Dk. Rashid, TANESCO na Dowans: Ndoa iliyoshindikana alfajiri


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 11 March 2009

Printer-friendly version
Makao Makuu TANESCO

KWA mara nyingine, serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) imetangaza kujitoa katika mipango ya kununua mitambo ya kampuni ya Dowans Holding (Tanzania) Limited.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashid amesema TANESCO imejiondoa katika mchakato wa ununuzi wa mitambo ya Dowans kutokana na kile alichoita, “Masuala ya msingi ya taaluma ya ufundi kumezwa na wanasiasa.”

Dk. Rashid alitoa kauli hiyo Ijumaa iliyopita, mjini Dar es Salaam katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Hii si mara ya kwanza kwa TANESCO kusema imejiondoa katika mjadala wa Dowans. Mwishoni mwa mwaka jana, TANESCO ilitangaza kujiondoa katika zabuni ya kuwania mitambo ya Dowans baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kushauri kufanya hivyo.

Uamuzi wa TANESCO unaweza kuwa ni hitimisho la mjadala uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa uliohusu “sakata” la Richmond na Dowans.

Kauli ya Dk. Rashid imekuja siku moja baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta kutahadharisha serikali kuhusu uamuzi wowote wa kununua mitambo ya Dowans.

Sitta alisema uamuzi wa Bunge ni serikali kuvunja mkataba na Dowans na si vinginevyo. Ametaka serikali kuagiza mitambo yake, badala ya kung’ang’ania ile ya Dowans.

Lakini ukifuatilia kwa makini, utagundua kwamba Dk. Rashid amethibitisha mwenyewe kwamba, ama ameshindwa kazi au anachokitenda kinatofautiana na kile anachokisema.

Aidha, kwa kauli hii inaonekana dhahiri kwamba Dk. Rashid hawezi kuaminika tena. Ameshindwa kusimamia kile anachokiamini.

Katika hali ambayo haikutarajiwa, katika mkutano wake na waandishi wa habari Dk. Rashid ameshindwa hata kutoa ufafanuzi wa msingi wa hoja ya TANESCO ya kutaka kununua mitambo ya Dowans.

Ameshindwa kusema porojo za wanasiasa zinaweza vipi kusukumiza nje ya mstari hoja za kitaalam hasa za mtaalam kama yeye.

Badala yake, anaishia kutoa tishio. Kwamba “asilaumiwe kwa yatakayotokea huko mbele.” Hiki ni kitisho kingine. Kitisho kinapata nguvu zaidi hasa pale Dk. Rashid anaposhindwa kukifafanua.

Kwa wanaomfahamu Dk. Rashid hawashangazwi na ndimi mbili zake na tabia ya kuamrisha vitu bila kufanya utafiti. Anasifika kwa sifa hizo mbili. Mifano ni mingi.

Kwanza, mara baada ya kuteuliwa kuwa mtendaji mkuu wa TANESCO, aliamua kuwanyang’anya wakurugenzi na mameneja wa TANESCO magari ya shirika kwa madai kwamba yanaongeza matumizi.

Badala yake alitaka watumie magari yao binafsi, huku shirika likigharamia mafuta. Hakufanya utafiti na wala hakushirikisha wenzake katika uamuzi huo. Matokeo yake zoezi zima limekwenda kombo.

Mameneja na wakurugenzi wanatumia magari yao binafsi wanapokuja kazini, lakini wanapokuwa kazini wanatumia magari ya shirika. Hali hiyo imefanya gharama kuongezeka maradufu.

Pili, ni Dk. Rashid aliyeamrisha kukatwa umeme katika Kiwanda cha Saruji cha Tanga. Kabla ya kuchukua hatua hiyo, kuna taarifa za uhakika kwamba aliombwa kutofanya hivyo na Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO wakati huo, Balozi Fulgence Kazaura, na hata aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.

Balozi Kazaura alitaka TANESCO irejeshe umeme kwa maslahi ya taifa na kuagiza mgogoro kati ya kiwanda cha Tanga Cement na TANESCO utatuliwe kwa njia ya mazungumzo. Hakufanya hivyo. Badala yake alitishia kujiuzulu.

Kilichosisitizwa na Balozi Kazaura kuwa ni kwa maslahi ya taifa, kilipuuzwa na Dk. Rashid. Lakini ni yeye ambaye sasa anasema, “Kununua mitambo ya Dowans ni kuangalia maslahi ya taifa.”

Bila shaka, Dk. Rashid anasahau kwamba miongoni mwa viwanda ambavyo anasema vitakosa umeme kutokana na uhaba wa nishati hiyo, tayari kilinyimwa umeme kwa siku kadhaa kutokana na amri zake.

Tatu, mara baada ya kuteuliwa kuwa mtendaji mkuu wa shirika, Dk. Rashid aliitisha mkutano na wafanyakazi wote wa Tanasco makao makuu ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani – Ilala, Temeke, Kinodoni Kusini, Kinondoni Kaskazini na Kibaha.

Katika mkutano huo, Dk. Rashid aliwambia wafanyakazi kwamba makao makuu ya TANESCO yana wafanyakazi wengi na kwamba wengi hawana kazi za kufanya.

Aliahidi kuunda ofisi za kanda na kuwapeleka huko, pamoja na kuimarisha ofisi za wilaya na mikoa.

Lakini katika hali ambayo ni Dk. Rashid mwenyewe anayeweza kuisemea, hivi sasa makao makuu ya TANESCO yana mlundikano wa wafanyakazi baada ya uongozi wake kuajiri wafanyakazi wapya zaidi ya 700.

Hadi sasa, waliopunguzwa au kuhamishiwa mikoani hawazidi 100. Ni wazi kwamba alitangaza uamuzi huo bila kufanya utafiti na bila kushirikisha wenzake.

Nne, Novemba mwaka jana, akiwa katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TANESCO, Dk. Rashid alitoa ripoti iliyoonyesha kuwapo kwa matumaini makubwa ya uzalishaji wa umeme nchini.

Ni katika ripoti hiyo, iliyoitwa “Ripoti ya Mwaka 2009,” uongozi wa TANESCO ulioyesha kwamba mwaka 2009 hali ya upatikanaji umeme itakuwa nzuri. Alisema kuongezeka kwa uzalishaji hakutaathiri upatikanaji wa umeme.

Akiongea kwa kujiamini, Dk. Rashid alisema hali hiyo inatokana na maji kujaa katika mabwawa ya Mtera, Kidatu na Nyumba ya Mungu. Aliwambia wafanyakazi pia kwamba shirika limekopa Sh. 285 bilioni kutoka mabenki mbalimbali yanayoongozwa na benki ya Stanbic.

Kwamba fedha hizo zinatumika kununua umeme kutoka makampuni binafsi kama vile Songas. Lakini leo ikiwa hata mate hayajakauka, Dk. Rashid anakuja na kisingizio cha mabwawa kukauka na mahitaji kuongezeka.

Wala Dk. Rashid hajasema fedha zilizokopwa na serikali katika mabenki ya nje zimetumikaje? Au ndiyo hizo anazotaka kuzinunulia Dowans? Kama ni hizo, mbona hakusema katika taarifa yake kwa wafanyakazi kwamba “fedha zilizokopwa zinatumika kununulia mitambo ya Dowans?”

Tano, tarehe 1 Agosti 2008, Dk. Rashid aliitisha mkutano wa waandishi wa habari, ambapo pamoja na mambo mengine alisema kuvunjwa kwa mkataba wa Dowans na serikali hakutaleta madhara kwenye upatikanaji wa umeme.

Kwa kujiamini alisema, “La hasha! Kwanza, hatuhitaji umeme wao (Dowans), tunao mwingi.” Akasema, “kuna mitambo ya megawati 100 ya Ubungo (ex-Wartsila) itakayozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni.”

Leo, ni Dk. Rashid yuleyule anayelilia Dowans kwa hoja dhaifu ya “Taifa kutumbukia kwenye giza,” kama kwamba taifa lote linamulikwa na TANESCO.

Aidha, tarehe 6 Januari 2009 Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliwaambia waandishi wa habari kwamba hatua ya serikali kusitisha mkataba wake na Dowans kumeipunguzia mzigo TANESCO wa kukodi mitambo hiyo.

Ngeleja alikuwa akizungumza na wanahabari katika kile alichokiita, “Kueleza mafanikio ya wizara yake.” Katika mkutano wake huo, waziri Ngeleja alisema taifa na TANESCO watapata ahueni kwa kutolipa gharama za kila siku za “Capacity charge kwa kampuni hiyo.”

Ngeleja hakusema kwamba kujiondoa kwa serikali katika mkataba wa Dowans kutaifanya TANESCO ishindwe kutimiza wajibu wake wa kuwapa wananchi umeme.

Hakusema hivyo. Si kwa sababu hakujua kwamba kuna tatizo, bali ni kwamba tatizo la sasa linaloimbwa na Dk. Rashid ni la kuchonga.

Tarehe 25 Oktoba 2008, Dk. Rashid alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuelezea upatikanaji wa umeme kwenye gridi ya taifa.

Katika kifungu cha nne cha mkakati wake wa kulinasua taifa na upugufu wa umeme, Dk. Rashid hakutaja hata chembe suala la ununuzi wa mitambo ya Dowans.

Badala yake, “mtaalamu” Dk. Rashid, alizungumzia umuhimu wa mradi wa umeme wa Kiwira, mkoani Mbeya ili uzalishe megawati 200 ifikapo mwaka 2010.

Aliwambia Watanzania kwamba TANESCO itajitahidi kukamilisha mipango ya uzalishaji umeme wa megawati 100 pale kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ili kuliokoa taifa na mgao wa umeme.

Alikumbushia kesi ya IPTL iliyofunguliwa katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ambayo alisema inaifanya TANESCO isizalishe umeme.

Kuna madai kwamba Bodi ya TANESCO inayoongozwa na Peter Ngumbulu ilikataa kupitisha ununuzi wa mitambo ya Dowans kwa sababu haikuwapo katika mipango ya awali.

Pamoja na kwamba madai haya bado hayajathibitishwa, lakini kuna ushahidi wa kutosha kuwa yana ukweli ndani yake. Na hili linapata nguvu zaidi baada ya Bodi ya TANESCO kuamua kukaa kimya na kuliacha “kasheshe lote hili” kwa Dk. Rashid mwenyewe.

Tarehe 5 Novemba 2008 Rais Jakaya Kikwete alizindua mitambo ya megawati 102.4 ya TANESCO iliyopo Ubungo.

Ni katika ufunguzi huo, Kikwete alimueleza waziri Ngeleja kwamba ahakikishe mitambo ya IPTL inageuzwa kutoka matumizi ya mafuta kwenda gesi asilia ili kupunguza gharama zikiwamo gharama za Capacity charge.

Rais alisema anataka kesho na kesho kutwa kusiwepo visingizio vya kukosekana kwa umeme kutokana na mitambo ya IPTL.

Si Dk. Rashid wala Ngeleja ambaye amesema agizo hili la rais wamelifanyia kazi kwa kiwango gani. Au ndiyo sababu Dk. Rashid hajazungumzia, katika mipango yake, mitambo ya IPTL?

Bali, Dk. Rashid anang’ang’ana kwamba “Hali ya maji katika mabwawa ya TANESCO haitarajiwi kuwa nzuri.” Lakini ni siku hiyohiyo, mkuu wa Idara ya Hali ya Hewa (MET) alitangaza kuwa mabwawa ya umeme yatapata maji ya kutosha katika miezi michache ijayo.

Je, kauli ya Dk. Rashid haikusudii kukataa moja kwa moja taarifa ya MET kwa lengo la kuhalalisha mipango yake ya kununua Dowans?

Kama hivyo sivyo, kwa nini Dk. Rashid anataka serikali inunue mitambo ya Richmond/Dowans, badala ya ile ya Aggreko ya megawati 40 na ambayo mkataba wake hauna utata kama huu wa Dowans?

Vilevile, kwa msingi na moyo ule anaoita wa “uzalendo,” kwa nchi yake na watu wake, kwa nini Dk. Rashid asishawishi serikali kununua mitambo ya Alston ya megawati 40 iliyopo mjini Mwanza na ambayo ipo katika hali nzuri?

Kwa nini TANESCO ya Dk. Rashid inafanya ubaguzi wa kiwango kikubwa kama hiki?

Ni kitu gani hapa ambacho Dk. Rashid ameahidiwa na Dowans na ambacho hakika, hataki kukitaja, au kukisema?

Ni wazi kwamba TANESCO inaendeshwa kienyeji. Hakuna mipango ya muda mfupi, kati na muda mrefu. Wanaganga lililopo wakati uliopo. Hakika huo siyo uongozi unaotakiwa ndani ya shirika nyeti la umma.

Inahitajika TANESCO inayoongozwa na wataalam wenye upeo na wenye uwezo wa kufanya kazi kwa maslahi ya nchi. Wataalam wanaotengeneza mipango inayoendana na hali inayotegemewa kutokea.

Lakini kwa hali ilivyo sasa, hakuna atakayeshangaa iwapo leo au kesho atasikia Dk. Rashid amejiuzulu. Kwanza amefikia ukomo wa uwezo wake, wakati TANESCO inadai uwezo mkubwa zaidi wa ubunifu na menejimenti.

Lakini pili, serikali, TANESCO na Dowans ni “ndoa ya utatu” iliyoshindikana alfajiri; hadi mmoja akubali kuwa mshenga na siyo mchumba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: