Dk. Mwakyembe akataa kujiuzulu


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe amesema hana mpango wa kujiuzulu.  “Nitapambana humuhumu ndani ya serikali,” amesema bila kutaja atapambana na nani.

Katika mahojiano maalum na gazeti hili mara baada ya kuongea na waandishi wa habari juzi, Jumatatu, mjini Dar es Salaam, Dk. Mwakyembe alikana kupanga kujiuzulu.

Kwa zaidi ya miezi mitatu sasa kumekuwa na tetesi kwamba Dk. Mwakyembe amesambaza taarifa kwa baadhi ya ndugu na marafiki akiwaeleza kuwa anataka kujiuzulu uwaziri.

Lakini alipoulizwa juu ya mpango huo, waziri alijibu taratibu, “Sina kabisa mawazo ya kujiuzulu. Ugonjwa unaonisumbua sasa umepona.”

Dk. Mwakyembe hakusema lolote iwapo rais aliyemteua atampumzisha, hasa ikitiliwa maanani kuwa anahitaji muda wa kupumzika na kurejesha afya yake ya mwili.

Hii ni mara ya pili katika wiki moja viongozi wawili kutamka kuwa “watapambana” lakini hawataji watakayepambana naye.

Alhamisi iliyopita, mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, akitokea Ujerumani, alisema kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere kuwa ana afya njema na “tayari yupo kupambana.”

Dk. Mwakyembe alizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Holland House, mtaa wa Samora, Jumatatu, ikiwa ni siku tatu tokea awasili nchini kutoka India alikokwenda kuangaliwa afya yake baada ya kuwahi kulazwa hospitalini Apollo, mjini Hyderabad.

Mbunge huyo wa Kyela, mkoani Mbeya kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa anaingia ofisini kwake kwa mara ya kwanza katika miezi mitano, isipokuwa alipokwenda ofisini kwa katibu mkuu wake kutoa salamu tu.

“Sasa kwa hakika sijambo,” aliwaeleza waandishi wa habari waliofurika hapo. “Wale waliodhani ningekufa au kung’oka, wahesabu kuwa hawajafanikiwa. Mimi nipo na mzima sasa; nitaendelea kuishi na napambana nikiwa ndani.”

Dk. Mwakyembe anasema sasa atabaki kutumikia wadhifa alioupata wakati Rais Jakaya Kikwete akiunda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa 2010, na kusisitiza, “Mwenye mamlaka ya kuteua mawaziri, kubadili waziri au kumuondoa katika nafasi yake ni rais.”

Amesema, “Nimerejea, na nimekuta mafaili mengi mno mezani kwangu. Natakiwa kuyafanyia kazi… ndiyo kazi niliyopewa kuifanya na rais.”

“Mimi niko kazini na ifike mahali sasa suala la Dk. Mwakyembe kuumwa lifike mwisho. Nami ni binadamu jamani,” alisema huku sura yake ikionyesha huzuni.

Kuhusu asili hasa ya ugonjwa uliomsumbua, Dk. Mwakyembe alisema ni ugonjwa wa ngozi, ila alikataa kufafanua ulivyo.

Alisema yupo tayari kuelezea kwa ufasaha suala hilo atakapoulizwa na kamati ambayo alisema imeundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani kufuatilia mazingira yaliyodaiwa kusababisha ugonjwa huo.

Dk. Mwakyembe amesema Waziri Shamsi Vuai Nahodha ameunda kamati ya maofisa wapelelezi wa polisi kuchunguza tuhuma kuwa huenda alilishwa sumu.

“Madaktari wamesema nina ugonjwa wa ngozi,” alisema. Alipoulizwa ni ugonjwa gani hasa, alisema, “Nina skin disorder…” au mparaganyiko katika ngozi yake.

Maneno mengine aliyoyataja baada ya hapo, hayakueleweka. Alikataa ombi la mwandishi huyu kutaka amwandikie aina ya ugonjwa wake. Alikataa pia kutaja herufi.

Siku chache kabla ya kuondoka nchini, Dk. Mwakyembe alisikika akilalamika kuwa anakabiliwa na ugonjwa wa ngozi.

Alitaja madhara ya ugonjwa huo kuwa ni kuwashwa mwili mzima na kila alipojikuna alibambuka ngozi, kutokwa ungaunga na nywele kunyonyoka.

Dk. Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria ambaye pia alisomea na kufanya kazi ya uandishi wa habari, alilalamika kuwa amekuwa akiandamwa na maadui zake kisiasa lakini hakuwahi kutaja kwa majina.

Kihistoria, mashaka yanayomsibu yalianzia alipowahi kulalamika kutishiwa maisha yake. Ilikuwa ni muda mfupi baada ya kunusurika kifo katika ajali ya gari.

Gari lake aina ya Toyota Land Cruiser, lilipinduka eneo la Mafinga, mkoani Iringa wakati akitoka Mbeya kurejea jijini Dar es Salaam. Yeye na dereva wake walinusurika.

Alilalamikia uchunguzi wa polisi akidai ndio maana walibaki kumlaumu dereva wake badala ya kumpongeza kwa kile alichoita “umahiri uliosaidia kutunusuru.”

Mara moja aliorodhesha vituko na washiriki wengi katika kilichoonekana kama sinema ya maigizo, watu wenye nia ya kumuua. Hajapata kutaja maadui zake wengine waziwazi.

Kumekuwa na madai kuwa huenda hofu yake inatokana na ripoti aliyowasilisha bungeni mwaka 2007 alipoongoza kamati teule ya bunge kuchunguza mazingira ya mkataba wa Richmond wa kuzalisha umeme wa dharura.

Katika ripoti hiyo, Dk. Mwakyembe alieleza kuwa mkataba huo uligubikwa na mazingira ya ufisadi kwa kuwa kampuni hiyo ilipewa zabuni wakati haikuwa na uwezo kifedha, zana wala utaalamu.

Ripoti ilisababisha Edward Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu, kujiuzulu baada ya kubainika alishinikiza Richmond ipewe zabuni ingawa alijua wataalamu ya wizara ya Nishati na Madini walithibitisha kuwa haikuwa na sifa.

Dk. Mwakyembe ameshukuru viongozi wa wizara, akiwemo Waziri Dk. John Magufuli na wasaidizi wake pamoja na wafanyakazi, kwa kufanya kazi wakati akifuatilia matibabu.

0
Your rating: None Average: 3.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: