Dk. Slaa atishia Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi

VIGOGO wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wameokoa kampeni za uchaguzi kwa kukataa kuingia katika malumbano yanayohusu maisha binafsi ya wagombea, imefahamika.

Kwa nyakati tofauti, katika mahojiano na gazeti hili, vigogo hao wamesema wana jukumu moja, “kuondoa nchi hii mikononi mwa mafisadi.”

Tangu Dk. Slaa atangaze kugombea urais, jambo ambalo lilibadili mkondo wa siasa nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeelekeza baadhi ya magazeti kuendesha “kampeni ya uchafuzi” dhidi ya Dk. Slaa.

Kampeni hiyo ni ya kurudiarudia taarifa, kwa wiki nzima sasa, kuwa mgombea urais wa CHADEMA “ametelekeza” mke wake na kuchukua mke wa mtu,” mambo ambayo Dk. Slaa amepuuza.

Kwa mujibu wa vigogo hao, CHADEMA wana taarifa nyingi, walizopelekewa na wafuasi, wapenzi na mashabiki wao, zinazohusu maisha ya kashfa ya viongozi wakuu wa serikali na CCM.

Miongoni mwa taarifa ambazo mwandishi huyu ameona zinahusu utitiri wa watoto wa viongozi wakuu kwa mama tofauti; mahawala wa ndani na nje ambao huingizwa katika misafara ya kiserikali nchi za nje na akina mama waliotelekezwa na watoto wao.

Miongoni mwa taarifa zilizopo ni ushahidi wa vinasa sauti za mabinti wa umri mdogo na waajiriwa serikalini, taasisi za umma na katika CCM, wanaokiri kuwa na uhusiano wa ngono na viongozi wakuu.

Asasi moja ya akina mama inayofanya shughuli zake mjini Arusha na Dar es Salaam ndiyo imefanya uchunguzi wa kina na kuandaa taarifa za maandishi na sauti “kwa wanaotaka kuzitumia.”

Kiongozi mmoja wa CHADEMA ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, amekiri kuona nyaraka hizo na kudai kuwa zimejaa kila aina ya taarifa juu ya viongozi wa ngazi mbalimbali.

Lakini Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alipoulizwa iwapo chama kinajua kuwa kuna taarifa za aina hiyo, alisema, “Tunajua.”

Mbowe alisema, “Kukaa kwetu kimya hakuna maana kwamba hatujui mambo binafsi ya viongozi wa CCM na serikali yao, akiwamo Rais Kikwete. Tunajua.”

Akiongea kwa msisitizo, Mbowe ambaye alikuwa akihojiwa ofisini kwake jijini Dar es Salaam alisema, “Tunajua sana.”

Alipotakiwa kueleza iwapo chama chake kitazitumia kukabiliana na kampeni chafu ya CCM, Mbowe alisema, “Tunaamini kwamba majukwa ya siasa huwa yanatumika kunadi sera, si kunadi maisha binafsi ya mgombea.”

Alisema hawataki “watu hawa” wawatoe katika hoja ya wizi wa fedha za umma zilizokwapuliwa katika mabenki na serikalini na kuwapeleka katika hoja juu ya mtu binafsi.

“Tunawataka CCM wajibu hoja, badala ya kukimbilia katika maisha binafsi ya Dk. Slaa,” aliasa.

Alisema chama chake kinapinga tabia ya viongozi wa serikali kushawishi na “kununua watu” kwa shabaha ya kuwatumia kuunda vitaarifa vya kuhalalisha matakwa yao.

Aidha, alisema CHADEMA inalaani kitendo cha kutumia vyombo vya habari, vikiwamo vya umma, kusambaza taarifa zenye lengo la kuondoa wananchi kwenye mambo yanayohusu maisha yao.

Mbowe alisema chama chake kimeamua “kufanya kampeni za kistaarabu, ambazo hazizungumzii masuala binafsi ya mgombea.”

Naye Dk. Slaa akihojiwa kwa njia ya simu kutoka mjini Singida juzi Jumatatu alisema, “Sina muda wa kujibu mambo madogo kama hayo. Naelekeza nguvu zangu katika kampeni za kuondosha utawala wa CCM ulioshindwa.”

Wakili mashuhuri Mabere Marando, naye alizungumzia taarifa juu ya nyaraka nyingi zinazoanika tabia na mwenendo wa viongozi serikalini.

Akiongea jijini Dar es Salaam juzi, Marando alisema kwa taarifa zilizopo, tuhuma wanazomtwisha Dk. Slaa ni kidogo sana ikilinganishwa na nyaraka walizokusanyiwa.

“Tunao ushahidi wa kutosha. Wakiendelea kutusumbua, nitawashauri CHADEMA wachukue hatua na hapo asiwepo wa kutulaumu. Sasa tunawavutia pumzi,” ameeleza Marando.

Taarifa zilizopatikana wakati tukienda mitamboni zimesema Aminiel Mahimbo, anayedaiwa kuwa mume wa Josephine Mushumbusi alikuwa na mpango wa kwenda mahakamani kudai kuwa Dk. Slaa amechukua mke wake.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wa gazeti hili, Mahimbo ametafutwa na CCM kwa udi na uvumba kwa maelekezo ya Katibu Mkuu Yusuf Makamba, ili kukamilisha “mradi” wao dhidi ya Dk. Slaa.

“Mengine sasa utafute mwenyewe na kuthibitisha; lakini naambiwa kuwa CCM wamemtafuta, kumpa gari, kumkodishia hoteli na kumhakikishia kulipa gharama za wakili, ilimradi ijulikane amempeleka Dk. Slaa mahakamani,” kimeeleza chanzo chetu.

Mwandishi huyu aliwasiliana na Mahimbo kupata maelezo ya upande wake na yafuatayo ni sehemu ya majadiliano kati yao.

Mwandishi: Tuna taarifa kwamba ulikutana na Yusuf Makamba wiki iliyopita na akakupa maelekezo juu ya hayaa unayofanya.

Mahimbo: Hayo mambo siyajui.

Mwandishi: Mbona kuna madai kuwa ulitengana na mkeo miaka mitatu iliyopita; kwa nini unaibuka leo?

Mahimbo: Hayo muulizeni yeye.

Mwandishi: Makamba amekupa gari na amegharamia ukae hotelini…

Mahimbo: Sijui…(akakata simu).

Naye Josephine ambaye anakata mbuga na “wapambanaji” wa CHADEMA alipoulizwa juu ya sakata hilo amesema, “Najua kinachoendelea. Haya yote yameibuliwa na wapinzani wa kisiasa wa Dk. Slaa. Nawafahamu hata kwa majina.”

Josephine anakiri kuwa alikuwa ameoana na Mahimbo lakini hawako pamoja kwa miaka mitatu sasa.

Amesema kwa ufupi, kwa njia ya simu kutoka Singida, kuwa kama wewe ni mwanamme na unakaa miaka mitatu bila kumuona mkeo, na katika kipindi chote hicho huchukui hatua, “basi wewe una matatizo.”

Juhudi za kumpata Makamba kujibu maswali kadhaa hazikufanikiwa. Alikuwa aulizwe iwapo ni yeye anayesimamia “mradi wa “kuchafua” Dk. Slaa.

Alikuwa aulizwe pia juu ya tuhuma kuwa ni kupitia kwake, gazeti moja lilipata fedha za kuchapisha toleo moja lenye taarifa zinazohusu Dk. Slaa na kugawiwa bure.

Swali jingine lililolenga Makamba lilihusu wafadhili wengine wa mradi huu ambako taarifa zinamtaja mfanyabiashara Rostam Aziz na Abdulrahman Kinana, mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya mgombea wa CCM.

Si Rostam wala Kinana aliyepatikana kuzungumzia ushirika wao.

Hata hivyo, MwanaHALISI linaweza kuthibitisha kuwa mmoja wa wahariri wa gazeti lililochapisha tuhuma dhidi ya Dk. Slaa, alikutana na Makamba, makao makuu madogo ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam siku mbili kabla ya gazeti kuchapishwa.

Taarifa zinasema miongoni mwa makubaliano kati ya mhariri na Makamba, ni kugharamia uchapishaji na baadhi ya gharama za uendeshaji wa gazeti.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: