Dk. Slaa atibua CCM


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 25 August 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Dk. Willibrod Slaa

MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema CCM haijawahi kuwa na ubunifu na uadilifu.

Amesema kwa CCM kuendelea kuwa madarakani ni kukosesha wananchi fursa za maendeleo.

Dk. Slaa amesema pia kuwa CCM haina utashi wa kisiasa na kwamba ndiyo maana kila mwananchi anaona ama taifa limesimama au linarudi nyuma kimaendeleo.

Alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na MwanaHALISI mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam.

Akionyesha udhaifu wa chama tawala kwa miaka mingi, Dk. Slaa alitoa mfano wa kupandisha bei za bidhaa kama bia na soda kila serikali inaposoma bajeti.

“Kila mwaka serikali ya Kikwete imekuwa ikiongeza bei za vyakula na vinywaji, kana kwamba hakuna vyanzo vingine vya mapato. Matokeo yake, wananchi wanashindwa kumudu gharama; na mapato ya serikali ambayo inadai kukusanya hayaonekani,” amesema kwa sauti ya ukali.

Amesema katika nchi zote zenye uchumi mzuri, bidhaa kama bia, soda na maji, huuzwa kwa bei ya chini ili kuwezesha wananchi wengi kumudu na hivyo uzalishaji viwandani kuongezeka na mapato ya serikali kukua pia.

“Kikwete na serikali yake wameshindwa kubuni mbinu mbadala za kuletea wananchi maendeleo. Iwapo wananchi wataichagua CHADEMA, baada ya miaka mitatu tu, taifa lote litakuwa limejitosheleza kwa chakula,” amejigamba.

Amesema atateremsha hata bei za vinywaji ambavyo vimekuwa vikiongezwa bei mwaka hadi mwaka ili wananchi wavifaidi kwa gharama nafuu. “Nitashusha bei za bidhaa hizo,” amesema kwa sauti ya kujiamini.

Mkakati huo wa kuteremsha bei, amesema unalenga wananchi kumudu gharama za maisha na kuongeza mapato ya serikali kwa kuchochea watu wengi zaidi kutumia bidhaa husika.

Katika mazungumzo hayo ya takribani saa mbili, mgombea huyo wa CHADEMA, amesema ataimarisha uchumi wa nchi kwa kupanua wigo wa mapato ya serikali na hivyo kuongeza kiasi cha kodi kinachokusanywa.

Amesema kiasi cha sasa cha Sh. 400 bilioni kinachokusanywa na serikali kwa mwezi kinakusanywa kutoka katika kikundi kidogo cha watu wanaokamuliwa sana.

“Ni vitu viwili tu vinavyotakiwa. Kwanza , unatakiwa ubunifu wa kubaini vyanzo vya Kodi. Pili, nia ya kisiasa. Na serikali ya CCM haina nia ya kisiasa ya kukusanya kodi na haina ubunifu unaohitajika,” alisema.

Akitoa mfano amesema asilimia 75 ya kodi yote inayokusanywa nchini hutoka katika mkoa wa Dar es Salaam , jambo alilolisema kuwa si zuri kwa uchumi wa nchi.

“Kukusanya kodi si kitu kinachohitaji msaada kutoka nchi wahisani. Hili ni jambo ambalo sisi wenyewe tunaweza kabisa kulifanya iwapo kweli tuna uchungu na nchi yetu.

Alisema serikali ya CCM inatumia fedha nyingi na kuchochea rushwa kwa kuiharamisha gongo, wakati ingeweza kupata mapato zaidi kwa kuhakikisha kinywaji hicho kinatengenezwa kwa viwango vua kitaalamu.

“Wenyewe wamekazania kuongeza bei za vinywaji kama soda, bia na maji kila kukicha. Kama wakipunguza bei, watu watanunua kwa wingi na ajira zitaongezeka na uchumi utakua. CCM hawana fikra hizi. Hawana ubunifu kabisa,” amesema.

Amejitapa kwamba kwa “fedha nyingi” ambazo serikali ya Kikwete imetenga katika mpango wake wa “Kilimo Kwanza ” ingekuwa CHADEMA ndiyo iko madarakani, zingetosha kufuta kabisa njaa nchini.

Alitoa mfano wa ununuzi wa matrekta 1,400 kwa ajili ya mradi wa Kilimo Kwanza katika nchi kubwa kama Tanzania , wakati fedha nyingi zikielekezwa kulipa posho na gharama nyingine zisizo na lazima za watendaji wa serikali.

Dk. Slaa amesema kutokana na kile alichoita kutokuwepo mipango thabiti, leo serikali inaagiza mchele kutoka Japan, wakati bonde la Rufiji pekee, mkoani Pwani, linaweza kuzalisha mpunga unaotosha kulisha taifa zima na kuwa na ziada kwa biashara na ujenzi wa urafiki na nchi zinazozongwa na njaa.

“Japan yote kwa ukubwa inalingana na Bonde la Rufiji. Sasa inakuwaje nchi ndogo kiasi hicho, iwe inafadhili kwa chakula taifa kubwa kama Tanzania ,” alihoji.

Mwanasiasa huyo anayesifika kwa msimamo wake usioyumba wa kutetea maslahi ya nchi, anasema, “CCM haina lolote la kujivunia, badala yake, chama hicho kinapaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa kuwafanya maskini.”

Amesema, “CCM inaweza kujisifu kwa wizi wa fedha na rasilimali za nchi, na siyo katika kuleta maendeleo. Badala ya kujisifu kwa kusema amefanya hiki na kile, ni heri Kikwete angewaomba radhi Watanzania kwa maisha magumu aliyowasababishia tangu apate madaraka.

“Katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wa Kikwete, mabilioni ya shilingi yameibwa ndani ya serikali. Haya na mengine tutayaeleza mara tutakapoanza kujinadi kwa wanachi,” alisema.

Amesema, “Sisi wapinzani walau tuna kitu cha kuonyesha; yeye hana lolote. Kama akiomba radhi Watanzania, tunaweza kusema anaweza akashindana na sisi, lakini katika hali ya sasa, hana haki hiyo.”

Kuhusu vita dhidi ya ufisadi, Dk. Slaa anasema atakapoingia madarakani, atapambana na ufisadi kwa nguvu zake zote kwa kuwa ni vigumu kuleta maendeleo bila kupambana na ufisadi.

“Ufisadi umerudisha nyuma maendeleo ya taifa. Na ili kupata maendeleo ya kweli ni lazima ufisadi utokomezwe,” alisema kwa sauti ya uchungu.

Kuhusu matamshi yake ya siku za awali kwamba “hata angepewa bure urais asingekubali,” Dk. Slaa alisema kauli hiyo ilichochewa na hali halisi iliyopo nchini.

“Nchi hii ina shida nyingi sana. Katika hali hii, huwezi kukimbilia ikulu. Kufanya hivyo, ni kutafuta laana. Nimezunguka katika wilaya zote nchini. Nimeona umasikini wa kutisha.

Huduma za kijamii ni mbovu. Akinamama wamebakwa wakiwa njiani kusaka maji visimani. Kwa mtu mwenye busara hawezi kukimbilia ikulu,” amefafanua.

Amesema, “Hata baada ya kushawishiwa na wenzangu niwanie urais, niliwaambia twendeni kwanza kwa wananchi nikajue kama nao wananitaka. Ndiyo msingi wa kutembelea nchi mzima na kufanya mikutano ile ya kutafuta wadhamini,” anaeleza.

Kuhusu uhusiano wake na Kanisa Katoliki ambalo aliwahi kulitumikia kama Padri, Makamu wa Askofu na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Dk. Slaa anasema, “Nimefanya kazi kwa ajili ya Watanzania na sina udini.”

Amesema, “Mimi niliwahi kuwemo katika Kamati ya Kitaifa ya Kumshauri Rais kuhusu mambo ya dini. Ndani ya kamati hiyo tulikuwapo Wakristo na Waislamu.

Mimi nilikuwa mratibu wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakitaka kuanzisha Kitivo cha Filosofia. Watu wa dini zote wanasoma pale.

“Wakati nilipotoa orodha ya mafisadi na kupambana na ufisadi kupitia Bunge la Jamhuri, hakuna aliyesema kwamba mimi ni mbunge wa Wakatoliki. Iweje leo nisemwe mie mgombea wa Kanisa? alihoji Dk. Slaa.

Dk. Slaa anasema ndani ya siku 100 tangu CHADEMA iingie madarakani, serikali itaanza mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya, ambao utashirikisha makundi yote ya Watanzania.

Kuhusu ukubwa wa serikali, Dk. Slaa amesema, “nikiingia madarakani, kazi yangu ya kwanza itakuwa kupunguza ukubwa wa serikali ikiwamo baraza la mawaziri.”

Amesema ataweka mfumo imara, ikiwamo kuingizwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, idadi ya mawaziri wanaopaswa kuwapo katika serikali yake na zile zitakazofuata.

“Haiwezekani kila kiongozi akija anateua tu mawaziri anaowataka. Tunapaswa kuwa na idadi inayojulikana ya wizara na mawaziri kikatiba. Hili litapunguza uteuzi wa kujali ushikaji badala ya uwezo,” amesisitiza.

Akizungumzia ununuzi wa magari ya kifahari ambayo yametapakaa ndani ya serikali na taasisi zake, Dk. Slaa amesema, serikali yake itakuwa na magari machache kwa ajili ya matumizi muhimu ya serikali, na kwamba fedha zitakazookolewa zitapelekwa katika miradi ya maendeleo.

“Kwa sasa gari moja la waziri aina ya Toyota Land Cruiser VX (Shangingi) lina thamani inayokaribia kiasi cha Sh. milioni 200, kiasi kilicho sawa na ujenzi wa zahanati nne,” amesema kwa msononeko.

Mahojiano kamili na Dk. Slaa yatachapishwa katika gazeti hili toleo lijalo

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: