Dk. Shein na serikali ya ‘mapinduzi daima’


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

JANA, tarehe 8 Februari, 2011, ilikuwa siku ya 100 tangu Dk. Ali Mohamed Shein aingie madarakani visiwani Zanzibar.

Aliapishwa 3 Novemba 2010 kuwa rais wa Zanzibar, baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba 2010.

Katika moja ya kauli nzito ambazo Dk. Shein amezitoa hivi karibuni, amesema vyombo vya habari vinakosea kuiita serikali anayoiongoza.

Anasema yeye anaongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na siyo serikali ya umoja wa kitaifa. Anafafanua kwamba serikali ya mapinduzi Zanzibar, ile iliyoundwa kufuatia mapinduzi ya 12 Januari, 1964, ipo palepale.

Serikali hiyo haijafa pamoja na ukweli kwamba sasa inaendeshwa kwa mfumo mpya wa ushirikiano wa vyama viwili vya siasa – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).

Vyama hivyo ndivyo vilivyopata uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa kupigiwa kura zilizofikia asilimia 10.

Dk. Shein aliwaambia wanachama wa CCM wa matawi mawili aliyoyafungua wiki iliyopita katika moja ya hafla za maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa chama hicho, kuwa anaongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa.

Miezi miwili nyuma, Dk. Shein alitumia muda mwingi kueleza kwamba yeye ndiye rais. Ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ingawa anao makamu wawili wanaomshauri.

Alisema katika matamshi yaliyofurahisha mno wana-CCM kwamba anaamua anavyotaka au ana hiari yake kuamua baada ya kushauriwa na wasaidizi wake hao.

Hapo tu ilionyesha dhahiri kuna tatizo upande wake. Ilisemekana kuwa alitoa kauli hiyo kutokana na manung’uniko yaliyokuwa yakitolewa na wanachama wa CCM waliohisi alikuwa anazidiwa kauli katika maamuzi anayoyafanya.

Wana CCM, hasa wakongwe na makada waliojengeka kisiasa hata kujionyesha ni watu wasiopenda mabadiliko, hawakupendezewa na walichokuwa wakisikia kinatokea pale Dk. Shein anapokaa na wasaidizi wake hao kwa mashauriano.

Haieleweki kama ni kweli walichokuwa wakikisikia. Binafsi sijapata kusikia kwamba Dk. Shein amekuwa akitawaliwa kimawazo na Maalim Seif Shariff Hamad, katibu mkuu wa CUF na mshindani mkuu wa Dk. Shein katika wadhifa wa urais wakati wa uchaguzi.

Wana CCM hao hawakuwa na tatizo na kuwepo kwa Makamu wa Rais wa Pili, Balozi Seif Ali Idi. Tatizo lao kubwa, kwa namna simulizi zilivyokuwa, ni Maalim Seif.

Kwa hivyo, kauli ya Dk. Shein ilikuwa ya kuwatoa hofu wenzake katika mawazo hasi waliyokuwa nayo. Inaonyesha hofu yao haijafutika sawasawa maana Dk. Shein ameendelea kutoa kauli inayofanana.

Kauli yake inaonekana kama mpya. Lakini mantiki yake ni ileile ya kutoa hofu wana CCM wanaodhani kwa kuitwa serikali ya umoja wa kitaifa, na hasa kama vile alivyopata kusisitiza Maalim Seif katika moja ya mikutano yake – kwamba iitwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar – basi ile ya mapinduzi imefutwa.

Nimeanza na kuelezea hili kwa sababu kubwa moja: Napata hofu kwamba muda mwingi katika siku hizi mia za uongozi wa Dk. Shein umetumika kujaribu kujenga mazingira ya kubaki na uongozi wenye mtizamo wa “kimapinduzimapinduzi.”

Wala nisingekuwa na tatizo na hilo. Wasiwasi wangu ni pale tu ninapoona kwamba utekelezaji wa majukumu ya kiserikali unazingatia zaidi mtizamo wa kisiasa unaoongozwa na utashi wa CCM. Hili ni tatizo.

Ni tatizo zaidi kwa sababu mimi nilidhani pamoja na kuwa Dk. Shein ametokana na CCM, kwa kuwa ndicho kilichomsimamisha kugombea kiti cha urais, ana jukumu la kuwaongoza wananchi wa Unguja na Pemba kwa kuzingatia matumaini yao zaidi kuliko utashi wa chama chake. Ndivyo fikra zangu ziliko.

Kumbe inaonyesha sivyo. Sivyo kwa kuzingatia yanayotokea ndani ya mioyo ya wanachama wa CCM hata kumsukuma rais kutumia muda muhimu kuelezea mambo kwa mitizamo ya siasa za kimapinduzi.

Naiona hasa inanyemelea serikali mpya. Serikali anayoongoza Dk. Shein imepatikana kwa raslimali nyingi za umma kutumika. Kulikuwa na majadiliano ya mitaani, baadaye yakawa ni majadiliano ya ndani ya baraza la wawakilishi. Mwisho ikapigiwa kura ya maoni ili wananchi waamue watakacho.

Baada ya utaratibu huo kukamilika, ukaja uchaguzi mkuu. Hapo ilishaeleweka kuwa mgombea urais atakayeshinda uchaguzi, atalazimika kuunda serikali ya ushirikiano kwa kushirikisha chama kingine au vingine vitakavyokuwa vimepata kura kwa asilimia ile inayotajwa na katiba. Ni kuanzia asilimia 10.

Kwa kuwa ni CUF kilifikia asilimia hiyo na CCM mgombea wake alitangazwa mshindi wa urais, vyama hivyo vikaunda serikali. Hii ndiyo serikali ya umoja wa kitaifa. Ikiitwa kwa kutanguliza au kuongezea maneno serikali ya mapinduzi, ni sawa tu na iitwe hivyo. Mantiki ya serikali yenyewe yanabaki kuwa ni serikali ya ushirikiano wa vyama.

Ni muhimu kutambua kuwa iwapo serikali hii itajielekeza tu kutumikia wananchi kwa kuzingatia utashi wa CCM, siamini kama itatimiza malengo ya kuundwa kwake. Sidhani. Kwanini sidhani?

Sidhani kwa sababu kilichounganisha wananchi waliokuwa wamegawanyika kutokana na siasa chafu zilizopandikiza chuki, hasadi, ubaguzi, ubwana na utwana, na ubinafsi ni maridhiano.

Maridhiano yalifikiwa baada ya viongozi wakuu wa CCM na CUF upande wa Zanzibar kuamua kuacha siasa za hasama na kujenga msingi wa siasa mpya za kuwatumikia watu.

Kulikuwa na siasa za kutumikia vyama na makundi ya watu wachache. Ndio maana kwa miaka mingi ya uhai wake, Zanzibar ilishuhudia maendeleo duni kwa sababu hayakuwa yanatolewa kwa uwiano.

Wapo watu walikuwa wakionekana hawana haki ya utawala. Hawana chao wala lao. Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu waliokuwa wakibezwa, ndio waliokuwa wanazalisha zao lililokuwa tegemeo kubwa zaidi la uchumi wa Zanzibar tangu miaka ya kwanza ya mapinduzi.

Hata fursa za kusoma na za ajira zilikuwa zikitolewa kwa mtizamo wa kibaguzi. Wale walionekana watu baki wasiostahili kunufaika na fursa hizo. Bali wale waliochukuliwa “ndio halali” walipewa hata bila ya kuzingatia sifa.

Kama kila mtu angeamini kwamba zama zile ndio hasa zilizokusudiwa kufutwa na maridhiano yaliyoanzia kwa mawazo ya watu wachache mno na kukomazwa kwa aliyekuwa rais wakati ule, Amani Abeid Karume na Maalim Seif, tusingesikia leo kiongozi anahimiza imani ya mapinduzimapinduzi. Mapinduzi daima.

Nilidhani kwa wakati uliopo, nguvu kubwa zingetumika kutafuta vyanzo vya mapato vitakavyoipatia serikali fedha za kutosha kukidhi matumaini ya watu, ndi ingekuwa dhamira hasa.

Nachelea kwamba muda utaendelea kupotea tukisisitiza "mapinduzi daima" badala ya kutenda yale waliyotarajia wananchi.

0
No votes yet