Dk. Rashid asirejeshwe Tanesco


Renatus Mkinga's picture

Na Renatus Mkinga - Imechapwa 14 April 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

NIMELAZIMIKA kuandika makala hii baada ya kuona jitihada za makusudi zikifanywa na baadhi ya vyombo vya habari kumpigia debe Dk. Idrissa Rashid kurejeshwa kuongoza Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO).

Dk. Rashid anayepigiwa debe anafahamika. Ni mtaalamu wa benki (Banker) ambaye hana hata chembe ya sifa ya kuogoza Tanesco, hasa kwa kuwa ndani ya Tanesco kuna wataalamu wa kutosha wenye sifa za kuongoza shirika.

Vinginevyo, serikali iseme kuwa inachagua watendaji wakuu wa mashirika ya umma kwa misingi ya uswahiba.

Kwanza, Dk. Rashid si mhandisi kama ilivyokuwa kwa wakurugenzi waliopita: Salvatory Mosha, Simon Mhaville na Baruany Luhanga.

Ni wakati wa uongozi wa wahandisi hawa, miundo mbinu ya Tanesco ilijengwa karibu nchi mzima kwa kufuata sera safi za Baba wa Taifa, Mwalimu Kambarage Nyerere – “Umeme kwanza.”

Hapa ndipo vituo vya kuzalisha umeme vya Kidatu, Mtera, Nyumba ya Mungu, Hale na Pangani vilijengwa. Ni wahandisi hawa waliosambaza nguzo za umeme za megawati 220 KV na 132KV nchi nzima.

Baada ya Nyerere kuna vituo gani vya umeme vilivyoanzishwa zaidi ya serikali kuingiza nchi katika mikataba ya kifisadi kama ule wa IPTL, Songas, Richmond, Dowans na Agrreco?

Pili, katika kipindi chake cha miaka mitatu ndani ya Tanesco, mgao wa umeme ulitangazwa mara sita na kusababisha hasara kwa taifa na wananchi kwa jumla.

Tatu, wakati serikali ilipotangaza zabuni ya kununua mitambo mipya ya kuzalisha umeme ya megawati 160, Tanesco chini ya Dk. Rashid ilishiriki kuvunja sheria za manunuzi ya umma (PPRA), jambo amlao ni utovu wa uadilifu.

Nne, akiwa kiongozi, kulikuwa na mitambo ya megawati 80 iliyokuwa imefungwa Ubungo na Mwanza.

Pamoja na wenye mitambo kuwa tayari kuiuza kwa Tanesco, uongozi chini ya Dk. Rashid ulikataa ombi hilo. Badala yake, ukataka kuagiza mitambo mingine, jambo lililosababisha kampuni za Aggreko na Alstom kung’oa mitambo yao.

Haikuchukua muda, Dk. Rashid akaja na mpango wa kutaka serikali kununua mitambo iliyomng’oa waziri mkuu, Edward Lowassa katika kiti chake – mitambo ya kampuni ya Richmond/Dowans.

Kabla ya kumaliza muda wake Tanesco, Dk. Rashid alikuwa na mpango wa kuleta mitambo mipya itakayowekwa mahali palepale ilipokuwa mitambo ya Aggreko na Alsstom.

Tano, Dk. Rashid ameshindwa kushauri vizuri serikali kutekeleza mpango wa muda mrefu wa kuzalisha umeme kwa kuwa muumini wa ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa dharula.

Kwa mfano, mgodi wa Kiwira mkoani Mbeya una uwezo wa kuzalisha megawati 200 za umeme, lakini serikali haitaki kuwekeza katika mradi huo.

Inataka kununua mtambo wa megawati 100 kwa kile kinachoitwa, “matumizi ya wananchi wa Dar es Salaam.”

Si hivyo tu, wakati mgodi wa Mchuchuma una uwezo wa kuzalisha megawati 400; miradi ya kufua umeme kwa njia ya upepo iliyopo Singida na Makambako ina uwezo wa kuzalisha megawati 100, serikali inaendelea kuota umeme wa Richmond/ Dowans.

Kama hiyo haitoshi, wakati mradi wa Rusumo, mkoani Kagera una uwezo wa kuzalisha megawati 60, Rumakali na Ruhuji megawati 400, Tanesco chini ya Dk. Rashid imeendelea na porojo za kumaliza tatizo la uhaba wa umeme mkoani Mwanza.

Mpango huo si kutafuta vyanzo vipya vya umeme; inataka kununua mtambo wa megawati 60 za kuzalisha umeme wa dharula.

Sita, chini ya Dk. Rashid Tanesco iliingia katika kashifa baada ya kuruhusu mamilioni ya shilingi kutumika kukarabati nyumba saba za shirika ikiwamo nyumba yake.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) inaonyesha kuwa ukarabati wa nyumba hizo ulitumia zaidi ya Sh. 1 .807 bilioni ambapo Sh. 681 ziliidhinishwa na bodi ya wakurugenzi na zilizobaki Sh. 1.2 bilioni zilitumika bila idhini ya bodi.

Nyumba anayoishi Dk. Rashid, iliyopo kitalu Na. 13 Chaza Lane, Oysterbay imekarabatiwa kwa Sh. 614 milioni; ameweka mapazia ya 17.3 milioni; amenunulia jenereta lenye ukubwa wa KV 59.2 linalotosha kuendesha kiwanda; ametengeza bustani kwa Sh. 12 milioni na ametumia Sh. 49 milioni kuweka maua ya plastiki.

Saba, ni Rashid aliyeingiza Tanesco katika mgogoro wa kiuchimi baada ya kuajiri zaidi ya wafanyakazi 600 ambao wamerundikwa makao makuu ya Tanesco wakiwa hawana kazi za kufanya.

Wakati Rashid anachukua uamuzi huo, ofisi za mikoa na wilaya zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafundi, magari na vitendea kazi.

Nane, utafiti uliofanywa wakati Dk. Rashid akiwa kiongozi unaonyesha kuwa Tanesco ndilo shirika linaloongoza kwa rushwa hapa nchini.

Hili linatokea wakati yeye mwenyewe tayari ametajwa kuhusika katika rushwa iliyohusisha ununuzi wa rada.

Nane, Tanesco imebebeshwa mzigo wa kuhudumia mwenyekiti wake wa Bodi, Peter Ngumbullu tangu alipoteuliwa mwishoni mwa mwaka 2008 kutokana na afya yake kuwa si mzuri.

Taarifa zinasema kwamba jukumu la kumtibu Ngumbullu nchini India linafanywa na Tanesco kwa maagizo ya Rashid, jambo ambalo limechangia kuzorotesha shughuli za shirika.

Tisa, Dk. Rashid ametumia Sh. 2 bilioni miezi michache tu kabla ya kuachia ngazi kununua magari ya shirika.

Wafanyakazi ndani ya shirika wanalalamika kuwa Dk. Rashid hakupaswa kununua magari ya bei mbaya – karibu sh. 200 milioni kwa kila gari - wakati wakurugenzi walionununuliwa magari tayari walikuwa na magari mengine.

Hivyo basi, kwa kuwa Tanesco si kampuni binafsi, haipaswi kurudishwa mikononi mwa Rashid.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: