Dk. Rashid aumbuka


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version
Dk. Idris Rashidi

UCHUNGUZI wa matumizi mabaya ya fedha katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) umemuumbua Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Idris Rashidi.

Miongoni mwa mambo ambayo yamegundulika ni matumizi ya jenereta katika nyumba ya Dk. Rashidi, ambalo ni kubwa kwa uwezo kuliko lile linalotumiwa na jengo zima la Wizara ya Nishati na Madini lenye ghorofa 11.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anasema TANESCO haikuwa makini kuwatumia wataalamu wake wa umeme kwani ilifunga jenereta kubwa katika nyumba ya Dk. Rashidi.

Jenereta ndani ya nyumba ya Dk. Rashidi ni la KVA 59.2 wakati lile lililoko kwenye wizara ni KVA 25 tu. CAG anasema jenerata hilo ni kubwa mno kwa nyumba ya kulala.

Anasema jenereta la KVA 15 lingetosha kwa nyumba hiyo na kuokoa gharama kubwa ya shirika.

Ni CAG aliyethibitisha matumizi mabaya ya Sh. 1,411,986,390 zilizotumika kukarabati nyumba saba za vigogo wa TANESCO, ikiwamo ya Dk. Rashidi. Zote ziko Dar es Salaam.

Sh. 600,000,000 zilitumika kukarabati nyumba anayokaa Dk. Rashidi wakati Sh. 250,463,140 zilitumika kukarabati nyumba Na. 89 ya kigogo mwingine wa shirika hilo, iliyopo barabara ya Guinea.

Shilingi 190,407,430 zilitumika kukarabati nyumba Na. 65 iliyoko barabara ya Laibon wakati nyumba Na. 459 iliyoko barabara ya Mawezi iligharimu Sh. 130,000,000.

Nyumba Na. 93 iliyopo barabara ya Guinea iligharimu Sh. 88,515,820; Na. 315 iliyoko mtaa wa Toure iligharimu Sh. 79,000,000 na Na. 98 iliyoko mtaa wa Uganda iligharimu Sh. 73,600,000.

CAG amebaini kuwa kutokana na ukarabati wa nyumba hizo saba kuchelewa kukamilika, TANESCO ilipata hasara ya Sh. 22,800,000. Fedha hizo zilitumika kulipia posho za wakurugenzi saba wa shirika hilo, ambao walipangiwa kukaa kwenye nyumba hizo. Kila mkurugenzi alikuwa akilipwa Sh. 800,000 kwa mwezi.

Uchunguzi umebaini kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi ya Umma na usimamizi mbaya wa mikataba ya ukarabati wa nyumba hizo.

Ripoti hiyo ya CAG kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Peter Ngumbulu, iliyowasilishwa mwishoni mwa Oktoba, 2009, imetoa lawama moja kwa moja kwa Dk. Rashidi na timu yake kwa usimamizi mbovu.

“TANESCO ina matatizo makubwa ya usimamizi wa mikataba na hapa wa kulaumiwa ni Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Rashidi.

“Menejimenti ya TANESCO imekuwa ikifanya maamuzi mengi bila kuihusisha bodi ya wakurugenzi au Wizara ya Nishati na Madini, ambao wangeshauri na kutoa mwongozo mzuri,” inasema ripoti ya CAG.

Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ilimwomba CAG kufanya uchunguzi baada ya mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, kuelezea bungeni, wakati akijadili matumizi ya fedha ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2009/2010, kuwa shirika hilo lilitumia zaidi ya Sh. 1.4 billioni kukarabati nyumba zake saba, wakati lina matatizo makubwa ya kifedha.

CAG ameridhika kuwa madai yote yaliyotolewa bungeni na Ndassa yalikuwa ya kweli na kwamba menejimenti chini ya Dk. Rashidi ilikiuka taratibu zote za ukarabati wa nyumba hizo.

Ripoti ya awali ya CAG imesema ilishindwa kukamilisha kazi yake kwa muda wa wiki tatu zilizopangwa, kuanzia  19 Agosti 2009 hadi  9 Septemba 2009, kwa sababu menejimenti ya TANESCO ilishindwa kukabidhi nyaraka zilizohitajika kwenye uchunguzi huo.

CAG anasema ingawa Bodi ya Wakurugenzi iliidhinisha Sh. 681,504,000 tu katika bajeti ya shirika ya mwaka 2007 na 2008 kwa ajili ya ukarabati wa nyumba hizo, hadi kufikia mwishoni mwa Septemba 2009, tayari Sh. 982,217,975 zilikwishatumika kuwalipa makandarasi. Hii ina maana Sh. 300,713,917 hazikuwa zimeidhinishwa na Bodi.

Kibaya zaidi ni kuwa ikichukuliwa mikataba yote ya nyumba unapata jumla ni Sh. 1,807,050,969 kwa maana kuwa fedha zikilipwa zile ambazo hazijaidhinishwa na Bodi ni Sh. 1,125,546,969.

Lakini pia CAG anawalaumu Dk. Rashidi na wenzake kuwa ingawa ankara za kiasi cha mahitaji (bills of quantities) zilitayarishwa wakati wa kukaribisha zabuni, lakini nyingi hazikuwa sahihi na ndiyo sababu kazi nyingine nyingi za nyongeza zilijitokeza. Uchunguzi umeonyesha zaidi ya Sh. 500 milioni zitatumika kulipia kazi za nyongeza.

“Matokeo yake gharama za ukarabati kutokana na kazi za nyongeza zilikwenda juu na wakati wote Dk. Rashidi, kama Mkurugenzi Mtendaji, alishindwa kukemea hilo kwa sababu na yeye alihusika kusababisha ongezeko kubwa la gharama za nyumba aliyopanga kuingia.

“Menejimenti ya TANESCO ilikiuka sera ya shirika inayoweka wazi kuwa kampuni itawajibika kwa matengenezo na ukarabati wa nyumba zake na si wafanyakazi wanaotarajiwa kuingia kwenye nyumba hizo,” ripoti inasema.

Sera hiyo haikufuatwa. Maofisa waliopangiwa kukaa kwenye nyumba hizo walitoa maagizo, kama ya kuongeza idadi ya vyumba na hata kujenga viwanja vya michezo.

Ripoti ya CAG pia imebaini kuwa kandarasi zote za nyumba hizo saba hazikuwa na vielelezo vya kutosha, bali maelezo ya juujuu ya kazi za ukarabati unaohitajika kufanyika.

Utaratibu wa kuidhinisha utekelezaji wa kazi za ziada haukufuatwa, na mfano mmojawapo ni kukosekana kwa idhini ya bodi ya zabuni ya TANESCO kabla ya kazi hizo kuanza.

Uchunguzi pia unaonyesha kuwa utafutaji wa mkandarasi aliyekarabati nyumba ya kukaa Dk. Rashidi, iliyoko Mtaa wa Chaza Lane, Na.13, na ununuzi wa jenereta kubwa kwenye nyumba hiyo, haukufuata sheria ya manunuzi ya umma.

Aidha, mkandarasi aliyekarabati nyumba hiyo alianza kazi bila kupewa kibali cha bodi ya zabuni ya TANESCO.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: