Dk. Ng'wandu sasa apaa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 April 2008

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

LEO Dk. Pius Yasebasi Ng'wandu anawasilisha hoja nzito mjini Vienna, Austria juu ya maendeleo ya nishati ya nyuklia kwa ajili ya kujenga amani na ustawi wa binadamu.

Dk. Ng'wandu aliteuliwa 3 Januari mwaka huu kuwa Kamishena wa Tume ya Watu Mashuhuri Duniani juu ya Nishati ya Nyuklia (Commission of Eminent Persons – COEP).

Ni tume hii inayokutana Vienna kuanzia leo hii na kuendelea kwa siku tatu.

Tume hii ya watu mashuhuri 18 imo ndani ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA) ambalo mkurugenzi wake mkuu ni Mohamed ElBaradei.

Ni Ng'wandu huyohuyo aliyekuwa mbunge wa Maswa hadi mwaka 2005 alipochagua kustaafu ubunge na kujitumbukiza katika masuala makubwa yanayolingana na taaluma yake.

Katika Tanzania na nchi nyingine, kuna wanasiasa waliochagua "kufia" kwenye ofisi za kisiasa kwa kuwa hawana jingine lolote wanalolijua, walilosomea au wanalokumbuka isipokuwa jukwaa la kubadilishana kauli na "kutunga sheria."

Dk. Ng'wandu ni tofauti na hao. Leo hii anashughulika na masuala mazito ya nyuklia katika Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (International Atomic Energy Agency – IAEA).

Kwenye hadhira ya Vienna, mada kuu ni "Nafasi ya IAEAkatika Maendeleo ya Nishati ya Nyuklia kwa ajili ya Usalama wa Dunia na Ustawi wa Binadamu."

Magwiji 18 wanajadili mada hii. Hawa ni Makamishena wa Tume ya Watu Mashuhuri Duniani juu ya Nishati ya Nyuklia (Commission of Eminent Persons – COEP). Dk. Ng'wandu ni mmoja wao.

Dk. Ng'wandu ni Mtanzania pekee katika Tume hii. Vilevile ndiye mwakilishi wa Afrika Kusini mwa Sahara. Afrika inawakilishwa na watu wawili. Mwingine anayewakilisha kanda ya kaskazini mwa Afrika anatoka Nigeria.

Mzaliwa wa kijiji cha Budekwa, wilayani Maswa, miaka 65 iliyopita, Dk. Ng'wandu alisomea ualimu, sosholojia na sheria katika masuala ya menejimenti ya raslimali maji.

Nafasi ya sasa ya Dk. Ng'wandu inakaribia kuhitimisha safari yake ndefu ya utumishi na uwakilishi.

Alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais; Waziri wa Nchi, Maji, Nishati na Madini; Waziri wa Ardhi, Maji na Maendeleo ya Miji; Waziri wa Maendeleo ya Maji; Waziri wa Biashara, Viwanda; Waziri Mawasiliano na Ujenzi; Waziri wa Maendeleo ya Maji na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu.

Dk. Ng'wandu amekuwa Balozi katika nchi za Japan, Australia na Philippines na amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Kamishna wa Tume ya Mipango.

Aidha, Dk. Ng'wandu amekuwa mwenyekiti wa bodi za taasisi mbalimbali zikiwemo Chama cha Elimu ya Watu Wazima; Shirika la Migodi Tanzania (STAMICO); Tume ya Taifa (UNESCO) Tanzania na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH).

Mwenyekiti wa Umoja wa Mawaziri wa Afrika (Sayansi/Teknolojia); Makamu wa Kwanza wa Bodi ya Uongozi ya IICBA (UNESCO) na Mjumbe wa Baraza la Udhamini la Taasisi ya Mafunzo ya Teknolojia (ACTS).

Dk. Ng'wandu ni mwanzilishi wa Taasisi ya Sayansi Tanzania (FTAAS) na Mzawadiwa Medali ya Dhahabu katika jumuiya ya wasomi wa sayansi mwaka 2000.

"Leo hii, mimi ni Mshauri Mtaalamu kitaifa na kimataifa," anasema Dk. Ng'wandu. Anatokea kwenye makampuni ya YASECONSULT na YASEKON ambako ni Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji tangu 2006.

Tume ta Kimataifa ya Nyuklia kwa matumizi salama (COEP), inaongozwa na rais wa zamani wa Mexico, Ernesto Zedillo, ambaye ni mwenyekiti.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, ElBaradei ni msomi na mtaalam aliyetajwa sana wakati Marekani ikihangaika kutafuta uhalali wa kuivamia Iraq kwa kisingizio cha kuwa inamiliki silaha za maangamizi (Weapons of Mass Destruction - WMD).

Tume ya Dk. Ng'wandu na wenzake 17 imepewa jukumu la kutathmini changamoto za matumizi ya nyuklia kwa njia ya usalama na maendeleo ya binadamu kuanzia mwaka 2020 na miaka ijayo.

COEP iliundwa na kikao cha IAEA, cha 25-26 Februari mwaka huu, pamoja na mambo mengine, iandae mifumo ya kuiwezesha kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake mazito katika kipindi ambacho IAEA inatimiza miaka 50 tangu ianzishwe.

Tayari Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wamempelekea Dk. Ng'wandu pongezi kwa uteuzi huu.

Tume ya Dk. Ng'wandu na wenzake inakuja wakati mataifa makubwa yanashinikiza Iran na Korea Kaskazini kusitisha uzalishaji wa nguvu ya nishati ya nyuklia kwa madai kuwa "unahatarisha" usalama wa dunia.

Swali ambalo ni muhimu wapenda maendeleo wajiulize ni je, mbongo 18, zikiwemo za Dk. Ng'wandu, zitaambukiza fikra mpya na kuleta mwelekeo mpya katika matumizi sawa na sahihi ya nyuklia?

Makamishena wa COEP ni Ernesto Zedillo (Mexico) mwenyekiti; Balozi Ng'wandu; Balozi Oluyemi Adeniji (Nigeria), aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Magavana wa IAEA.

Lakhdar Brahimi (Marekani), aliyewahi kuwa msaidizi na mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa UN; Lajos Bokros (Hungary), Profesa (Uchumi na Sera za Umma).

Wengine ni Dk. Rajagopala Chidambaram (India) ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Nishati ya Atomiki na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Atomiki cha Bhabha.

Makamishena wengine ni Seneta Lamberto Dini (Italia), Rais wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge; Gareth Evans (Australia), Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Usuluhishi cha Brussels, Waziri wa Mambo ya Nje (1988-1998) na Waziri wa Maliasili na Nishati (1984-1987).

Louis Frechette (Canada), Mwanazuoni Mahsusi katika Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Uvumbuzi na aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na Msaidizi wa Katibu Mkuu, UN.

Wengine ni Anne Lauvergeon, Ofisa Mwendeshaji Mkuu makampuni ya AREVA; Kishore Mahbubani (Singapore), Profesa wa Masuala ya Sera; Seneta Sam Nunn (Marekani), Mwenyekiti Mwenza na Mtendaji Mkuu Taasisi ya Nyuklia.

Balozi Karl Theodor Paschke (Ujerumani), Msaidizi Katibu Mkuu wa UN (Huduma za Dharura 1994-1999), alikuwa Mwakilishi wa Kudumu kwenye IAEA (1984-1986); Dk. Wolfgang Schussel (Austria), alikuwa Chansela na Kiongozi wa wabunge wa Chama cha APP; Evgeny Velikhov (Urusi), Rais wa Kituo cha Utafiti cha Kurchatov.

Profesa Wang Dazhong (China), Mwenyekiti wa Heshima wa Baraza la Chuo Kikuu Tsinghua, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Nyuklia (INET) ya Chuo, na Dk. Hiroyuki Yoshikawa (Japan), Rais wa Taasisi ya Taifa ya Maendeleo ya Sayansi ya Viwanda na Teknolojia, Tokyo.

0
No votes yet