katika kutumwa huku na kule, Dk. Migiro atakuwa amejaribu kujifunza kuwa meneja wa taratibu katika ofisi yake; lakini siyo kiongozi.

Kuwa kiongozi anahitaji usadiki wa kweli wa anachotaka kufanya; dhamira ya dhati na iliyothibitika ya anacholenga; na uwezo mkuu wa kukisimamia. Dk. Migiro hajafika huko.

0
No votes yet