Dk. Slaa ataka CCM isiingilie Bunge


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 February 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana

BUNGE limemaliza mkutano wake wa 14 bila kujadili hoja ya Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), kuhusu Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kuingilia mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya taifa. Mwandishi Wetu alifanya mahojiano na Dk. Slaa juu ya hoja yake.

Swali: Hoja yako binafsi bungeni juu ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kuingilia mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya taifa imefikia wapi?

Jibu: Kwa mujibu wa Kanuni 47 na 48 za Bunge, niliwasilisha hoja bungeni chini ya kanuni inayoruhusu hoja ya dharura. Niliamini hoja hiyo ni ya dharura kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, kwa mujibu wa taarifa nilizonazo, waziri Masha amevunja Sheria ya Manunuzi ya Umma, Na. 21 ya mwaka 2004.

Suala la kuvunja sheria ni la dharura na mtu yeyote anayevunja sheria anafikishwa mahali panapostahili; yaani mbele ya vyombo vya dola. Kwa kuwa hilo halikufanyika, basi nilitaka serikali inipe majibu ni kwanini hatua hiyo haikuchukuliwa.

Pili, Sheria za Manunuzi ya Umma  zinataka, iwapo kipengele chochote cha sheria hiyo kimevunjwa, basi kipengele hicho kinashughulikiwa bila kuathiri mchakato wa zabuni; na mimi sikutaka uvurugwe.

Tatu, kwa utaratibu wa kawaida, sheria inapovunjwa, huwezi kusema ngoja kwanza uvunjaji ukamilike ndipo uchukue hatua. Hatua madhubuti zinatakiwa kuchukuliwa palepale, ili kuzuia madhara zaidi.

Hata hivyo, baada ya kuwasilisha hoja yangu chini ya Kanuni ya 47, ambayo kimsingi inataka mbunge kusimama mahali pake na kulianzisha jambo hilo, hoja yangu ilielekezwa na Kamati ya Uongozi kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Nilistushwa sana nilipoona hoja yangu imejadiliwa na Kamati ya Wabunge wa CCM (Caucus) kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la kila siku nchini.

Kikao cha wabunge wa CCM siyo chombo cha kikanuni na iwapo mambo yataendelea hivyo, hakuna sababu ya hoja zetu kuwasilishwa kama zinaweza kufanyiwa maamuzi na kuzimwa na vyombo visivyo vya bunge.

Swali:  Je, Masha aliieleza nini Kamati ya Bunge?

Jibu: Mimi si msemaji wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kimsingi mambo yakiwa ndani ya Kamati bado ni siri isipokuwa pale ambapo kazi za Kamati zimefanyika kwa uwazi kwa mujibu wa Kanuni.

Swali: Kwa maoni yako, Kamati ilitimiza wajibu wake na kutenda haki?

Jibu: Mamlaka ya kuzungumza kama Kamati ilitimiza wajibu wake siyo yangu. Naweza kusema tu kwamba nilistuka kusikia na kusoma kwenye gazeti lalamiko la mjumbe wa Kamati hiyo kuwa "hawajakaa kama Kamati kuamua hatua ya kuchukua" baada ya mimi kuwasilisha hoja yangu.

Iwapo taarifa hii ni ya kweli, basi  nadhani bado tuna kazi kubwa sana ya kujenga demokrasia nchini.

Swali: Kuna taarifa kwamba Masha amekana kuifahamu kampuni ya Sagem Securite anayodaiwa kubeba. Hili likoje? 

Jibu: Nimezungumza kwa kina na Mheshimiwa Masha; naye ametamka hivyo mbele ya Kamati kuwa tumezungumza. Kwa vile mazungumzo yangu naye hayafungwi na Kanuni yeyote, ni kweli kuwa Masha ameniambia, nje ya ukumbi wa Bunge, kuwa “haifahamu” kampuni ya Sagem Securite na kuwa hakuwa na sababu ya kuibeba.

Bali nimestushwa sana na taarifa kwamba Oktoba 2008, kabla hata hajamwandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alikutana na watendaji wa kampuni hiyo nchini Uswisi.

Taarifa zilizochapishwa katika magazeti kadhaa nchini zimetaja hadi namba ya chumba ambacho Masha alikutana na watendaji hao; kwamba walikula chakula cha jioni pamoja, na siku iliyofuata walimwalika ofisini kwao.

Mheshimiwa Masha hajakanusha hayo; hivyo sina sababu ya kuwa na mashaka kuwa alikuwa akiifahamu Sagem Securite. Cha ajabu ni kwa nini ameficha ukweli kwa kusema hakuwa akiifahamu kampuni hadi siku alipopata nyaraka.

Swali: Hayo yanatoa sura gani kwa taifa? Je, hapa Masha hajadanganya bunge na taifa?

Jibu: Suala la Masha kuingilia mchakato lina utata; ndiyo maana nilikuwa ninatoa, katika hoja yangu, pendekezo la kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza utata huo.

Ikumbukwe kuwa mradi wa vitambulisho umechukua muda mrefu sana. Ulipoanza taifa lilishawahi kushitakiwa kwa mchakato huu kutokupelekwa sawa.

Inasemekana Mheshimiwa Masha mwenyewe alikuwa wakili wa upande ulioshitaki serikali, na walioshitaki ndio walishinda kesi.

Swali: Unadhani bado Masha anayo hadhi, sifa na heshima ya kuendelea kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani?

Jibu: Maoni yangu nimekwisha kutoa mara kadhaa; kwamba katika nchi zilizoendelea na zinazoheshimu demokrasia, Masha angekwisha kujiuzulu, kwani amevunja sheria ambazo ameapa kuzilinda.

Tayari Masha amepoteza hadhi ya kuwa Waziri. Isitoshe, majibu yake na taarifa zinazoendelea kutoka zinazidi kuonyesha kuwa hakuwa akisema ukweli. Na hakuna kosa kubwa kama kosa la kiongozi kutokusema ukweli.

Swali: Unasemaje juu ya uamuzi wa Spika wa Bunge kuahirisha hoja yako?

Jibu: Hoja yangu ingekuwa imeahirishwa kwa uamuzi wa Spika, nisingekuwa na tatizo. Nina tatizo kubwa iwapo Spika atakuwa ameahirisha hoja yangu kutokana na shinikizo lililotoka kwa kikao cha chama chake kama ilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari.

Kwa kuwa taarifa hiyo nayo haikukanushwa, ndiyo maana naona kuwa demokrasia yetu bado iko mbichi. Ni jambo la fedheha maamuzi ya kanuni za Bunge kufanyika nje ya vikao vya kanuni.

Iwapo Spika atakuwa kweli ameshauriwa hivyo na Kamati, hilo  nisingekuwa na tatizo nalo. Lakini haiwezi kuwa bahati mbaya kuwa siku Spika anapoahirisha suala langu, gazeti la siku hiyo tayari limekwisha kutangaza kuwa kulikuwa na kikao kilichojadili namna ya kudhibiti hoja ya Dk. Slaa.

Hili ndilo linalonitisha katika mwenendo mzima wa suala hili na demokrasia kwa jumla.

Swali: Kuna taarifa kwamba CCM walijadili hoja yako kwenye vikao vyao vya ndani.

Jibu: Tatizo siyo CCM kulizungumzia jambo hilo kwenye vikao vyao. Hatuwezi kuwapangia agenda ya kuzungumza katika vikao vyao. Tatizo ni pale hoja za kibunge zinapozimwa kwa kutumia vikao vya chama ambavyo havina mamlaka ya kikanuni.

Swali: Kutokana na yaliyotokea, umeamua kuchukua hatua gani?

Jibu: Nitaangalia kama hoja yangu itapangiwa kujadiliwa kwa utaratibu wa kikanuni. Iwapo haitajadiliwa, basi nitatumia busara kujua ni njia gani nitumie kufikisha suala hili kwa wananchi.

Wakati sisi tunacheza siasa, taifa linaathirika vibaya. Ikishindikana basi nitatumia njia zote zilizoko ikiwa ni pamoja na kutumia "Nguvu ya Umma."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: