Dk. Slaa aongoza kura za maoni


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version

MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa anaendelea kupeta katika kura za maoni zilizopigwa katika mitandao mbalimbali nchini, imefahamika.

Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la kila siku la Mwananchi, www.mwananchi.co.tz, hadi juzi Jumatatu saa 3:37 usiku, Dk. Slaa alikuwa akiongoza kwa asilimia 76.8.

Kati ya wasomaji 11,815 waliojitokeza kupiga kura, 9,072 wamemchagua Dk. Slaa kuwa rais.

Upigaji kura kwenye mtandao wa gazeti hilo ulifunguliwa tarehe 12 mwezi huu.

Mshindani mkuu wa Dk. Slaa katika kinyang’anyiro hicho ni Jakaya Kikwete wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye amepata kura 2,073 ambazo ni sawa na asilimia 17.5 ya kura zote.

Wagombea wengine – Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF), Mutamwega Mganhywa wa Tanzania Labour Party na Hashim Rugwe wa NCCR-Mageuzi, wamepata chini ya asilimi 10 ya kura zilizopigwa.

Kwa mujibu wa kura hizo, Lipumba amepata kura 542 ambazo ni sawa na asilimia 4.6, Mutamwega kura 80 ambazo ni sawa na asilimia 0.7 na Rungwe kura 48 sawa na asilimia 0.4.

Katika mtandao mwingine, Jamii Forum (JF), www.jamiiforums.com, Dk. Slaa anaongoza kwa asilimia 68.66. Amepata kura 6,641 kati ya 9,672 zilizopigwa.

Kikwete ambaye anafuatia, ana asilimia 22.20 kwa kupigiwa kura na watu 2,147 wakati Lipumba ana asilimia 2.88 kwa kupigiwa kura na watu 277.

Nalo gazeti la serikali, Daily News liliendesha kura ya maoni ya aina yake kwa kuuliza, “Je, Dk. Slaa atashinda urais?” Hii ilikuwa mwezi uliopita (Septemba).

Katika kura hiyo Dk. Slaa alipata asilima 60.87. Kura zilizosema “hapana” zilikuwa asilimia 28.57. Jumla ya watu 161 walishiriki katika maoni hayo.

Aidha, mtandao wa MwanaHALISI, www.mwanahalisi.co.tz, unaonyesha kuwa hadi juzi Jumatatu saa 12 jioni, watu 3,087 walikuwa wamepigakura na Dk. Slaa alikuwa akiongoza kwa asilimia 87.

Anayemfuatia kwa karibu ni Kikwete mwenye asilimia 8 wakati Lipumba ana asilimia 3. Wagombea wengine wanagawana asilimia moja.

Matokeo haya yanakuja baada ya yale ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (REDET) na Synovate Tanzania Limited.

Redet walionyesha Kikwete akiongoza kwa asilimia 71 wakati Synovate walionyesha akiongoza kwa asilimia 61. Synovate walionyesha pia kuwa Dk. Slaa alipata asilimia16 na Lipumba asilimia tano.

Bali ripoti ya Redet ya Machi mwaka huu inaonyesha Kikwete alikuwa mashuhuri kwa asilimia 77.2.

Kwa maoni ya wengi wanaotumia mitandao, Dk. Slaa anaoangoza kwa mbali. Mara nyingi ni jumuia za mijini ambazo zina nafasi ya kusoma mitandao na kutathmini uwezo wa viongozi kwa kuzingatia uelewa wao na ukomavu wa hoja wanazotetea.

Hata hivyo, CCM waliokubaliana na utafiti wa Redet, wadau mbalimbali walipinga ripoti hiyo wakisema utafiti unapaswa kulaaniwa kwa kuwa ni “mkakati maalumu wa kuijengea CCM mazingira ya ushindi.”

Wapinzani wa utafiti wa Redet wamejenga hoja katika misingi mikuu miwili: Kwanza, ni taasisi iliyo chini ya chuo kikuu kinachomilikiwa na serikali.

Pili, mwenyekiti wake, Profesa Rwekaza Mukandala, ni mteule wa Kikwete katika nafasi yake ya sasa ya makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na rafiki yake wa karibu.

Nyaraka kadhaa ambazo gazeti limenasa, zinaonyesha hata hivyo, kuwa Synovate ina mahusiano ya karibu ya kibiashara na binafsi na ikulu au watumishi wake.

Katika hatua nyingine, taarifa zinasema kuna mpango uliosukwa kusambaza ujumbe wa kumchafua Dk. Slaa na chama chake kwa njia ya simu.

Inaelezwa kwamba ujumbe wa simu ya mkononi (sms) utakaosambazwa utafanana na ule uliosambazwa nchi mzima wiki mbili zilizopita.

Namba za simu ambazo zimekuwa zikiporomosha tuhuma dhidi ya Dk. Slaa, ni Na. +3588976578 na +3588108226.

Taarifa zinasema ujumbe huo wa simu ya mkononi ulitumwa katika mtambo mkuu (Master Switch) wa kampuni ya Vodacom ulioko karibu na ubalozi wa Ufaransa.

Kampuni ya Vodacom inamilikiwa kwa ubia na mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM, Rostam Aziz na Peter Noni, mmoja wa watuhumiwa wakuu wa wizi katika akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa sasa, Noni ni mkurugenzi mkuu wa Benki ya Rasilimali nchini (TIB). Ni benki hii ambamo Rais Kikwete alisema ameweka fedha ambazo zilirejeshwa na waliokiri kuiba kutoka BoT.

Alipouliza Richard Kayombo, mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhusu ujumbe mchafu, alithibitisha kuwa ulitumwa kutoka ndani ya nchi.

Alisema, “Kuna ushahidi usio na shaka kwamba meseji hizo hazijatoka Finland kama namba hizo za simu zinavyoelekeza. Ukitaka kujua kwamba namba hizo si za Finland, ukipiga au kutuma meseji kupitia namba hizo hutapata majibu. Ni kwa sababu, namba hizo hazipo.”

Hata hivyo, Kayombo alisema ipo teknolojia ya kutengeneza namba za simu za uongo kwa kuweka namba unayoitaka. Amesema hiyo ni sawa tu na mtu anayetumia mtandao wa Skype. Anasema wakati kwenye Skype linakuja jina la mhusika, kwenye utaratibu huu inakuja namba.

Alisema mamlaka yake inachunguza chanzo cha meseji hizo na kwamba tayari wametoa “maagizo kwa makampuni yote ya simu nchini kutaka wafanye uchunguzi kujua iwapo meseji hizo zimetoka kwao.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: