Dk. Mponda hajui jukumu alilopewa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

JESHI la Polisi kupitia kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wiki iliyopita lilitoa ufafanuzi kuhusu hali ya afya inayomkabili Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe likisisitiza “hajalishwa sumu”.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya watu kadhaa akiwamo Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, mara mbili kukaririwa na vyombo vya habari wakidai kuwa Dk. Mwakyembe amelishwa sumu.

Matamshi hayo yanayoashiria jinai ndiyo yalilazimisha Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kuanzia siku aliyougua, ripoti ya Hospitali ya Muhimbili alikolazwa na ripoti ya hospitali ya Apollo, India anakotibiwa.

Mgonjwa yeyote anapopelekwa nje kwa gharama za serikali, anakwenda na ripoti kutoka hospitali aliyotoka na akirudi hupewa ripoti ya kurejesha serikalini ili itumike kujua kinachomsumbua, gharama za matibabu na safari.

Kwa vile huu ni utaratibu uliowekwa na serikali, hatuelewi kwa nini Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda hajawahi kuiona ripoti hiyo, ambayo iko wizarani kwake, inayomhusu waziri mwenzake na inabishaniwa.

Sisi tungemwelewa Waziri Mponda kama angesema hawezi kusema kinachomsumbua naibu waziri huyo kwa kuwa ni siri ya mgonjwa mwenyewe, lakini si kudai kwamba eti hajawahi kuiona ripoti. Kama waziri huyo hajawahi kuiona ripoti, Jeshi la Polisi limepika ripoti hiyo?

Alichokifanya Waziri Mponda si kulinda heshima yake, bali atasababisha Jeshi la Polisi lisiaminike tena na ameiingiza serikali katika mnyukano wa ndani kwa ndani.

Tazama, Waziri Sitta anadai Dk. Mwakyembe kalishwa sumu; Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi inasema naibu waziri huyo hajalishwa sumu, halafu Mponda anaruka kimanga!

Tuliamini, baada ya Sitta na Jeshi la Polisi kutofautiana, kwa sababu bila shaka ya misimamo ya kambi za kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, Dk. Mponda alipaswa kuondoa shaka na kuweka rekodi sahihi, lakini yeye amelikana Jeshi la Polisi, hivyo kumwacha Waziri Sitta akisimamia anachoamini bila ushahidi wa kisayansi.

Maana yake nini? Kama hajaiona ripoti inayoeleza matatizo ya Dk. Mwakyembe na aina ya matibabu, wizara imemruhusu vipi kwenda tena India kutibiwa kwa gharama za serikali? Dk. Mponda amethibitisha hajui majukumu aliyopewa.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: