Dk. Shein kuzua utata


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly version
Dk. Ali Mohammed Shein

UTEUZI wa Dk. Ali Mohammed Shein kuwa mgombea urais Zanzibar huenda ukazua utata, MwanaHALISI limeelezwa.

Dalili za utata zilianzia kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma, Ijumaa iliyopita wakati mjumbe mmoja alipotaka Dk. Shein aondoe jina lake kwa madai kuwa amekosa sifa za kugombea urais Visiwani.

Mjumbe aliyewasilisha hoja ya Dk. Shein kuondoa jina lake ametajwa kuwa ni Nimrod Mkono, mbunge wa Musoma Vijijini ambaye pia ni wakili wa mahakama kuu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 26 (2), sifa za kuchaguliwa kuwa rais ni pamoja na kuwa Mzanzibari wa kuzaliwa na aliyetimiza umri wa miaka 40.

Sifa nyingine ni kuwa na “sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi; na mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa kilichosajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya 1992.”

Lakini katika eneo la haki ya kupiga kura, kuna sharti la nyongeza ambalo ndilo linaonekana kuangaliwa zaidi na wapinzani wa Dk. Shein kuwa mgombea urais Zanzibar.

Ibara ya 7 kifungu kidogo cha 2(d) inasema Mzanzibari aweza kuzuiwa kutumia haki ya kupiga kura kutokana na “kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpigakura.”

Katika eneo hili, hoja ni kushindwa kujiandikisha katika daftari la wapigakura Zanzibar. Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa Dk. Shein alijiandikisha Oyster Bay, Dar es Salaam na siyo Zanzibar.

Sifa ya kujiandikisha inajitokeza pia katika Sehemu ya Tatu inayohusu, pamoja na mengine, Baraza la mawaziri.

Ibara ya 68(b) kuhusu sifa za kuchaguliwa chini ya eneo hili inasema anayechaguliwa sharti “awe amejiandikisha au ana sifa za kujiandikisha katika jimbo la uchaguzi kama mpigakura katika uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi.
Eneo hili pia linamgusa Dk. Shein ambaye anadaiwa kutokuwa “mkazi” wa Zanzibar “kwa zaidi ya miaka saba sasa.”

Kwa mujibu wa kanuni za kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura, sharti mtu awe Mzanzibari mkazi na kuwa na hati inayothibitisha hivyo.

Wanaopinga uteuzi wa Dk. Shein wanadai kuwa ana hati ya ukazi Zanzibar anayodaiwa pia kukabidhiwa hadharani, lakini hakuitumia kujiandikisha kupiga kura Visiwani.

Kwa mujibu wa taratibu za kupata hati ya ukazi, kila Mzanzibari ambaye amekuwa nchini kwa miaka mitatu mfululizo, anastahili kupewa hati hiyo. Awali sharti lilikuwa miaka mitano.

Wakili mmoja wa mahakama kuu mjini Dodoma ameliambia MwanaHALISI, “Sijaelewa vema hoja za pande zote mbili, lakini jambo moja kuu ni kwamba ili kupiga kura, sharti uwe umejiandikisha.”

“Kama Dk. Shein hakujiandikisha basi hana sifa ya kupiga kura,” amesema. Kwa mujibu wa katiba, “Zanzibar itahesabika kuwa ni jimbo moja.”

Hili linafafanuliwa kwa maelezo kuwa aliyejiandikisha kupiga kura katika kumchagua mjumbe wa baraza la wawakilishi atakuwa na uwezo wa kupiga kura katika uchaguzi wa rais katika jimbo hilohilo moja.

Katika katiba ya Zanzibar hakuna panapoonyesha kuruhusu kuhamisha hati ya kupiga kura kutoka upande mmoja wa Muungano kwenda upande mwingine.

Katika mazingira haya, wapinzani wa Dk. Shein wanasema hawezi kujipigia kura na hawezi kupigia yeyote katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuwa anabanwa na sheria.

Aidha, Dk. Shein hana uwezekano wa kuandikishwa kwa sasa kwa kuwa zoezi la kuandikisha wapigakura tayari limefungwa kwa pande zote mbili za Muungano.

“Hatua ya kuruhusu mgombea urais kujiandikisha wakati zoezi limekwishafungwa, itatafsiriwa kuwa ubaguzi; jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano,” ameeleza wakili.

Hoja ya Dk. Shein kuwa au kutokuwa na sifa ilichukua muda kujadiliwa ndani ya NEC. Ilikuwa baada ya Mkono kulitupa uwanjani, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Andrew Chenge aliidaka na kumtetea mteuliwa.

Chenge ambaye amekuja kujulikana zaidi kwa jina la “mzee wa vijisenti,” alitumia hoja ya Ibara ya 26(2)(c) inayosema mgombea awe na “sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi” na mwanachama aliyeteuliwa na chama chake.

Awali Mkono alishauri Dk. Shein kuondoa jina lake ili kukiepusha chama kukumbwa na fedheha. Alisema kwa mujibu wa Katiba, mtu mwenye sifa ya kugombea urais Zanzibar lazima awe na sifa ya kuchagua mwakilishi au kugombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, hoja ya Chenge ilipokewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete aliyechukua muda mrefu kufafanua moyo wa katiba ya Zanzibar, akisema kuwa alichokuwa akitumia ni “tafsiri ya kisheria.”

Iwapo Dk. Shein ataweza kuchaguliwa kuwa rais wa Zanzibar, atakuwa rais wa kwanza nchini kuchaguliwa bila yeye kujipigia kura.

Kawaida, vyombo vya habari duniani, katika nchi za kidemokrasi zinazotumia uchaguzi, huwafuata viongozi wanaowania nafasi za juu kupata ushahidi wa wao kujipigia kura, ikiwa kielelezo cha kuonyesha umma umuhimu wa kutumia haki yao kuchagua wanayemtaka.

Kwa upande mwingine, taarifa kutoka ndani na nje ya vikao vya CCM zimeeleza kuwa kushindwa kwa Dk. Mohammed Gharib Bilal kuwa mgombea Zanzibar kulitokana na kuungwa kwake mkono na baadhi ya viongozi bara.

Wanaotajwa kumkosesha kura ni Edward Lowassa na Rostam Aziz ambao wanadaiwa kufanya kampeni kubwa ya “kumwingiza madarakani na kutangaza kuwa tayari wamemaliza kazi.”

Lowassa alikuwa waziri mkuu hadi miaka miwili iliyopita. Alijiuzulu kutokana na kashfa ya mkataba wa umeme ya Richmond.

Rostam ni mbunge wa Igunga anayetuhumiwa kushiriki ufisadi katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Taarifa zinadai kuwa Rostam alikuwa akitoa kauli zilizoonyesha kuwa ameongoza kambi ya kumjenga Dk. Bilal kuwa mgombea na hatimaye rais wa Zanzibar.

MwanaHALISI limefahamishwa kuwa Rostam aliwaambia baadhi ya wajumbe wa NEC, “…It is too late (mmechelewa)… na usiku huu mheshimiwa Dk. Bilal atatangazwa mgombea urais wa Zanzibar, na miezi michache ijayo atatangazwa kuwa rais.”

Inadaiwa washirika hao wawili walikaririwa wakieleza wafuasi wao kwamba kambi yao huwa haishindwi kimikakati na katika suala hilo, “Dk. Bilal lazima atakuwa rais wa Zanzibar.”

Taarifa zinaeleza akina Lowassa na Rostam walikuwa wakieleza kuwa tayari wamepata wajumbe 112 kwa upande wa Bilal na kwamba hakukuwa na woga wa kushindwa.

Mmoja wa wana-CCM waliopewa taarifa hizo amedai kuwa taarifa zilivujishwa kwa Rais Kikwete lakini haikuelezwa alichukua hatua zipi.

Katika hatua nyingine, mjumbe mmoja wa mkoani Tabora alilalamikia mwenendo wa Rais Kikwete na kuhoji, “Mbona Kamati Kuu inatulazimisha kuchagua mgombea hapa.”

Hiyo ilikuwa baada ya kubaini kuwa kauli za Kikwete zilikuwa elekezi; zikionyesha kuwa alikuwa anapendelea Dk. Shein.

Mtoa taarifa, hata hivyo, ameeleza kuwa hoja hiyo ilijibiwa na Kikwete kwa kusema “Kamati Kuu imeleta wagombea watatu.”

Katika kinyang’anyiro hicho Dk. Shein alipata kura 117, Bilal kura 54 na Shamsi Vuai Nahodha kuambulia 33.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: